Saturday, 26 September 2015
WAZIRI CELINA KOMBANI AFARIKI, MWILI WAKE WAREJESHWA DAR KUTOKA INDIA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani amefariki dunia juzi jioni katika hospitali ya Appolo nchini India, alikokwenda kwa matibabu.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alisema Kombani alipelekwa nchini humo wiki tatu zilizopita.
“Ni Kweli amefariki dunia leo jioni (jana) ndiyo ninachoweza kusema kwa sasa,” alisema Dk Kashillilah kwa ujumbe mfupi bila kueleza waziri huyo alikuwa akisumbuliwa na nini.
Katika mchakato wa kura ya maoni ndani ya CCM, chama hicho kilimpitisha Kombani kuwa mgombea tena ubunge katika jimbo la Ulanga.
Waziri huyo alishiriki vikao vyote vya Bunge la Bajeti lililomalizika mwezi juzi mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2015/16.
Wasifu wa Celina Kombani
Celina Kombani alizaliwa Juni 19, 1959.
Alisoma katika Shule ya Msingi Kwiro mwaka 1968-1975, Sekondari ya Kilakala 1975-1978 na baadaye katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora kwa masomo ya juu 1979-1981.
Baada ya masomo ya elimu ya sekondari alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe 1982-1885 na kati ya mwaka 1994-1995 alisomea shahada ya pili ya uongozi katika Chuo cha Mzumbe.
Kabla ya wadhifa wake wa sasa ndani ya utumishi, Kombani aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi) 2008-2010, Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri Tamisemi, Ofisa Utawala mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Meneja wa Kiwanda cha ngozi Morogoro na ofisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Wakati huo huo, mwili wa marehemu Celina umerejeshwa nchini leo mchana kutoka India, ambako alifariki dunia juzi kwenye hospitali ya Appolo alikopelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mwili huo ulipokelewa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, ambao walionekana kuwa na majonzi makubwa huku baadhi yao wakishindwa kuyazuia machozi yaliyowatoka.
Baada ya kuwasili uwanja wa ndege, mwili wa marehemu Celina ulipelekwa nyumbani kwake Masaki kabla ya kupelekwa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, ambako utahifadhiwa kusubiri taratibu za mazishi.
Marehemu Celina anatarajiwa kuzikwa shambani kwake Ulanga mkoani Morogoro.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment