NA MOHAMMED ISSA
OKTOBA 14, mwaka 1999, Tanzania ilipata pigo baada
ya kutokea kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kilichotokea Jijini
London, Uingereza.
Msiba wa Mwalimu Nyerere licha ya kuacha simanzi
na majonzi kwa familia yake, pia ulitikisa Tanzania na dunia kwa ujumla
kutokana na mambo aliyoyafanya katika kipindi cha utawala wake.
Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake, alitoa mchango
mkubwa katika ukombozi wa baadhi ya nchi za bara la Afrika, hivyo alijipatia
jina kutokana na mchango wake huo.
Akizungumzia msiba wa Mwalimu Nyerere, mwanasiasa
mkongwe hapa nchini, Paulo Kimiti anasema mwaka 1999, baada ya Baba wa Taifa
kufariki dunia, ilibidi yafanyike maandalizi ya aina mbili.
Kimiti, ambaye aliwahi kufanya kazi na Mwalimu
Nyerere, akishika nafasi mbalimbali, ikiwemo uwaziri na ukuu wa mkoa kwenye mikoa
mbalimbali nchini, anasema maandalizi ya kwanza yalikuwa ni ya kuupokea mwili wake
kwa wakazi wa Dar es Salaam.
“Mipango hiyo ilikuwa inasimamiwa na Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye, lakini utaratibu mwingine yalikuwa ni maandalizi ya
mahali pa kumuhifadhi Baba wa Taifa na hapo ilikuwa lazima yafanyike nyumbani
kwake alikozaliwa, Butiama,” anasimulia.
Anasema haikuwa rahisi kwa sababu mwanzoni watu
wengi walikuwa wanapendekeza kuwepo utaratibu wa kuwa na mahali pamoja pa
kuzikia viongozi wa taifa.
Anasema katika kutekeleza hilo, ikaamuliwa achaguliwe
kiongozi mmoja na waziri mmoja, waende kwa Musoma na maandalizi yote yafanyike
Butiama.
“Rais Benjamini Mkapa kipindi hicho aliniteua mimi
kama Waziri wa Kazi na Vijana. Labda aliniteua kutokana na kazi yenyewe kwamba
iwe wizara inayohusika na maandalizi, kwamba vijana watasaidia kuweka mambo
yakawa mazuri kule,” anasema.
Anaongeza: “Mimi niliondoka mara tu baada ya mwili
kuwasili Tanzania na nikaenda Butiama kushirikiana na viongozi wa kule.”
Anasema miongoni mwa viongozi alioshirikiana nao
ni Chifu Japheti Wanzagi, ambaye ni mkuu wa familia ya Mwalimu Nyerere na pia
kiongozi wa kabila la Wazanaki.
“Yeye ndiye aliyenisaidia sana kusimamia utaratibu
mzima wa maandalizi ya mazishi. Wapo kina Jenerali Musuguri (David), anafahamika
ni wazee wamekaa sana pale. Jenerali Musuguri ni kati ya majenerali wa mwanzo
nchini, lakini anaishi Butiama akishirikiana na wazee wengine wa pale,”
anasimulia.
Kimiti anasema kwa mkoa wa Dar es Salaam, walikuwa
wakiwasiliana na Mzee Joseph Butiku, Mama Maria Nyerere na Jaji mstaafu Joseph
Warioba ili wawe na uhakika wa mipango yote inayofanyika ili iwe inayokubalika
na pande zote mbili.
Hata hivyo, anasema Butiama kulikuwa na matatizo
ya aina tatu, kwanza ni eneo lipi azikwe Mwalimu na kwa sababu zipi tuchague
eneo hilo.
“Sasa katika kuchagua sehemu yenyewe, kwanza watu
walipendekeza pale ambapo wazazi wa Baba wa Taifa, yaani baba yake na mama yake
Mwalimu Nyerere walipozikwa, ambako ni mbele ya nyumba yao,” anasema
Anaongeza: “Hiyo ikawa ngumu kuikubali kwa sababu
huyo ni kiongozi wa taifa, lazima apate nafasi azikwe pekee yake. Huwezi
kumchanganya na familia nyingine, ingawa ukweli ni baba na mama, lakini katika
taratibu, lazima kiongozi huyu awe na eneo la pekee yake katika mazishi.”
Kimiti anasema eneo jingine, ambalo lilipendekezwa
ni mahali ambapo yeye mwenyewe alishaweka picha yake ya kuchonga na alitaka
azikwe sehemu hiyo.
“Ni kweli tulitaka tupatumie mahali hapo, lakini
tukaja kugundua kwamba, sehemu hiyo makosa yalifanyika wakati wanamjengea nyumba
yake. Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), walipitisha mfereji wa maji
machafu sehemu hiyo, ingawaje huwezi kuuona kwa sababu uko kwa chini. Sasa
tukasema hatuwezi kufanya makosa, ingawaje mzee mwenyewe alitaka sehemu kama
hiyo, lakini isingewezekana kwa sababu ya hila ya mfereji huo,” amesema.
Anasema wazo la tatu, ambalo waliona ni vizuri
walitumie baada ya kushindikana sehemu
mbili, wawasiliane na viongozi walioko Dar es Salaam kwa lengo la kufikia
mwafaka.
Kimiti anasema walimshirikisha Mama Maria, Mzee
Butiku na Jaji Warioba ili wakubaliane kuhusu jambo hilo.
“Tulichofanya
kwa kushirikiana na viongozi wa pale, tuliona Mwalimu Nyerere alikuwa na
bustani yake pale pale karibu na nyumba yake, ilikuwa bustani mzuri tu. Tukaomba
kibali, ikiwezekana tumzike katika eneo hilo,” anasema.
Anaongeza: “Kulikuwa na utata mkubwa, baadhi ya
viongozi walisema hapana, tutakuwa tumemtupa, yuko nje ya himaya yake, lakini
tukasema huwezi kusema nje ya himaya maana eneo lake limezungukwa na fensi,
hivyo eneo lote lile ni lake.”
Kimiti anasema uamuzi waliofikia ni kutengeneza
kaburi lake sawa kabisa na mlango wa
kuingilia, baada ya kukubaliana na wazee
wote.
“Na mimi kama kiongozi wa serikali, nikamuomba
Chifu Wanzagi atusaidie kusimika fimbo mahali pale, ambalo anataka Baba wa Taifa azikwe, ili iwe ushahidi, isionekane
ni mtu mmoja ameamua azikwe wapi. Alichomeka mkuki na papo hapo tukaanza
kuchimba kaburi bila kuchelewa,” anasimulia.
Anasema kuwa kaburi hilo lilianza kuchimbwa na vijana
wa JKT na kwamba ndio walioshiriki kuanzia mwanzo, ikiwa ni pamoja na
kulijengea.
Kimiti anasema wakati akiwa Butiama, alipewa
majukumu ya kukaimu nafasi ya mkuu wa mkoa wa Mara kwa muda ili awe Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo.
Anasema huwezi kufanya kazi hiyo bila ya kuwa na
kibali maalumu na ndipo alipopewa barua hiyo ikieleza kuwa, pamoja kwamba
alikuwa waziri, pia awe mkuu wa mkoa wa Mara kwa kipindi hicho.
Kimiti amemtaja Mkuu wa Mkoa wa Mara, aliyekuwepo wakati
huo kuwa ni Lugoye, ambaye hali yake ya afya haikuwa nzuri na kwamba,
asingeweza kusimamia majukumu hayo ipasavyo.
Anasema aliendelea kuchukua madaraka ya ukuu wa
mkoa kwa kipindi chote hicho na kwamba, alifanya mikutano ya hadhara wilayani Musoma
ili kuwaeleza wananchi ratiba mzima itakayotumika katika kumuhifadhi Baba wa
Taifa.
“Tulifanya mikutano, wazee waliuliza maswali na
baadhi ya wazee walitaka mwili wa Baba wa Taifa ukifika Musoma Mjini, wapewe
heshima ya kumuona pale pale uwanjani. Lakini niliwakatalia, nikasema huwezi
kuufanya mwili wa Baba wa Taifa kama Mwenge wa Uhuru, kuzunguka huku na huko,”
anasema.
Anaongeza: “Watu wengi walikuwa wameomba mwili wa
Baba wa Taifa uende katika mikoa mingine. Dodoma waliomba, Tabora waliomba, Mwanza waliomba mwili upelekwe wakamuone, lakini
nikasema hapana, mwenye shida atakwenda Butiama.”
Kimiti anasema baada ya kuelewana na wazee wa
Musoma na kukamilika kwa maandalizi yote muhimu, walikuwa wanajiandaa kwa ajili
ya kuupokea mwili wake.
Anasema mambo ya usafiri yalikuwa tayari na hapo
aliwaeleza wananchi kwamba, watatoa nafasi ya kuuaga mwili nyumbani kwa Baba wa
Taifa.
“Mwili wake uliletwa jioni kwa ndege, ukiwa na
viongozi wengi sana, lakini tulikuwa tumejiandaa vizuri, tulikuwa na usafiri wa
kutosha, hivyo tukauchukua mwili mpaka nyumbani kwake,” anasema.
Anaongeza: “Siku hiyo ilikuwa ngumu, kulikuwa na
manyunyu, mtikisiko ambapo watu wengi walishangaa, kwani kipindi chote walichokuwa
wamekaa Butiama, mambo hayo hayakutokea, lakini walimuachia Mwenyezi Mungu
kwani yeye ndiye anayejua kila kitu.”
Anasema mipango iliendelea na kwamba waliamua kwa
kipindi chote watoe nafasi ya siku mbili ili wananchi wapate fursa ya kutoa
heshima za mwisho.
Kimiti anasema wananchi wa mikoa ya karibu
walifika wilayani Butiama kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho.
Akizungumzia siku ya mazishi, Kimiti anasema maandalizi
yalianza asubuhi na waliohusika na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) na kwamba, upande wa ibada ulisimamiwa na Kanisa Katoliki, ambapo
Muadhama Policapy Kardinali Pengo, alisimamia shughuli zote za misa, kuanzia
kanisani Butiama hadi kaburini.
Kimiti anasema siku hiyo yeye alikuwa
mshereheshaji, kuanzia kanisani mpaka kaburini na kwamba, aliwaanda viongozi wakuu
na familia kuweka mashada ya maua.
“Suala hilo lilichukua muda wa kutosha kuanzia
asubuhi mpaka mchana, karibuni saa nane na ilipofika saa tisa au kumi hivi, tulikuwa
tumemaliza kwani viongozi wengi walirudi siku hiyo hiyo na tukabaki kama
familia tu,” anasema.
Anasema baada ya siku mbili, nao walirudi na
kuwaacha wanajeshi kulinda kaburi hilo mpaka wakati walipolijengea upya kwani
lilikuwa la muda.
Kimiti anasema baada ya miezi miwili, ilipofika Desemba,
1999, Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alitembelea Tanzania na kwamba
Rais Mkapa alimteua kusafiri naye hadi Butiama.
Anasema Baba wa Taifa alikuwa na mvuto kwa
wananchi wengi kwa sababu alikuwa na haiba mbele ya jamii na alikuwa akipenda
watu.
“Baba wa Taifa alikuwa mtu wa watu, alikuwa
anapenda watu na siku zote ukipenda watu nao watakupenda. Hakutaka mtu mwingine
aonewe ama aonekane anadharauliwa mbele ya wengine bila sababu ya msingi,”
anasema.
Anaongeza: “Mwalimu alikuwa mcha Mungu kila wakati,
sasa tabia hiyo iliwafanya watoto kwa wakubwa, kila mmoja kumpenda.”
Kimiti anasema atamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa
sababu ya mapenzi yake kwa taifa, ambapo hakutaka kuliona taifa linakuwa
masikini, kwani alitaka watu wote wawe na hali mzuri ya maisha.
Anataja sababu ya pili kwamba, Mwalimu Nyerere hakupenda
kusikia maneno bila ya kufuatilia yeye mwenyewe.
