Monday 21 November 2016

JPM AVUNJA BODI TRA


SAFISHA SAFISHA ya Rais Dk. John Mgufuli kwenye idara na taasisi za serikali, imeendelea kutawala kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bernard Mchomvu.

Uamuzi huo wa rais umekwenda pamoja na kuivunja bodi ya mamlaka hiyo.

Aidha, Rais Dk. Magufuli, amemteua Charles Kichere, kujaza nafasi ya Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, iliyokuwa wazi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu, Dar es Salaam, jana, uteuzi wa mwenyekiti mwingine pamoja na bodi nzima ya mamlaka hiyo utatangazwa baadaye.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kushusha rungu ndani ya mamlaka hiyo, ikiwa ni mkakati wa kuisuka ili kuiwezesha kupanua wigo wa ukusanyaji mapato.

Novemba 27, mwaka jana, Dk. Magufuli alimsimamisha kazi aliyekuwa Kamishina Mkuu wa TRA, Rishard Bade, kisha kumteua Dk. Phillip Mpango, kuchukua hiyo kabla hajateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwenye bandarini ya Dar es Salaam na ofisi za TRA, ambapo alibaini upotevu wa makontena 349, yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80, ambayo taarifa zake ndani ya Mamlaka ya Bandari zipo, lakini katika mtandao wa TRA hayaonekani.

Katika kashfa hiyo ya upotevu wa makontena, vigogo wengine wa TRA walisimamishwa kazi kisha kufikishwa mahakamani. Vigogo hao ni Kamishina wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Tiagi Masamaki, Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.

No comments:

Post a Comment