Thursday, 24 September 2015

UTAFITI WA TWAWEZA WAZUA GUMZO KILA KONA


NA MOHAMMED ISSA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakikushangazwa na matokeo ya utafiti wa Taasisi huru ya Twaweza, ambayo yanatoa ushindi wa asilimia 65 kwa Dk. John Magufuli, ambaye ni mgombea urais wa CCM dhidi ya Edward Lowassa wa CHADEMA.

Aidha, kimesema kinashangazwa na kauli iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, ambaye alidai CCM haijathibitisha kushiriki mdahalo wa wagombea.

CCM imesema mgombea wake, Dk. Magufuli amekubali kushiriki mdahalo huo wa wagombea urais na inasisitiza kuwa uwashirikishe wagombea wenyewe na si wawakilishi wao.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Januari Makamba, alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisi Ndogo za CCM za Makao Makuu zilizoko Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.

Alisema utafiti uliofanywa na Twaweza na matokeo yake kutangazwa juzi, ambayo yanatoa ushindi kwa Dk. Magufuli dhidi ya Lowassa wa CHADEMA, haujakishangaza Chama.

Utafiti huo unaonyesha kuwa, kama uchaguzi huo ungefanyika kati ya Agosti na Septemba, Lowassa angepata ushindi kwa kupata asilimia 25.

Januari alisema CCM haikushangazwa na matokeo ya utafiti huo kwa sababu tano.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni siku UKAWA walipomteua Lowassa kuwa mgombea wao, ndio siku CCM ilipohakikishiwa ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu.

Januari alisema Chama hakikumteua Lowassa kwa sababu kiliamini hakuna namna ambayo Watanzania watamchagua.

Alisema sababu ya pili ni kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, Chama kinafanya utafiti wa kisayansi kila wiki kufahamu mwenendo na mwelekeo wa kampeni na maeneo yanayohitaji nguvu mahususi.

“Tokea tuanze utafiti wetu Agosti, mwaka huu, kila wiki asilimia za ushindi wa CCM hazijawahi kushuka chini ya asilimia 60, na zimekuwa zikipanda,” alisema.

Alisema sababu ya tatu ni kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Dk. Magufuli na Samia kuzunguka nchi mzima kwa barabara na kuongea na wapigakura.

Januari, ambaye pia ni mjumbe wa timu ya ushindi ya CCM,  alisema sababu ya nne ni kampeni kubwa inayofanywa na wagombea ubunge na udiwani, makada na viongozi wa Chama katika ngazi zote nchini kila siku kumuombea kura Dk. Magufuli zinazaa matunda.

Alisema CCM kinaamini kuwa migogorio ndani ya UKAWA katika kipindi hiki cha uchaguzi, iliyosababisha mitafaruku katika kuachiana majimbo na kutokana na uteuzi wa Lowassa, yote hayo yamepunguza imani ya wananchi kuhusu uwezo wa vyama vya upinzani kushika dola.

Januari alisema CCM kimeyachukua baadhi ya matokeo ya utafiti huo na wanayafanyia kazi ili kujihakikishia ushindi.

Hata hivyo, alisema wameshangazwa na taharuki hasa kutoka miongoni mwa wasomi na wanaharakati kuhusu matokeo ya utafiti huo.

Alisema CCM ilitegemea kuwa jamii ya wasomi na wanaharakati ingefurahia utamaduni wa tafiti za kisiasa unaoanza kujitokeza hapa nchini.

Januari alisema Chama kinasikitika kuwa yamewekwa mazingira ya kutisha na kukatisha tamaa kwa watu wanaotaka kufanya tafiti za kisiasa.

“Utafiti ni sayansi, hivyo matokeo ya utafiti hupingwa kwa matokeo ya utafiti mwingine na si kuponda au kwa matusi. Ni vyema tukajifunza kupokea habari mbaya bila taharuki,” alisema.

Alisema Agosti, mwaka 2010, taasisi ya utafiti ya kimataifa ya Synovate ilitoa utafiti ikionyesha kuwa CCM itashinda uchaguzi mkuu mwaka huo kwa asilimia 61.

Januari alisema baadhi ya wana-CCM hawakufurahishwa na matokeo hayo kwa sababu waliamini ushindi wa Chama ni mkubwa zaidi.

Alisema wapinzani walilaani matokeo ya mwaka huo na kutaka kuishitaki taasisi hiyo, lakini kwenye matokeo halisi ya kura, CCM ilipata ushindi kwa asilimia hizo hizo 61.

Alisema Chama kinaridhika na mwenendo wa kampeni za uchaguzi mkuu na katika nusu ya pili ya kampeni kitaongeza kasi na msukumo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa mbinu na mikakati mipya.

Kuhusu kauli ya MCT, alisema Chama kilipokea mwaliko wa baraza hilo na kuujibu kwa barua ya Septemba 13, mwaka huu, yenye kumbukumbu CMM/OND/M/190/132, iliyotiwa saini  na Stephen Msami, ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM.

Alisema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alifanya kikao na wawakilishi wa MCT katika ofisi za Lumumba ili kufahamu zaidi na maoni ya Chama kuhusu utaratibu mzima wa mdahalo.

WANANCHI, WASOMI WAMPONDA MBOWE

MAKUNDI mbalimbali ya kijamii nchini yamesema kitendo cha CHADEMA kupendekeza Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kumwakilisha mgombea urais wao, Edward Lowassa, kwenye mdahalo wa wagombea urais ni ishara ya woga na kutojiamini.

Kauli hiyo ilitolewa jana kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja tangu kamati ya maandalizi ya mdahalo huo kupitia kwa Mwenyekiti wao, Kajubi Mukajanga, kusema imesononeshwa na kitendo cha baadhi ya vyama kutothibitisha ushiriki huku CHADEMA wakipendekeza mbadala wa Lowassa.

Mkufunzi wa Sayansi za Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Joseph Ngwiliza, alisema mdahalo ni fursa nzuri kwa mwananchi kutanua uelewa wake juu ya sera na misimamo ya chama na mgombea hivyo kupanua wigo wa uamuzi wa kuchagua.

Alisema ni jambo la kushangaza kutokana na kwamba kiitifaki mdahalo huo umewalenga wagombea wa nafasi ya juu ya uongozi wa nchi wanaotarajiwa kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano huku Watanzania wakitarajia mabadiliko makubwa katika kila sekta.

Profesa Ngwiliza alisema kitendo cha CHADEMA kujitokeza na kusema hawako tayari kumruhusu Lowassa, badala yake achukue nafasi Mwenyekiti wa chama au Katibu Mkuu ni woga kutokana na ugeni wa mgombea juu ya sera za chama chao.

Alisema ni wazi kuwa viongozi wa CHADEMA wanaogopa mgombea wao hana uelewa thabiti wa sera za chama husika, hivyo anaweza kusema suala ambalo linakinzana na chama chao, hivyo kupoteza matumaini ya upande huo kuingia Ikulu kwa mwaka huu, jambo wanaloliamini mpaka sasa.

Mhadhiri huyo aliongeza kusema kuwa hakuna sababu ya kuogopa mdahalo au maswali kwa mgombea mwenye utayari wa kuiongoza nchi, kwa sababu litakalofanyika si kupambanisha vyama bali ni kutoa uhuru kwa wagombea husika kujieleza zaidi ya wanavyofanya kwenye majukwaa yao ya kampeni.

“Naamini kutakuwa na nafasi kwa wananchi kuuliza maswali, ni fursa kwa wagombea na wananchi kushirikiana kwenye kampeni tofauti na inavyofanyika kwenye majukwaa ya kampeni, hivyo hakuna sababu ya kuogopa kama mgombea yuko makini na analolifanya,” alisema.

Aidha, alisema sera ndio jambo muhimu ambalo Mtanzania anatakiwa kulisikia kutoka kwa wagombea na jinsi watakavyozitekeleza kwa muda husika, hivyo suala la kudhani mtu ndio kivutio cha watu kwenye upigaji kura linaweza kufutika baada ya mdahalo huo, jambo linalowatishia baadhi ya viongozi wa vyama.

