Monday 21 November 2016

MAKONDA AFICHUA UFISADI WA KUTISHA KIGAMBONI

ZIARA ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, imefichua kuwepo kwa harufu ya ufisadi katika ulipaji wa fidia  kwa wananchi katika miradi mbalimbali wilayani Kigamboni.

Kufuatia  hali hiyo, Makonda amesema kuwa tayari  amewasilisha nyaraka mbalimbali katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili iweze kuchunguzwa.

Mbunge wa wilaya hiyo, Dk. Faustine Ndungulile, aliulipua mradi mkubwa wa  nyumba za kisasa wa AVIC Town, kwamba ulijaa utapeli mkubwa kwa wananchi waliokuwa wanamiliki maeneo ulipojengwa mradi huo.

Alisema hadi sasa wananchi hao waliohamishwa kupisha mradi huo, yakiwemo maeneo yaliyokuwa yanamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawajalipwa.

Tuhuma hizo ziliibuka mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati wa ziara ya Makonda, yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi  mkoani Dar es Salaam, ambayo ameanzia wilayani humo.

Kufumuka kwa tuhuma hizo kulitokana na  malalamiko kutoka kwa wananchi waliokuwa wakiishi eneo la mradi wa AVIC Town,  kutolipwa fidia zao, hali iliyomfanya mama mmoja kuangua kilio   hadharani.

Mwanamke huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Pascalina Warioba, alijikuta akiangua kilio  wakati akitoa kero zake mbele ya mkuu huyo wa mkoa na kusababisha simanzi kubwa.

Pascalina alisema tangu mradi huo ulipotambulishwa na kuanza kujengwa, hawajalipwa stahiki zao.

“Mimi ni mwathirika wa mradi huu, tangu unaanzishwa na kuhamishwa,
nilipaswa kulipwa shilingi 700,000, lakini hadi leo sijalipwa na thamani ya fedha inaongezeka,”alisema mama huyo kisha kuangua kilio.

Kufuatia malalamiko ya mama huyo, Makonda alimtaka Dk. Ndungulile kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo, ambapo mbunge huyo alikiri kuwa mradi huo umejaa harufu ya utapeli mkubwa.

Mbunge huyo alisema wananchi waliokuwa wanamiliki eneo ulipojengwa mradi huo, hawajalipwa licha ya kuondolewa kimabavu huku jeshi la polisi likitumika.

Alisema sehemu ya ardhi hiyo yenye ukubwa wa ekari 18,  zilikuwa zikimilikiwa na CCM na zilichukuliwa kwa matumizi katika mradi huo.

“Huu mradi umejaa  utapeli mkubwa. Hakuna mwananchi aliyelipwa fidia mpaka sasa, licha  ya mradi huu kukamilika na hivi sasa unatumika,”alisema Dk. Ndungulile.

Alimuomba Makonda kuingilia kati sakata hilo  ili wananchi waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo waweze kutendewa haki.

Akizungumzia hatua hiyo, Makonda alisema leo watendaji wa serikali wanaohusika na taarifa za mradi huo, wanapaswa kumfikishia taarifa sahihi kwani hataki kuona vitendo vyaubadhirifu katika  mkoaa wake na kuona haki inatendeka kwa wananchi hao.

“Sitaki kuona kigogo wala kijiti anahusika katika mradi huu.
Nitasimamia na polisi waliohusika katika kuwatoa wananchi hawa waseme walitumia vigezo gani kuwatoa,”alisema.

Alisema wananchi walioondolewa eneo hilo wafike kwenye ofisi za mkuu wao wa wilaya huku akiiagiza TAKUKURU kutekeleza majukumu yao katika suala hilo ili wananchi wapate haki zao.

Makonda alisema yuko tayari kuhakikisha kwamba haki za wananchi hao zinapatikana pamoja na wale wa mradi mkubwa wa kuendeleza mji mpya wa Kigamboni (KBD).

Mkuu huyo wa mkoa alisema zipo dalili za kuwepo kwa ufisadi mkubwa katika miradi mingi ya ulipaji fidia katika maeneo ya Kigamboni na kwamba, baadhi ya nyaraka ameziwasilisha TAKUKURU kwa uchunguzi zaidi, zikiwemo za mradi wa KABD.

“Nilibani kwamba baadhi ya nyaraka za fidia zina sahihi tofauti tofauti na mihuri tofauti, ingawa  mtu aliyetakiwa kusaini ni mmoja tu. Lakini pia kuna hofu kwamba, baadhi ya watumishi wasiowaaminifu wanashirikiana a wananchi kuandika uthamini wa uongo, ikiwemo kuandika kama mtu mmoja anamiliki nyumba zaidi ya mbili wakati kiuhalisia anayo nyumba moja tu,”alisema Makonda.

Alisema pia wapo watumishi waliosimamia miradi hiyo, ambao wanaandika viwango vya malipo visivyo sahihi kwa kuwadhulumu haki wananchi.

“Nyaraka tulizozitilia wasiwasi, nimeziwasilisha TAKUKURu. Zinachunguzwa na majibu yatatoka.Tunataka kila mwananchi Kigamboni alipwe haki yake anayostahili na mtalipwa,”alisema Makonda.

No comments:

Post a Comment