Wednesday, 23 September 2015

ANNE KILANGO ACHARUKA, AAPA KUPAMBANA NA WABAKAJI



WILIUM PAUL, SAME
MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Same Mashariki, kupitia CCM, Anne Kilango Malecela, ameahidi kuwa atatokomeza vitendo vya ubakaji watoto vinavyoshamiri katika jimbo hilo.
Anne Kilango ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni, uliofanyika katika Kata ya Maore, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Alisema vitendo vya ubakaji watoto ni vya kinyama na vimekuwa vikikua kwa kasi.
Anne alisema endapo wananchi watamchagua kuwatumikia tena kwa miaka mitano, atahakikisha kuwa vitendo hivyo vinakuwa historia katika jimbo hilo kwa kuwachukulia hatua  wote watakaofanya vitendo hivyo.
“Wananchi wengi mmekuwa mkiumizwa kwa kutojua sheria, mtoto wako anabakwa na mtuhumiwa akifikishwa mahakamani anaachiliwa sasa, nataka sote tuungane kwa pamoja kwa kushirikiana na Tume za Haki za Binadamu, ili kuhakikisha kuwa wale wote watakaogundulika kufanya kitendo hiki wanawajibishwa,” alisema.
Mgombea huyo ambaye ameliongoza jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 15, ambapo katika kipindi chote hicho aliwaletea maendeleo  wananchi wake, ikiwemo afya, elimu, miundombinu ya barabara na juhudi zake za ujenzi wa kiwanda cha kusindika tangawizi.
Anne alisema wakati analichukua jimbo la Same Mashariki lilikuwa  limejifunga sana, ukilinganisha na utajiri unaopatikana katika jimbo hilo, lakini kupitia juhudi zake na serikali sasa mambo mengi yamefunguka.
 “Jimbo letu ni tajiri, lakini tatizo kubwa lilikuwa ni barabara, kwani magari yalikuwa hayapitiki na kuwafanya wananchi wa jimbo hili wanaofanya kazi za kilimo cha tangawizi na mpunga kushindwa kufikisha sokoni,” alisema Anne.
Alisema mpaka sasa amepigana kuhakikisha kuwa barabara zinajengwa na magari yanaweza kupita, ambapo alifanikiwa kwa asilimia 80.
Akizungumzia kuhusu barabara ya Mkomazi yenye urefu wa kilomita 96, imepitishwa  na kuwa barabara ya mkoa, ambapo imetengewa sh. bilioni 77.
Alisema barabara hiyo inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ndiye rais ajaye, kwani ameteuliwa na Mungu na ndio maana katika kipindi cha mchujo jina lake halikuvuma sana.
“Ndugu zangu kumbukeni kuwa kiongozi anatoka kwa Mungu, hebu kumbukeni katika kipindi cha kumpata mgombe urais mlikuwa mkisikia jina la Magufuli?lakini yeye ndiye aliyeshinda, ina maana Mungu ndiye kamteua kuwa rais hata wapinzani wanalijua hilo,” alisema
Alisema katika kipindi chote Dk. Magufuli alipokuwa waziri katika  wizara mbalimbali, hajawahi kupata tuhuma zozote chafu, hivyo wananchi wanapaswa kumpa kura zote za ndio ambapo kazi yake ya kwanza kama watampa ridhaa ni kupambana na mafisadi wote.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Maore, Hamadi Sempombe, alisema kuwa vijana wamekuwa wakitumika sana na wanasiasa wapinzani kuhakikisha kuwa wanavunja amani ya nchi  na kuwataka kutodanganyika na viongozi hao.
Alisema badala yake wapinzani wamekuwa  wakisimama majukwaani na kusema kuwa CCM haijafanya kitu, hivyo aliwataka wananchi kutoyaamini maneno yao

No comments:

Post a Comment