Kwa upande wa wanafunzi wa elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini, walisema siasa za uchaguzi wa mwaka huu zimesheheni mizaha na maigizo, ambayo Watanzania wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wanapoteza kura zao kwa kumchagua mtu ambaye atakuwa mwiba kwa nchi.

Walisema midahalo ambayo awali ilizuiwa na serikali ni jambo jema kwenye maendeleo ya demokrasia, hivyo nafasi iliyotolewa ya kuwakutanisha wagombea urais wote wa uchaguzi mkuu mwaka huu, haitakiwi kufanyiwa maigizo na wanasiasa kwa sababu Watanzania wanaihitaji.

Fidelis John, mwanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, alisema kila chama kinatakiwa kujibu ushiriki wa mgombea wake kwenye kamati maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya mdahalo huo bila kukosa kwa sababu Watanzania wamechoka kuendeshwa na siasa za maigizo bali wanahitaji kusikia sera.

“Nilivyosikia nilishangaa, wewe umeambiwa tunamhitaji mgombea urais halafu unasema nitamleta Mwenyekiti au Katibu Mkuu…kweli ni halali? Kama sio sanaa hizo za mchana kweupe?” Alihoji mwanafunzi huyo.

Thomas Anyalwise, mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), aliwatahadharisha wananchi kujitambua na kuepuka kuendeshwa na siasa uchwara ambazo zimeonekana kushika hatamu kwenye kampeni za mwaka huu.

Wakazi wa Dar es Salaam nao walisema CHADEMA inapaswa kuacha kucheza na akili za Watanzania kwa sababu nyakati hizi wengi wameelimika na hawako tayari kuiweka Tanzania kwenye mikono isiyo salama, hivyo waheshimu maelezo yaliyotolewa na kamati ya maandalizi ya mdahalo huo.

Walisema dalili zinaonyesha kuwa mgombea urais wa CHADEMA anahofia uwezo wake wa kuzungumza kwa hoja jukwaani kutokana na mwenendo aliouonyesha mpaka sasa kwenye kampeni, ambapo amekuwa akizungumza kwa muda mchache kuliko kawaida.

Hii ni mara ya pili kwa Lowassa kutaka kukacha mdahalo kwa mwaka huu, tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu ambapo mara ya kwanza alihitajiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe na aliyekuwa Spika Dk. Samuel Sitta, waliomtaka azungumzie tuhuma zake kuhusu sakata la zabuni ya kampuni ya Richmond.

ACT- WAZALENDO YAUNGA MKONO UTAFITI


CHAMA cha ACT-Wazalendo kumeunga mkono utafiti uliotolewa na Taasisi ya Twaweza, ambao umeonyesha mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli, anaongoza kwa asilimia 65.

Pia, chama hicho kimesisitiza kuwa mgombea wa urais wa ACT,  Anna Nghwira, atashiriki mdahalo wa wagombea urais ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT)

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi na Kampeni, Nixon Tugara, alisema endapo maoni kutoka kwa wananchi yakikusanywa katika kipindi kilichobakia kabla ya uchaguzi mkuu, ACT kitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukubalika na wananchi.

Alisema utafiti huo umeonyesha namna ambavyo chama hicho kinavyokubalika kwa kutajwa na zaidi ya wapigakura asilimia moja licha ya kutofungamana na UKAWA.

Tugara alisema nafasi ya ACT kuwa chama cha nne kilicho karibu na Watanzania, inaonyesha namna ambavyo kinakubalika na matokeo hayo ni changamoto ya kuongeza juhudi.

Akizungumzia mdahalo kwa wagombea urais, msemaji wa chama hicho, Abdallah Khamis, alisema kimezingatia matakwa ya MCT kuhusu ushiriki wa wagombea urais kwenye mdahalo.

“Barua kutoka MCT ilitaka wagombea urais ndiyo washiriki kwenye mdahalo, hivyo kwenye mdahalo huo kwa mgombea urais wa ACT atashiriki,” alisema.

No comments:

Post a Comment