Thursday, 24 September 2015
DK MAKAIDI MAJI YA SHINGO UKAWA
HATIMAYE ubinafsi na tamaa ya madaraka umeendelea kuzua mtafaruku ndani ya vyama vinavyounda kundi la UKAWA, baada ya Mwenyekiti Mwenza wa kundi hilo, Dk. Emmanuel Makaidi, kutoswa rasmi ndani ya UKAWA.
Dk. Makaidi, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha NLD na mgombea ubunge wa Jimbo la Masasi Mjini, amejikuta akisusa kuendelea na mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, baada ya kukataliwa kutambulishwa kama mgombea pekee wa ubunge kupitia UKAWA.
Kwa mujibu wa makubaliano ya vyama hivyo, Makaidi kupitia chama chake cha NLD, kilipewa majimbo matatu likiwemo la Masasi, lakini vyama vya CUF na CHADEMA vimesimamisha wagombea wao kinyume na makubaliano.
Hatua hiyo imesababisha kuwepo kwa mtafaruku ndani ya jimbo hilo uliosababisha kuvunjika kwa mkutano huo uliofanyika juzi, jimboni humo.
Kuvunjika kwa mkutano huo kulitokana na madai ya viongozi wa CUF na CHADEMA kumkataa Dk. Makaidi kuwania nafasi ya ubunge.
Kabla ya Lowassa kuhutubia wafuasi wa UKAWA, inadaiwa kuwa kundi la vijana liliandaliwa na baadhi ya viongozi wa UKAWA kupinga uamuzi wa kumtangaza Makaidi.
Mpango huo unadaiwa ulikuwa ni sehemu ya mkakati wa CUF na CHADEMA kutaka nafasi hiyo ichukuliwe na Ismail Makombe ‘Kundambanda’ kupitia CUF.
Wakati mkutano huo ukiendelea, zilisikika sauti kutoka kwa watu wakisema kuwa hawamtaki Dk. Makaidi.
Ilipofika zamu ya kutambulishwa kwa viongozi wa jukwaa kuu, zomeazomea ilianza baada ya kutajwa kwa jina la Dk. Makaidi.
Wafuasi wa UKAWA waliokuwa kwenye mkutano huo, walikataa kiongozi huyo ahutubie kwenye mkutano huo huku wakipaza sauti wakiimba ‘tunamtaka Kundambanda’.
Baada ya kuona kelele za wananchi hao zinazidi, ndipo Meneja Kampeni wa CHADEMA, John Mrema, alipowataka wafuasi hao watulie na kwamba Dk. Makaidi atazungumza kama Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na si kama mgombea wa nafasi ya ubunge jimboni humo.
“Makamanda tulieni namleta mzee Makaidi asalimie wananchi wa Masasi kama Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA…naomba tumheshimu kwa nafasi aliyonayo na hamna uwezo wa kumkataza kuongea ila mnao uwezo wa kumkataa kuwa mbunge wenu, hivyo naomba mtulie tumsikilize,” alisema Mrema.
Mrema alifanikiwa kulituliza kundi hilo, ambapo Dk. Makaidi alisema lengo la uchaguzi ni kupata viongozi bora na si bora viongozi, na kwamba wanapaswa kuchagua mbunge mwenye elimu ili aweze kuwaletea maendeleo ya kweli.
Kauli hiyo ya neno ‘elimu’ ilizusha tafrani kubwa ambapo wafuasi wa UKAWA walidai ni kejeli, kashfa na dharau ambayo ilimlenga Kundambanda, ambaye elimu yake ni ya darasa la saba.
Kundi hilo liliendelea kuzomea huku wakimtaka Dk. Makaidi aache kipaza sauti na ashuke jukwaani.
Makaidi alikiacha kipaza sauti kwa hasira na kumwachia mkewe, Modesta Makaidi, ambaye anawania ubunge katika Jimbo la Lulindi.
Baada ya zomeazomea hiyo iliyodumu kwa muda wote mkutanoni hapo, ilimlazimu Lowassa kumtaka Dk. Makaidi akubali kumwachia jimbo hilo Kundambanda au wote wasimame kwa tiketi ya vyama vyao.
Katika mkutano huo, viongozi wa UKAWA walimtaka Dk. Makaidi akubali ombi hilo licha ya mgawanyo wa UKAWA kuonyesha kuwa majimbo ya Lulindi, Masasi na Ndanda ni ya NLD.
Katika kudhihirisha mpango wa UKAWA kumkacha Dk. Makaidi, Lowassa alimsimamisha Kundambanda jukwaani kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni kumtosa Makaidi.
Akiwa amemshika mkono Kundambanda, Lowassa alisema: “Kwa hapa tulipofikia nakuomba mzee Makaidi umwachie huyu kijana hili jimbo.”
Mgogoro huo ni wa muda mrefu ambao ulizusha tafrani hata siku aliyofika mgombea mwenza wa CHADEMA Juma Duni Haji, jambo ambalo lilisababisha kuvunjika kwa mkutano wa kampeni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment