Friday 14 October 2016

WAPINZANI WASIZUNGUMZE MABAYA TU KUHUSU SERIKALI, ASEMA MAMA MARIA NYERERE

LEO imetimia miaka 17, tangu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipofariki dunia nchini Uingereza. Ni siku ambayo Watanzania huiadhimisha kwa kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere. Katika makala hii ya ana kwa ana, iliyoandikwa na kutoka kwenye gazeti la Uhuru, Oktoba 14, mwaka 2013, Mwandishi Wetu, alizungumza na mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere (86), kuhusu umuhimu wa siku hii, mwelekeo wa kisiasa na mustakabali wa taifa la Tanzania.

SWALI: Oktoba 14, mwaka huu, Tanzania itaadhimisha miaka 17, tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Unapenda kuwaeleza nini Watanzania kuhusu siku hii?

JIBU: Ninachoweza kusema ni kuishukuru serikali kwa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa kila mwaka. Pia ninaishukuru serikali kwa kuendelea kudumisha amani. Ni nchi chache ambazo zimeweza kudumisha uhuru na amani kwa muda mrefu kama Tanzania. Nchi zingine zinagombana zenyewe kwa zenyewe kwa kipindi kirefu. Kwa maoni yangu hili jambo ni la kutilia mkazo.

SWALI: Unayaonaje maisha bila ya kuwa na Mwalimu Nyerere?

JIBU: Kwa maisha ya kawaida, nashukuru kwamba taifa linatuhudumia vizuri. Ninachokikosa ni kutokuwa karibu na mtu niliyemzoea na ambaye kila wakati anawaletea jambo jipya. Si kwamba tangu ameondoka hatujafanya mambo mapya, hapana. Kiubinadamu tunasema, mwalimu angekuwepo, tungefikia ngazi hii, labda hilo ndilo la maana sana.

SWALI: Ni changamoto zipi ulizowahi kukumbana nazo ukiwa mke wa rais?

JIBU: Kwa bahati nzuri nimekuwa mke wa kwanza wa rais na katika nchi masikini, halafu yenye mapungufu ya elimu na kila hali. Ingawa utajiri wa nchi ulikuwa mkubwa, lakini tulikuwa tunaona hakuna kitu kutokana na elimu tuliyokuwa nayo. Hatukuwa na uwezo mkubwa wa kuwaendeleza ndugu  zetu kama walivyofanya kina mama hawa wa viongozi wetu hawa wawili, Mama Anna Mkapa na Mama Salma Kikwete.

SWALI: Kwa nini wewe binafsi katika kipindi chote cha uongozi wa Mwalimu Nyerere, hukutaka kuanzisha taasisi ya mke wa rais kama ilivyo kwa wake wengine wa marais duniani?

JIBU: Wakati ule na sasa ni tofauti. Nilifanyakazi nyingi za kijamii, lakini hazikuweza kuonekana. Kwa mfano, nilishiriki kuanzisha vijiji vya mfano, lakini kazi hizo kwa wakati ule zilikuwa hazitangazwi. Hatukuona kama kulikuwa na faida kuzitangaza. Zilikuwa hazionekani kama nguo dukani. 

Tulipopata uhuru, shabaha yetu ya kwanza ilikuwa tujitambue. Na mtu hawezi kujitambua bila kujitegemea. Hilo lilikuwa jukumu letu la kwanza. Ilikuwa ni mazoea wakati ule kumuona mwanamke hawezi kufanyakazi ya aina fulani ama kitu fulani, labda mpaka awe waziri. Labda angekwenda vitani akashika bunduki, angeweza kuonekana.

Lakini sasa ni tofauti. Mama Anna Mkapa alikuwa na taasisi yake, amefanyakazi nyingi za kuwainua kina mama na kuwapatia ajira. Mama Salma Kikwete naye anayo taasisi yake, anatoa misaada kwa wanawake na watoto ili waweze kujitegemea.

Wanasema ukimwelimisha mwanamke, umeelimisha taifa zima na wote wawili wanapata misaada mingi kutoka nje. Wamejenge shule na kazi zao zinaonekana kwa sababu zinatangazwa kwenye vyombo vya habari tofauti na wakati ule.

SWALI: Wakati wa uhai wake, Baba wa Taifa alichukia sana rushwa. Lakini katika kipindi hiki, kumekuwepo na malalamiko mengi kuhusu tuhuma za rushwa. Baadhi ya wagombea wananunua ama kupata uongozi kwa kutoa rushwa. Nini mtazamo wako kuhusu jambo hili?

JIBU: Wakati wa uongozi wa Chama kimoja, viongozi walikuwa wakijileta wenyewe. Walikuwa wanavutwa na kitu fulani. Lakini tukumbuke kwamba, kiongozi analetwa na Mungu. Na wakati huo kampeni zilikuwa zinafanywa na Chama, rushwa haikuwa na nafasi na pesa hazikuwepo.

Sasa hii ya mgombea kufanya kampeni mwenyewe, atalazimika kuwanunulia chakula wapiga kura, kuwapa nauli ya kusafiri ya kwenda na kurudi na watadai zaidi. Bado mtu atasema kule nyumbani nina matatizo.

Sasa akisaidiwa na mgombea kwa kutimiziwa haja zake zote na kwa kuwa ameomba katika kipindi cha kampeni, tayari itaonekana kuwa hiyo ni rushwa, hata kama atakuwa amesaidiwa kwa nia njema.

Nakubali kwamba rushwa ipo, lakini sio kwamba imeanza katika awamu hizi za sasa. Ilikuwepo tangu awali, hata wakati wetu. Lakini masharti yalikuwa yanawabana wale waliokuwa wakiomba uongozi.
Walikuwa hawaoneani haya na muhusika alikuwa anaambiwa kistaarabu, kama unataka kufanya biashara, nenda kafanye biashara.

Lakini hivi sasa sasa rushwa imewatala. Wanaotoa na kupokea rushwa wanajulikana, lakini wanalindana. Na rushwa sote tunaichukia, sio Mwalimu peke yake, ni adui mkubwa wa maendeleo. Na sababu kubwa ya ongezeko la rushwa ni kulindana. Tunapolindana ndipo inazidi kuongezeka na taifa linakosa mwelekeo.

SWALI: Unadhani uwepo wa vyama vingi vya siasa unaisaidia serikali kuzinduka katika uendeshaji wa mambo yake?

JIBU: Bahati nzuri huwa nafuatilia sana vyama vya siasa. Nionavyo mimi, viongozi wa vyama vya upinzani wanasaidia kujenga nchi. Mkiwa chama kimoja, kikitokea kitu fulani mnaweza kuambiana, hiki hakifai.
Lakini mkiwa na vyama vingi, atajitokeza mtu na kusema mambo mengine ya ajabu. Kuhitilafiana ni jambo muhimu katika kujenga nchi. Mimi naona uwepo wao unasaidia na wanarekebisha mambo mengi. Wote ni viongozi walioletwa na Mwenyezi Mungu, uwepo wao ni sawa tu.

Lakini viongozi wa upinzani hawapaswi kuzungumza mambo mabaya tu kuhusu serikali. Yanapofanyika mambo mazuri, wanapaswa pia kuyasema, wasiishie tu kulaumu. Kama kuna kitu kinaonekana wazi kimefanyika, wanapaswa kusema ukweli.

SWALI: Ni jambo lipi lililowahi kumchukiza sana Mwalimu Nyerere katika maisha yake?

JIBU: Swali hilo labda angekuwepo mwenyewe ungemuuliza. Lakini unafikiri ile vita ya Kagera haikumchukiza? Nadhani ilimchukiza sana. Hata matamshi yake kuhusu vita ile yanadhihirisha hilo. Alisema uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo.

SWALI: Na ni tukio lipi, ambalo liliwahi kumfurahisha Mwalimu Nyerere akiwa madarakani au hata baada ya kustaafu?

JIBI: Nadhani ni lile la kumshinda Iddi Amini katika vita vya Kagera.

SWALI: Wewe binafsi ni tukio lipi, ambalo lilikufurahisha sana katika maisha yako?

JIBU: Ni ile siku niliposhuhudia bendera ya Uingereza ikiteremshwa na kupandishwa bendera ya Tanganyika. Japokuwa hatukuwa na uelewa wa kutosha, lakini kitendo hicho kilinifurahisha mno.

SWALI: Na ni tukio lipi, ambalo lilikuhuzunisha sana katika maisha yako?

JIBU: Ni ule ujinga wangu kwamba, Mungu hakustahili kumchukua Mwalimu Nyerere mapema. Hili lilinisikitisha sana kwa sababu ni ujinga kutokubali kwamba Mwenyezi Mungu ana mipango yake.

SWALI: Unatoa mwito gani kwa wanawake wa Tanzania, hasa wale waliojitosa katika masuala ya siasa ama kupewa nafasi za juu za uongozi?

JIBU: Kwa kweli tunapaswa kuwapongeza. Bahati nzuri nimekuwa nikifuatilia sana habari zao na wengine huwa wakija Butiama kunitembelea. Baadhi yao wamepata nafasi hizo kwa shida. Mawazo yao ni mazuri. Nawaomba waongeze bidii kwa sababu wanafanyakazi kubwa.

SWALI: Unatoa ushauri gani kuhusu mwelekeo wa Taifa kwa sasa?

JIBU: Tunapaswa kuendeleza yote mazuri yaliyofanywa na waasisi wetu. Hawa watu walifanya mambo mazuri na makubwa sana. Tunapaswa kudumisha muungano wetu.

Kama kuna mtu aliyejenga nyumba na kuna watu wanaendelea kuishi, wale waliopo wanapaswa kuiboresha kwa kuipaka rangi na vitu vinginevyo. Hii nchi ni yetu sote, siyo ya mtu mmoja.

No comments:

Post a Comment