Friday 14 October 2016

FAMILIA YA BABA WA TAIFA YASEMA, RAIS DK. MAGUFULI ANAFUATA NYAYO ZA MWALIMU NYERERE

FAMILIA ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere imeipongeza serikali ya awamo ya tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, kwa kuchukua hatua mbalimbali katika kuinua uchumi na maisha ya wananchi wa kipato cha chini.

Imesema hatua zilizochukuliwa na serikali hadi sasa chini ya Rais Magufuli, zimeonyesha kila dalili kwamba, anatembea katika barabara ile ile aliyokuwa akipita Mwalimu Nyerere.

"Hadi sasa serikali inakwenda vizuri sana. Uongozi wa Rais Magufuli ni wa kupigiwa mfano. Amejitahidi kwa kiasi chake kutembea katika barabara ile ile aliyokuwa akitembea Baba wa Taifa," imesema familia hiyo.

Hayo yamesemwa na Msemaji mkuu wa familia ya Mwalimu Nyerere, Japhet Wanzagi, wakati alipokuwa akizungumza na Uhuru, kuhusu maadhimisho ya miaka 17, tangu Baba wa Taifa alipofariki dunia Oktoba 14, 1999.

"Rais Magufuli amejitahidi kufanya mambo mbalimbali mazuri, tangu alipoingia madarakani Novemba, mwaka jana. Watanzania sote tunapaswa kumuunga mkono na kuiheshimu serikali yake," alisema Chifu Wanzagi, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa kabila la Wazanaki, ambalo makao makuu yake yapo katika kijiji cha Butiama, kilichoko wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara.

Chifu Wanzagi alirithi cheo cha uchifu wa kabila hilo Machi, 1997, baada ya kufariki kwa baba yake, Chifu Edward Wanzagi Nyerere, ambaye alikuwa kaka mkubwa wa Mwalimu Nyerere.

"Serikali kwa sasa imerejesha nidhamu ya utendaji wa kazi serikalini. Imekuwa ikipambana kikamilifu na wezi wa mali ya umma, wala rushwa, mafisadi na kukusanya kodi kwa kiwango cha juu kwa manufaa ya nchi huku ikiziba mianya ya kupotea kwa fedha za umma,"alisema msemaji huyo wa familia ya Mwalimu Nyerere.

Aidha, Chifu Wanzagi ameipongeza serikali kwa kuendelea kuandaa maadhimisho ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kila mwaka, wakati ambapo jambo hilo halipo kwenye utaratibu wa nchi.

Alisema kwao wanaliona jambo hilo kuwa ni la heshima na kumshukuru Mungu na kwamba, familia inafarijika na kuamini kuwa Watanzania wamedhamiria kwa dhati kumuenzi Baba wa Taifa.

"Hata biblia inasema 'kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka, bali jina la mtu muovu litaoza,'" alisema Chifu Wanzagi,  ambaye ni mtoto wa 37 kati ya watoto 57 wa Chifu Edward Wanzagi, ambaye naye alirithi cheo hicho kutoka kwa baba yake Mwalimu Nyerere, Chifu Burito Nyerere.

Aliongeza kuwa mwanadamu mwenye viwango, aliyeishi kwa hofu ya Mungu, kumkumbuka kuna baraka zake.

Chifu Wanzagi alikiri kuwa pengo aliloliacha Baba wa Taifa bado lipo na kwamba iwapo angekuwepo, kungekuwa na vitu vingi vya ziada, ambavyo angeelekeza vifanywe kwa niaba ya wananchi.

Ili kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo, kiongozi huyo wa Wazanaki amewataka Watanzania kusimama katika misingi ya haki na kudumisha amani, mambo ambayo alikuwa akiyapigania kwa nguvu zote.

"Kama ni kutofautiana, basi tutofautiane kimtazamo, lakini tusigombane wala kupigana. Kila mmoja ailinde amani tuliyonayo kwa nguvu zote,"alisisitiza.

Alisema nchi zote zilizo jirani na Tanzania zinavutiwa na amani iliyopo nchini na kila zinapopatwa na shida, kimbilio lao kubwa ni Tanzania na siku zote zinaomba amani iliyopo isitoweke.

Aidha, Chifu Wanzagi amewataka Watanzania kudumisha umoja, ambao Mwalimu Nyerere aliujenga kwa kuwaunganisha pamoja wananchi, licha ya kuwepo kwa makabila zaidi ya 120.

Alisema Tanzania ndio nchi pekee inayoongoza kwa umoja barani Afrika, kutokana na wananchi wake kuishi kwa upendo na ushirikiano bila kujadili tofauti za makabila, dini, rangi na jinsia.

"Hapa Tanzania wapo waarabu, wazungu na waafrika, lakini wote Mwalimu aliwaona ni Watanzania. Hivyo tusikubali kutenganishwa kwa misingi hiyo," alisema.

Chifu Wanzania pia amewataka Watanzania kuwa na upendo na kuachana na makundi yanayosigana kwa misingi yoyote. Alisema makundi yanayopaswa kuwepo katika jamii ni yale tu yenye mahitaji maalumu.

Amesisitiza umuhimu wa kuwalinda na kuwatunza wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi, ambao alisema enzi za uhai wake, Mwalimu Nyerere aliwatunza na kuwapatia mahitaji yote muhimu.

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, kiongozi huyo wa Wazanaki alisema ni nzuri na kumtetea Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa yenye viashiria vya uvunjifu wa amani.

Alisema siyo kweli kwamba Rais Magufuli ni dikteta kama alivyoitwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, bali alifanya hivyo kutokana na dhamana aliyonayo ya kulinda amani ya nchi.

"Kunapokuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani, rais anao wajibu wa kuchukua hatua kwa lengo la kulinda usalama wa nchi na wananchi. Na kufanya hivyo hakuna maana kwamba yeye ni dikteta. Yuko sahihi kabisa,"alisema.

Amewataka viongozi wa vyama vya siasa, wanapoamua kuitisha mikutano au maandamano, wafuate taratibu na isiwe na lengo la kuvuruga amani ya nchi.

Chifu Wanzagi alisema ni vyema mikutano ya vyama vya kisiasa itumike kutangaza sera za vyama, badala ya kutambiana na kuhubiri machafuko. Alisema mikutano hiyo ni sawa na ya kidini, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kukubaliana na sera anazohubiriwa ama kuzikataa bila ya kushinikizwa kufanya hivyo.

"Siasa za vyama vyote ni sawa tu, kusiwepo na kulazimishana kufanya hivyo. Viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kushindana kwa nguvu za hoja katika kunadi sera zao na sio hoja za nguvu,"alisema.

Aidha, amewataka viongozi wa serikali kufanyakazi zao kwa kuwatumikia wananchi kwa kuwa cheo ni dhamana na kwamba, wakati wowote wanaweza kuvuliwa nyadhifa zao na kukabidhiwa wengine.

Ameiomba serikali kuongeza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa kwa vile vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kuwakosesha haki wananchi wasio na uwezo kifedha.

Amesema iwapo rushwa itapungua ama kumalizika katika taasisi nyeti kama vile mahakama, polisi na hospitali, nchi itatulia na maisha ya Watanzania yataboreka.

Amewaponda viongozi wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitoa katika Chama na kuhamia upinzani baada ya kuenguliwa kugombea nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Alisema kitendo chao hicho kimedhihirisha wazi kuwa, walichokuwa wakikitaka ni tamaa ya madaraka na sio kuwaongoza wananchi na kuwaletea maendeleo.

"Kwanza wana bahati kwa sababu waliwahi kupata nafasi za uongozi kwenye Chama na serikali, wengine hawakupata kabisa. Hivyo walipaswa kutosheka na walichokipata kwa sababu kila kukicha kuna vijana wanaomaliza masomo na wanahitaji nafasi hizo na wengine wanazaliwa,"alisema.

No comments:

Post a Comment