Friday, 14 October 2016

MAMA KARUME ASIMULIA MWALIMU NYERERE ALIVYOKUTANA NA ABEID KARUME





NA MOHAMMED ISSA
MJANE wa muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, Mama Fatuma Karume, ameeleza siri ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kukutana na Mzee Karume kwamba, hawakukutana katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, bali chanzo cha kukutana kwao kilikuwa klabu ya African Sports.
Amesema kuwa chimbuko la waasisi hao kukutana lilikuwa kabla ya Uhuru wa Tanganyika.
Mama Karume, alieleza hayo hivi karibuni, wakati akihojiwa na kituo cha redio cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC-Taifa), mjini Unguja.
Amesema Mzee Karume na Mwalimu Nyerere hawakujuana wakati wa Muungano, bali walifahamiana kabla ya Uhuru wa Tanganyika.
“Ulipopatikana Uhuru wa Tanganyika, tukasema hee. Lakini chanzo chake kilikuwa African Sports. Kila mwezi wa Aprili, wakati wa Pasaka, watu wa kule walikuwa wanakuja hapa,” alisema na kuongeza: “Ndio sababu mpaka leo hii utaratibu huu unaendelea na hilo ndilo chimbuko la kukutana kwao.”
Katika simulizi yake hiyo, Mama Karume anasema kulikuwa na klabu ya African Sports ya Zanzibar na ile ya Tanganyika, ambazo zilikuwa na ushirikiano wa kimichezo na utaratibu wa kutembeleana kila mwaka.
“Baada ya hapo ndipo ikaanza kuingia siasa, lakini vyama vya mpira na hasa Yanga. ilikuwa mstari wa mbele kufanya mashindano na kuwafahamisha watu walipo na wao ndio mpaka leo wana kijani na majano,” anasimulia Mama Karume.
Anaongeza: “Hata bendera walitengeneza wao kwa utaratibu mwingine, lakini Yanga bado mpaka leo wanaitumia upande mmoja manjano na mmoja kijani.”
Mama Karume anasema Mzee Karume alikutana na Mwalimu Nyerere wakati anadai Uhuru wa Tanganyika na wakakubaliana kila upande ufanye hivyo.
Anasema Zanzibar kulikuwa na vyama vingi vya michezo na shughuli mbalimbali kama vile Shiraz Assosiation, African Assosiation, Comorian Assosiation, Hindu Assosiation na Arabu Assosiation.
“Hizo Assosiations havikuwa vyama vya siasa. Baada ya Mwalimu Nyerere kuzungumza na Mzee Karume, wakakubaliana kuviunganisha kwa kuwa Washirazi na Waafrika ni hao hao tu,” anasimulia.
Ameongeza kuwa katika kuongeza chachu ya kupigania uhuru wa pande hizo mbili, Mwalimu Nyerere aliwaeleza viongozi wa Zanzibar nini wanapaswa kufanya.
Mama Karume anasema awali, Mzee Karume alionyesha wasiwasi kuhusu jambo hilo na kuamua kumueleza ukweli Mwalimu Nyerere.
“Kuna sharti moja akalitoa Mzee Karume, ndipo Mwalimu Nyerere akamwambia kubali, kwani unakataa nini.  Mzee Karume akamwambia mimi nina mke wangu mdogo (kijana) na nina watoto wawili, hivyo nikitumbukia katika siasa na kugombana na hawa waarabu nahisi watanitoa roho hawa,” amesema Mama Karume.
Alimkariri Mzee Karume akimweleza Mwalimu Nyerere: “Watoto wangu wadogo, ndio hofu yangu iko hapo. Mzee Karume alizungumza hayo kwenye mkutano. Niliyajua hayo kwani aliporudi kwenye mkutano, alikuja kunieleza.”
Anasema baada ya kueleza hayo, Mwalimu Nyerere alimwambia Mzee Karume kwamba, yeye ndiye Rais wa Tanganyika, hivyo wakipata Uhuru hataweza kuwasahau.
Mama Karume anasema baada ya ubishani wa hapa na pale, hatimaye Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walifikia makubaliano.
“Baada ya kukubali, Mzee Karume akawa ndiye mwenyekiti wa Chama cha Afro Shiraz. Kwa sababu kulikuwa na waafrika yaani Shiraz Assosiation na African Assosiation, ndipo ikazaliwa Afro Shiraz,” amesimulia na kuongeza kuwa, huo ulikuwa mwaka 1957.
Kuhusu Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar, Mama Karume amesema upo na kwamba, watu wa hali ya chini wanauimarisha na kuukubali.
Amesema wanaotaka kuuvunja Muungano, wana jambo lao ambalo wanataka kulifanya kwa sababu zao.
“Muungano uliopo sasa umewawezesha watu wengi wa Zanzibar kuishi Bara na wa Bara kuishi Zanzibar,” amesema.
Akizungumzia mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini, Mama Karume alivitaka kujikita katika maendeleo na kwamba, wabunge waingie bungeni na washirikiane na serikali.
“Sasa leo unamuona mtu anahutubia anasema sisi tunataka Uhuru wetu, tunataka nchi yetu, kwa nini?” Alihoji na kuongeza kuwa, binafsi anawashangaa na kushindwa kuwaelewa.
Amesema ni vyema viongozi wa kisiasa wakipanda kwenye majukwaa ya kisiasa, wahimize kujenga nchi badala ya kuzungumza mambo ambayo hayana maana.
Akizungumzia misingi imara ya uongozi iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mama Nyerere, anasema iliwekwa itumiwe kwa pamoja, vikiwemo vyama vya siasa.
Hata hivyo, anasema vyama vya siasa haviwezi kufuata misingi hiyo kwa sababu vinapinga misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere.
“Hawataweza kuendeleza misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa. Kazi yao ni kuivuruga kwa sababu hawaitaki. Sisi tuendelee hivyo hivyo, tumegemege kidogo kidogo, tuendelee na maisha,” anasema.
Mama Karume amesema kwa sasa, Watanzania hawana wanachokipigania kwa sababu kama uhuru, ulishaatikana tangu miaka ya 1960. Amesema kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni wananchi kuigania maendeleo.
“Maendeleo yaliyoachwa tunayo, tuendeleze maendeleo hayo na kuongeza mengine. Wale wanaosema mambo yaliyoachwa na Mwalimu Nyerere yamepitwa na wakati, walete mapya wayafanye tuyaone,”amesema.
Mama Karume amesema hafurahishwi na mwenendo wa viongozi na wabunge wa upinzani, kufanya vitendo vya kuzomea na kutoka kwenye ukumbi wa bunge kwa sababu vinawavunjia heshima.
Amevitaka vyama vya upinzani kushirikiana na serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi, hata kama vyama hivyo havina wabunge. Amesema kwa vile vipo na vinafanya kazi, vinapaswa kushirikiana na dola.
“Kuna vijiji huko wanaweza kwenda kufanya shughuli za maendeleo ya wananchi, badala ya kuleta mapambano. Hata wanapoikosoa serikali, wanapaswa kuikosoa kwenye makosa na siyo kuitukana,”amesema.
Mama Karume anasema kumuenzi mtu, hasa kiongozi ambaye amefariki au aliyeuawa, ni kufuata mazuri aliyoyaacha, kauli zake na matendo yake.
“Binadamu ana mazuri yeye mwenyewe na kama ni kiongozi, ana mazuri aliyofanya kwa taifa, hivyo kila mmoja analo jukumu la kuwaenzi viongozi wetu,” amesema.
00000


No comments:

Post a Comment