Thursday 6 October 2016

MO ASHINDA TUZO YA KIONGOZIBORA KIJANA AFRIKA


RAIS na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Mohamed Dewji ‘Mo”, ameibuka kidedea, baada ya kutangazwa kushinda tuzo ya Kiongozi Bora Kijana wa Biashara Afrika.

MO, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo na  Taasisi ya Choiseul 100 Afrika, yenye makao makuu jijini Paris, Ufaransa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam, jana, ilisema Choiseul 100 Afrika, imetoa tuzo hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo, orodha yake ya viongozi vijana wenye ushawishi katika biashara barani humu, ijulikanayo kama ‘Choiseul 100 Africa: Viongozi wa Uchumi wa Kesho.

Tuzo hiyo hulenga kutambua wafanyabiashara wenye ushawishi na kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Afrika na ambao ni mfano wa kuigwa kwa ajili ya ufufuo wa bara hilo.

Katika orodha ya mwaka huu, MO ameshika nafasi ya kwanza kati ya viongozi vijana wa kibiashara 100.

Kwa miaka kadhaa, Choiseul imekuwa kichocheo cha kuleta mabadiliko makubwa, kukua kwa fursa na vipaji barani Afrika.

Ilisema utambuzi wa MO katika tuzo hiyo, unatuma ujumbe mkubwa wa matumaini kwa Tanzania na Afrika kuwa, bara hili linazidi kujihusisha katika kuchochea ukuaji wake na watu wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanaoingia katika Choiseul 100 AfriKa ni wenye sifa maalumu, ikiwemo kuwa na utaifa katika moja ya nchi 54 za Afrika, umri wa miaka 40 au chini ya hapo hadi kufikia Januari, mwaka huu na mchangiaji mzuri wa maendeleo ya uchumi Afrika.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dewji alisema: “Nimepata heshima kubwa na nina furaha kupokea hadhi hii kwa kutambua kazi, ambayo nimekuwa nikiifanya barani Afrika.

“Katika safari yangu yote ya ujasiriamali, nimekuwa nikiendelea kuboresha ubora katika tasani ya biashara. Kupitia MeTL, nitaendelea na dhamira yangu ya kuiendeleza Afrika kupitia sekta binafsi.”

Dewji anahusika na kuiongezea mapato MeTL kutoka Dola za Marekani milioni 30 hadi bilioni 1.3, kati ya mwaka 1999 na 2014.

Watanzania wengine waliochomoza katika tuzo hizo mwaka huu ni Elsie Kanza, Mkuu wa Afrika wa Jukwaa la Uchumi wa Dunia (WEF),  Luca Neghesti, Mwasisi wa Bongo 5 Media Group, Edha Nahdi, CEO wa Amsons Group na Moremi Marwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

No comments:

Post a Comment