Friday, 14 October 2016

HOTUBA YA RAIS MSTAAFU MKAPA SIKU YA MAZISHI YA KITAIFA YA MWALIMU NYERERE


RAIS Benjamin Mkapa amesema kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kimeonyesha kuanza kwa maisha mapya yenye ishara kwamba Watanzania watadumisha mshikamano.

Akihutubia wananchi na wageni kutoka nje ya nchi, wakiwemo wakuu wa nchi walioshiriki katika mazishi ya kitaifa ya Mwalimu Nyerere, kwenye  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Oktoba 21, 1999, Rais Mkapa alisema:

"Nimebahatika kuongoza msafara wa mazishi ya mtu huyo na kiongozi wa pekee katika mitaa ya Dar es Salaam. Nimeelemewa na huzuni na majonzi ya Watanzania kila tulikopita. Lakini nilipewa matumaini na maneno ya wananchi na yale yaliyoandikwa kwa mkono kwenye mabango, yakiapa kulinda uhuru, utulivu, umoja, mshikamano, hali ya kuvumiliana na misingi yote aliyotufundisha Mwalim katika uhai wake wote.

"Napenda nimthibitishie kila mtu, ndani na nje ya Tanzania kuwa, serikali yangu itahakikisha kuwa urithi wa Mwalimu haupotei kamwe,"alisema.

Rais Mkapa alisema kila lililo ndani ya uwezo wa Watanzania, litafanywa ili kudumisha umoja wa kitaifa, upendo, mshikamano na maelewano.

"Kwenu Watanzania wnzangu, ninazo shukurani tele pia. Tarehe 26, Septemba, niliwaelezeni maradhi yaliyokuwa yakimsumbua Baba wa Taifa, nikawaombeni kila mtu kwa imani yake amwombee apone upesi. Na kweli nchini kote, katika dini na kabila zote, maombi yalifanywa usiku na mchana,"alisema.

Mkapa alisema japokuwa Mwalimu hayupo, lakini nchi nzimainaungana tena bila kujali kabila, dini, jinsia au rangi kuomboleza kifo chake kwa umoja, amani na utulivu kama alivyotufundisha Mwalimu katika uhai wake na kuwa hali hiyo ni dalili nzuri ya kuhitimu yale aliyotufundisha Baba wa Taifa na ni mwanzo mzuri wa maisha bila Mwalimu.

Katika hotuba yake, ambayo ilikuwa ikizikilizwa kwa makini na wakuu wa nchi na umati mkubwa uliofurika uwanjani hapo tangu mapema asubuhi, Mkapa alisema pia kuwa vita dhidi ya umasikini vitaendelezwa kwa bidii zaidi na kuhakikisha matunda ya jitihada hizo yanawafikia wengi kwa haki na usawa, ikiwemo wanyonge katika jamii.

Suala lingine ambalo  Rais Mkapa alisisitiza ni kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, aliouasisi akishirikiana na hayati Sheikh Abeid Amani Karume, utalindwa kwa nguvu zote.Karume aliuawa kwa kuigwa risasi na wapinga mapinduzi Aprili 7, 1972.

"Tusisahau ndugu zangu kuwa, heshima kubwa ambayo Mwalimu alikuwa nayo duniani ndiyo iliyowaleta kuungana nasi katika majonzi, viongozi wengi kiasi hiki kutoka nchi jirani na bara zima la Afrika, kutoka Ulaya, Amerika na Asia. Kweli wamekuja kutoa heshima zao za mwisho kwa Mwalimu, lakini pia kwa kuja kwao, wanatuhimiza tuwe warithi waadilifu watakaoendeleza yale yote aliyoyafanya Mwalimu hatayakampa umaarufu,"alisema Rais Mkapa.

Rais Mkapa alisoma baadhi ya sehemu za salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi, mojawapo ikiwa ni ile ya Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi Afrika (OAU), na Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouateflika, ambayo ilisema ifuatavyo kuhusu Mwalimu:

"Hakuna kiongozi mwingine wa kulinganishwa naye, aliyetoa maisha yake kutumikia nchi yake na bara lake, mtetezi asiyechoka kwa kila lililo la haki na anayestahili kuitwa mwasisi wa ushindi wa Waafrika kuwa mataifa huru miongoni mwa mataifa ya dunia."

Kwa niaba ya Jumuia ya Kimataifa, alinukuu sehemuya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, aliyesema ifuatavyo kuhusu Mwalimu:

"Aliweka mfano katika Afrika wa kuachia madaraka kwa hiari na kuyakabidhi kwa aliyerithi madaraka hayo kwa utulivu na kuzingatia Katiba."

Akinukuu salamu za Shirika la Kimataifa la Elimu na Watoto (UNICEF) katika salamu zake za rambirambi, lilimwelezea Mwalimu kama:

"Mtu mwembamba, wa maungo madogo, mwenye kicheko kinachoambukiza na akili yenye makali ya kukata hadi katika moyo wa kila hoja na ulimi mwema kiasi cha kutuliza roho ya kila mpinzani wake."

Katika hotuba yake, Rais Mkapa alielezea jambo, ambalo katika miaka ya hivi karibuni, Mwalimu alikuwa akilipigania kwa dhati kuwa ni kutatua mgogoro wa Burundi, ambao alisema pamoja na hatua ile ya ugonjwa, alitaka aendelee na kazi yake ya usuluhishi.

"Hakika alikuwampatanishi mkubwa, zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu, ambayo nasi tunaweza kuitoa ni kuharakisha na kukamilisha mazungumzo ya amani ya Burundi na kisha kuisaidia kuwarejesha wakimbizi wa Burundi makwao,"alisema.

Akimwelezea zaidi Mwalimu, Rais Mkapa alisema alikuwa mwalimu wa mengi. Alikuwa na kiu isiyokatika ya kujua mambo, hamu isiyoisha ya kuwapa wengine ufahamu wa mambo. Mtu mvumilivu, msikilizaji makini na siku zote alikuwa radhi kutilia maanani mawazo ya aina nyingi ya wengine.

"Mwalimu alikuwa na kipaji cha kuona mbali, mtu mwenye ucheshi na akili kupindukia. Alikuwa mtu mwenye taamuli, mwenye tafakuri asilia na bunifu. Siku zote alichajishika na fikra mpya, akavutiwa na kutafuta ukweli wa mambo katika sayansi na historia," alifafanua Rais Mkapa.

"Dunia yetu ina watoaji na wapokeaji. Wapokeaji wanaweza kula vizuri, lakini watoaji wanalala vizuri zaidi. Katika kifo, kama ilivyo katika uhai, Mwalimu alilala na ataendelea kulala vizuri, Maana, maisha yake yote yalikuwa ya kutoa siyo ya kupokea,"alisema Rais Mkapa kabla ya kumaliza hotuba yake, ambayo iliwafanya baadhi ya wananchi kutoa machozi.

No comments:

Post a Comment