“Mwalimu Nyerere hakupenda umbea. Alipokuwa
anasikia kitu, alikuwa anakuita na kukuliza ili umpe uthibitisho. Mimi yaliwahi
kunitokea. Aliposikia ninajenga nyumba Dodoma, nikaitwa na kuulizwa unajenga
nyumba, umepata wapi hela. Wewe ni waziri wangu, najua mshahara wako, hizi hela
umepata wapi, hebu niambie,” anasimulia.
Anaongeza: “Kwa bahati nzuri nilikuwa nimepata
mkopo kutoka Benki ya Nyumba wakati huo, ikawa ndio ponyaponya yangu.”
“Usipokuwa na kiongozi, ambaye anafuatilia mambo, majungu
yanaweza kuharibu na watu wakashindwa kufanya kazi kwa sababu ya majungu. Ndio
maana watu wengi walikuwa wanaogopa kumpelekea uongo Mwalimu kwani ukimpelekea
uongo atajua tu na atamwita muhusika ili amueleze ukweli,” anasema Kimiti.
Anasema pia kuwa alikuwa anampenda Mwalimu kwa
sababu mara nyingi alikuwa anawaonya kwamba, wachezee mshahara wao, kamwe
wasichezee kazi.
“Watu wanaweza kuchukulia jambo rahisi, lakini
maneno hayo yalikuwa na maana, kwani ukichezea mshahara, unaweza ukaupata siku
nyingine, lakini kazi ukiichezea, hata huo mshahara huutaupata,” anasema.
Kimiti anasema ilikuwa vigumu kumfananisha Mwalimu
Nyerere na kiongozi mwingine yeyote kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya
kazi.
Mwanasiasa huyo mkongwe amewataka viongozi
mbalimbali nchini, kuwa watumishi wa watu kwani wakitekeleza hilo, watafanikiwa
zaidi.
Akizungumzia utendaji wa mawaziri wa serikali ya
awamu ya tano, amewataka wafanye kazi kwa bidii kubwa bila ya kuwa na wasiwasi
wa kuogopa kufukuzwa.
“Mawaziri lazima watambue kwamba, Rais Dk. John
Magufuli amewaamini, hivyo jukumu lao ni kufanya kazi bila ya wasiwasi wa
kuogopa kufukuzwa, badala yake wazingatie kiapo walichoapa,” anasema.
Anasema mawaziri hao kupewa dhamana na Rais
Magufuli siyo kwamba amewajaribu, bali amewaamini, hivyo wajibu wao ni
kutekeleza na kufanya kazi kwa misingi na falsafa ya serikali ya awamu ya tano
ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Kuhusu utendaji wa Rais Magufuli, Kimiti amesema
anafanya kazi kubwa na nzuri na kwamba, anatanguliza upendo katika kutekeleza
majukumu yake.
Anasema Rais Magufuli anafanya kazi bila ya kujali
kabila, dini, rangi, chama na muda wote anataka watu waishi kama familia moja.
AMETOKEA
WAPI?
Akizungumzia historia yake kwa ufupi, Kimiti anasema
alizaliwa mjini Sumbawanga, mwaka 1940 na alipata elimu yake ya msingi wilayani
humo mkoani Rukwa.
Kimiti anasema elimu ya sekondari aliipata Mzumbe
na kwamba, shahada ya kwanza alichukua nchini Uholanzi, ambapo shahada ya pili
aliipata nchini Marekani.
Anasema kitaaluma ni mtaalamu wa kilimo, ambapo
mwaka 1980, alichaguliwa kuwa mbunge wa taifa na miaka miwili badaye,
alichaguliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kimiti anasema mwaka 1984, aliteuliwa kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro na mwaka 1989 hadi 1991, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Mwaka 1991 hadi 1995, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya na mwaka 1995 hadi 1998, alikuwa
Waziri wa Kilimo na Ushirika.
Kuanzia mwaka 1998 hadi 2000, alikuwa Waziri wa
Kazi na Vijana na kuanzia mwaka 2000 hadi 2004, alikuwa Mwenyekiti wa Kamisheni
ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Afrika (AU), ambapo alistaafu rasmi kwa hiari yake
mwaka 2010.
0000000
No comments:
Post a Comment