Monday 21 November 2016

SHAKA AWASHA MOTO UVCCM

KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, amesema mtendaji au kiongozi wa jumua hiyo,  atakayeshindwa kuwa mbunifu, kuibua mambo  au kutofanya kazi kwa kufuata kanuni, atakuwa amepungukiwa sifa za kuendelea kuwa kwenye dhamana aliyonayo.

Amesema miongoni mwa mambo anayopaswa kuyasimamia ni pamoja na utekelezaji wa malengo ya serikali yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Shaka alitoa matamshi hayo jana, mjini hapa, ambapo alisisitiza kuwa UVCCM inakoelekea hivi sasa haitamuonea haya wala soni, mtendaji au kiongozi atakayeshindwa kuonyesha uwezo wa kuisaidia jumuia hiyo kimaendeleo.

Kaimu Katibu Mkuu alisema hayo mwishoni mwa wiki, baada ya kuzindua jengo jipya la ofisi ya UVCCM, lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 10.400, zilizotokana na michango ya fedha taslimu na vifaa kutoka kwa wadau na nguvu kazi ya vijana wa Simanjiro, mkoani Manyara.

Alisema kitendo cha kijana kukabidhiwa jukumu ndani  ya UVCCM, anahitaji kujivunia hadhi aliyopewa na pia aone fahari katika maisha yake kwa kubahatika kuitumikia taasisi ya Chama kinachoongoza nchi.

"Ikiwa umepata dhamana ya kiutendaji au kuwa kiongozi, shirikiana na wenzako. Washirikishe katika utekelezaji wa majukumu, kataa kufanya uamuzi kwa hiyari au  utashi wako, utendaji wa pamoja una faida kuliko uamuzi binafsi,"alisema.

Kaimu Katibu Mkuu aliusifu uongozi wa UVCCM  mkoa wa Manyara, hususani watendaji na wajumbe wa kamati ya utekelezaji na Baraza Kuu la Wilaya ya Simanjiro, kwa kuonyesha umoja ulioleta mafanikio kwa kubuni, kujenga na kumaliza jengo hilo jipya la kisasa

"Kaa katika nafasi yako ya utendaji au uongozi ili siku moja ukiondoka wenzako wakukumbuke, historia ikuandike na kukuenzi. Huwezi kupendwa na wote, ila asilimia kubwa ikutaje kwa mema kuliko mabaya. Tunataka ubunifu badala ya majungu na kugawa watu,"alisema.

Aidha, Shaka alisema wapo baadhi ya wanajumuia huyo wanaofikiri ili awe  kiongozi, analazimika kuwa hodari wa kuwagawa watu, kupika majungu, kueneza maneno yanayoleta mgawanyiko huku akiwa hana uwezo wa kutimiza majukumu aliyokabidhiwa katika ngazi yake.

Alisema aina hiyo ya viongozi hawatapata nafasi tena ndani ya UVCCM, kwa kuwa hivi sasa umoja huo utachuja na kupembua nani ana dhamira njema, nia thabiti, uwezo na uaminifu wa kuitumikia jumuia hiyo na si vinginevyo.

"Mara nyingi kila mtoto anayebebwa mbelekoni, hukitazama kichogo cha mama yake. Kiuongozi au mtendaji wa UVCCM, naye aitazame spidi ya serikali ya CCM, kisha ajipime kama anatosha au la, kama hawezi aseme ili apumzishwe kuliko kuboronga,"alisisitiza Shaka.

No comments:

Post a Comment