Thursday, 6 October 2016

JPM AWATUMBUA WATUMISHI WAWILI JNIA


NA MWANDISHI WETU

RAIS Dk. John Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha, kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wawili, kwa kumpa taarifa za uongo alipozuru uwanjani hapo kwa mara ya kwanza Mei, mwaka huu.

Agizo hilo alilitoa jana, alipofanya tena ziara ya kushtukiza kwenye sehemu ya kukagulia mizigo na abiria, baada ya kumsindikiza Rais wa DRC, Joseph Kabila, aliyekuwa akirudi nchini mwake, baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku tatu hapa nchini.

Kwenye ziara hiyo ya jana, Rais Magufuli alibaini kuwa mashine mbili za ukaguzi (Scanners) wa mizigo ya abiria upande wa terminal 1, zinafanya kazi tofauti na alivyoarifiwa na maofisa hao wawili Mei, mwaka huu.

Alisema katika ziara hiyo ya mara ya kwanza, ambayo aliifanya kwa kushtukiza, akitokea Kampala kwenye sherehe za kumuapisha Rais wa Uganda, Yoweri Museven, alifahamishwa na watumishi hao wawili kuwa mashine hizo ni mbovu baada ya kuwahoji.

Walimpa taarifa kwamba hazifanyi kazi kwa muda mrefu, huku moja kati ya hizo walidai haikutumika tangu ifike uwanjani hapo kwa sababu ilipelekwa kwa ajili ya kuhifadhiwa na ile ya pili vifaa vyake vimepelekwa nje ya nchi kwa matengenezo.

Dk. Magufuli alisema jana alipofika tena eneo hilo, alibaini kuwa mashine husika ni nzima na zinafanya kazi vizuri, baada ya kujionea mwenyewe uhalisia wa namna mizigo inavyokaguliwa katika eneo hilo.

“Leo kweli mashine zinafanya kazi na mimi nimeona, lakini wale walionidanganya mara ya kwanza nilipokuja, Mkurugenzi hakikisha unawachukulia hatua," aliagiza Dk. Magufuli na kuondoka.

Awali, kabla ya tukio hilo, Rais Magufuli alimuaga Rais Kabila, ambaye akiwa nchini, alifanya mazungumzo naye na kufanikiwa kufikia makubaliano ya kudumisha ushirikiano kwenye masuala mbalimbali, ikiwemo biashara, ambapo mkataba wa bomba la mafuta na gesi ulitiwa saini.

Pia, Rais huyo wa DRC, alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla na kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la kisasa la biashara ya pamoja (one stop centre), linalomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), ambalo pia ni refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati.

Viongozi wengine walioungana na Rais Magufuli kumuaga Rais Kabila ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, mawaziri na mabalozi wa nchi mbalimbali, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na viongozi wa dini.

No comments:

Post a Comment