Thursday, 24 September 2015

WATAKUBALI TU

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, Joseph Msukuma akihutumia mkutano wa kampeni wa mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, uliofanyika jana mjini Katoro
Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni katika mji wa Katoro


Na Charles Mganga, Geita

SHUGHULI katika Mji wa Geita na vitongoji vyake jana zilisimama kwa muda wakati mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, alipohutubia mkutano wa kampeni kuomba kura.

Mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Kalangalala mjini hapa, ulishuhudia umati mkubwa wa watu ambao ni wa kihistoria, uliojitokeza kumsikiliza mgombea huyo.

Huku akionekana mwenye furaha na afya imara, Dk. Magufuli alieleza kufurahishwa kwake na mapokezi makubwa na umati wa kihistoria uliojitokeza uwanjani hapo.

Haikuwa kazi rahisi kwa askari waliokuwa wakilinda usalama kutokana na umati huo kila mmoja kuwa na shauku ya kutaka kumuona Dk. Magufuli kwa karibu.

Maofisa wa CCM na kwa nyakati tofauti Dk. Magufuli mwenyewe alilazimika kuwasihi wananchi kuwa watulivu na kukaa kwenye maeneo yao ili kuhakikisha usalama wa kutosha unakuwepo mahali hapo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk. Magufuli aliwahakikisha wananchi kuwa, serikali yake itajali maslahi ya wanyonge na kuwainua kiuchumi.

Alisema anatambua matatizo ya Watanzania ni ndio sababu ya kuwania nafasi hiyo kubwa ili aweze kuwahudumia kikamilifu.

Aliwaasa kutokubali kudanganywa na wagombea ambao hawana dhamira ya dhati ya kuwatumikia na wanaoponda kuwa serikali haijafanya chochote wakati maendeleo makubwa yanaonekana.

Dk. Magufuli, ambaye aliwasili Geita akitokea Bukombe na kupokewa na umati mkubwa wa watu, pia aliwaongoza wananchi kuwazomea mafisadi ambao wamekuwa adui wakubwa wa maendeleo ya Watanzania.

Alisema mafisadi hao ni kikwazo kwa maendeleo na kwamba kamwe wasipewe nafasi ya kuongoza kwani wataliingiza taifa kwenye matatizo na kuwataka wananchi kuwakataa.

Alisema serikali yake haitakubali wachimbaji wadogo na Watanzania kunyanyaswa kwa kunyang’anywa maeneo yao.

Alisema watu wachache wenye tabia ya kuwaonea wachimbaji hao muda wao umekwisha na kwamba  hakuna atakayevumiliwa.

“Sitakubali wachimbaji wadogo kuchukuliwa maeneo yao baada ya kuyagundua.

Tutahakikisha maeneo ya wachimbaji  wanapewa wahusika hao wenyewe,” alisema

Kwa majibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015,  Dk. Magufuli alisema wachimbaji watawezeshwa kwa kapewa mikopo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Pia, wachimbaji hao watapewa vifaa bora kwa ajili ya uchimbaji madini na kuwawezesha kupata leseni za uchimbaji.

“Wale wanaodhulumu wachimbaji madini sitawavumilia, tutawawezesha (wachimbaji wadogo) waweze kunufaika na rasilimali za nchi yao,” alisema mgombea huyo wa CCM.

Mgombea huyo ambaye alikuwa njiani akitokea Kagera kwenda Geita, alisema maeneo ya uchimbaji dhahabu, yatatengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Ili kuthibitisha serikali ya awamu ya tano, imedhamiria kuwapa maisha bora wachimbaji, Dk. Magufuli alimuita mgombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Steven Masele kufafanua kilichomo kwenye Ilani ya Uchaguzi.

Masele ambaye ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alisema tayari maeneo kwa ajili ya uchimbaji madini yametengwa.

Alisema kuna maeneo yametengwa ya pori la Runzewe lililopo Tulawaka na kuahidi watanufaika nalo kwa majibu wa ilani.

Kuhusu barabara ya Ushirombo mpaka Bwanga kwa kiwango cha lami, alisema taratibu za kujenga zimeanza.

Kuhusu mazao ya pamba na tumbaku, Dk. Magufuli alisema atahakikisha bei zinapanda ili kuwanufaisha wakulima.

Alisema vitajengwa viwanda ambavyo vitasaidia kupandisha bei na kuwasaidia ajira vijana.

Akiwa Katoro, Dk. Magufuli alipokewa kama mfalme katika Uwanja wa Mnadani, kabla ya kuanza kuwahutubia na kisha kuwaomba kura wamchague awe rais wa awamu ya tano.

Magufuli alipokewa kwa msururu wa bodaboda zilizopambwa kwa bendera za CCM.

Kabla ya kuanza kupanda jukwaani, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Kusheku, maarufu kama Msukuma, aliendelea kuwahimiza wananchi wamchague Dk. Magufuli kwani ndiye chaguo sahihi.

Msukuma aliwaambia wananchi kuachana na ahadi hewa za mgombea wa UKAWA.

“Mimi namfahamu Lowassa kuliko mtu mwingine, nimempakia kwenye ndege yangu mwezi mzima, nawaambia vijana UKAWA ni genge la wasanii, halipaswi kusikilizwa.” 

Naye mgombea urais, alianza kwa kuwashukuru wakazi wa Katoro na Buseresere kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo.

“Leo Katoro na Buseresere mmefunika, mmetisha kabisa. Yaani umati wote huu halafu, niwasahau. asanteni sana ndugu zangu,” alisema.

Aliwaomba wampigie kura za urais na wamchague Lorencia Bukwimba kuwa mbunge ili waweze kuzitatua kero za Jimbo la Busanda.

Mbali ya Bukwimba, Dk. Magufuli aliwaomba wakazi wa Katoro nao wampe ushindi mkubwa, Dk. Merdad Kalemani awe mbunge wa Chato.

Hata hivyo, Dk Magufuli alisisitiza kuzimaliza changamoto za majimbo hayo na lile la Bukombe linalowaniwa na Dotto Biteko.

“Sipendi mnichanganyie, nichagulieni wabunge wa CCM na madiwani ili tufanye kazi,” alisema Dk. Magufuli.

 Aliwaahidi kuwatengenezea barabara yenye urefu wa kilomita saba. Mbali ya Bukombe na Katoro,  Dk. Magufuli alifanya mkutano Geita.

Staili ya ‘push up’ gumzo

Mara baada ya kumaliza kuzungumza mjini Geita, Dk. Magufuli alipokea wanachama wapya kutoka upinzani akiwemo aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA.

Pia, alikuwepo mlinzi aliyekuwa akitumiwa kwenye kikundi cha ulinzi cha Red Brigade, ambaye alisema kilichopo ndani ya CHADEMA ni usanii na uhuni.

Baada ya kazi hiyo umati huo ulipaza sauti ukimuomba Dk. Magufuli awaonyeshe jinsi ya kupiga ‘push up’. “Mnataka push up sio…” umati huo uliitikia ambapo Dk. Magufuli alimuita jukwaani mwanamuzi nyota wa hip hop Hamis Mwinyijuma au Mwana FA, na kuwaeleza kuwa ndiye atakayewaonyesha.

Akiwa jukwaani hapo, Mwana FA alisema wapo kwa ajili ya kumuunga mkono Dk. Magufuli, ambaye anakwenda kuwa Amiri Jeshi Mkuu, hivyo  suala la afya njema ni la muhimu.

Alisema kiongozi wa nchi hatakiwi kuwa na afya yenye utata na kwamba  hatua ya Dk. Magufuli kupiga push up inadhihirisha kuwa yuko vizuri na ndio sababu ya kumuunga mkono.

“Tuko hapa kumuunga mkono  Dk. Magufuli, ambaye anakwenda kuwa Amiri Jeshi Mkuu, hivyo  ameonyesha kuwa yuko ngangari na afya yake haina mgogoro. Kwa sababu hiyo basi mimi na kundi langu hapa tutapiga push up ili kumuunga mkono kiongozi wetu,” alisema na kuanza kutekeleza agizo hilo na kuamsha shangwe uwanjani hapo.

No comments:

Post a Comment