Sunday 27 September 2015

NGELEJA APELEKA KILIO UKAWA




NA PETER KATULANDA, SENGEREMA
WANACHAMA wa CCM mjini hapa wameendelea kuselebuka kwa shangwe na kujihakikishia ushindi wa tsunami, baada ya wafuasi wengine 47 wa CHADEMA, akiwemo Katibu wa Kata ya Nyamazugo, Edward Prosper, kujiunga na CCM.
Prosper na kundi lake wanafanya idadi ya wafuasi wa CHADEMA na baadhi ya viongozi wake waliojiunga na CCM toka kampeni zizinduliwe Septemba 13, mwaka huu, wafikie 876 na kuwaweka katika hali ngumu wagombea wa UKAWA.
“Wazazi wetu tumerudi nyumbani kuwaunga mkono Ngeleja na Tingatinga Dk. Magufuli. Huko tulikokuwa ni kwenye saccos ya watu, tuliyoyaona na kujifunza ni kujengewa ujasiri wa kufanya fujo na vurugu, tumehofu tumepoteza muelekeo ndiyo maana mimi na vijana hawa 46 tumeamua kurudi,” alisema Prosper.
Kiongozi huyo wa zamani wa CHADEMA, alisema hayo kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM, uliofanyika katika Kata ya Nyamazugo wilayani Sengerema, mwishoni mwa wiki na kuanza kuselebuka wakiimba ‘CCM mbele kwa mbele’.
Akiwapokea wanachama hao wapya, mgombea wa ubunge jimboni Sengerema, William Ngeleja, alisema CCM ndicho Chama pekee nchini chenye demokrasi ya kweli, vingine vinaendeshwa kama saccos na magenge ya kusaka ulaji.
Aliwataka wananchi waliokusanyika kwenye mkutano huo, wakipe tena Chama ridhaa ya kuongoza taifa kwani kimepata jembe jingine bora (Dk. Magufuli).
Ngeleja aliwashukuru wananchi wa Nyamazugo na Bungonya kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo, na kusema iwapo watamchagua tena, baadhi ya vipaumbele vyake ni pamoja na ujenzi wa barabara za Kamanga-Sengerema na Sengerema Nyamazugo kwa kiwango cha lami.
Awali, akiwakaribisha wanachama hao wapya, Katibu Mwenezi wa CCM wilayani humo, Masumbuko Bihemo, alisema toka Chama chake kizindue kampeni zake Sepetemba 13, mwaka huu, Prosper na wenzake wanafanya idadi ya wafuasi wa Chadema waliojiunga na CCM kufikia 876 na kukihakikishia ushindi wa tsunami jimboni humo.
Bihemo alisema wafuasi wengine 46 wa Chadema, wakiwemo Mwenyekiti wa Kata na Tawi la Katunguru,  Faida Nzeyele na Slyicus Magege, walijiunga na CCM siku walipozindua kampeni katika Kata ya Katunguru  huku wengine zaidi ya 780 wakijiunga katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment