WATU 11 wakiwemo madiwani wawili wa CCM na CHADEMA, wanashikiliwa na polisi wilayani Karatu kwa kuharibu mali, zikiwemo mashine zaidi ya 10, za kunyonya maji kwa kuzipondaponda na kuzichoma moto kwa madai zimewekwa kwenye vyanzo vya maji.
Mbali na hilo, watu hao wakiwemo madiwani, wanadaiwa kuteketeza kwa moto kibanda umiza kimoja.
Hadi sasa mashine zilizothibitika kuchomwa moto ni tano, tatu zikiwa za Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Wilaya ya Karatu, Daniel Awakii na mbili za Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Karatu, Mustafa Mbwambo.
Nyingine ni mashine za wakulima, ambao wote wameitwa polisi kwa ajili ya kuandikisha maelezo.
Mapema jana, Mbunge wa Karatu, Willium Qumbalo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilet Mnyenye, waliitwa Kituo cha Polisi Karatu kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na sakata hilo.
Tukio hilo linatokea siku chache baada ya kumalizika kwa ziara ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, ambaye alipokea kilio cha wananchi wa vijiji vinavyotumia maji hayo vikiwemo Qamndet, Barazani, Dumbechan, Maleckchand na Laghangareri, ambapo aliagiza uongozi wa serikali ya mkoa na wilaya, kuhakikisha ndani ya siku moja mashine zote zilizoko katika vyanzo vya maji zinaondolewe na kuwekwa umbali ya mita 60.
Akithibitisha kukamatwa kwa watu hao 11, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema wanakabiliwa na kosa la kuhamasisha wananchi kwenda kufanya uharibifu huo, lakini juzi, kabla ya kukamatwa, walionywa juu ya harakati zao hizo, zilizosababisha kuharibiwa kwa mali hizo.
Mkumbo alisema juzi, asubuhi watu hao wakiwemo madiwani, waliendelea kuwahamasisha wananchi kwenda kutenda kosa hilo, licha ya kuwa walionywa, jambo ambalo lilisababisha jeshi la polisi kuwatia mbaroni.
Aliwataja madiwani hao wawili kuwa ni Lazaro Gege wa Kata ya Mang’ola Barazani (CCM) na Moshi Darabe wa Kata ya Baray (CHADEMA) na kusisitiza kuwa, mashine zilizoharibiwa na kuchomwa moto hazikuwa katika vyanzo vya maji kama inavyodaiwa na wananchi na madiwani hao.
Mkumbo alisema mbali na uharibifu huo, wananchi hao waliingia na kuharibu mahindi shambani kwa kuyakanyagakanyaga, jambo ambalo linaweza kusababisha wilaya hiyo kukumbwa na baa la njaa kwa kuwa kwa kiasi kikubwa wilaya hiyo inategemea chakula kutokana na kilimo hicho.
Kamanda huyo wa polisi mkoa alisema pamoja na uharibifu huo, suala hilo linaonekana kuwa na mvutano kati ya pande mbili, ambazo wakati wote wa tukio, zilikuwa zikizomeana, ambapo upande mmoja ulikuwa ukidai kuwa, mashine hizo hazikuwa katika chanzo cha maji na upande mwingine ukidai zilikuwepo ndani ya chanzo.
Mkumbo alisema bado tathmini ya mali zilizoharibiwa inaendelea na watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa huku jeshi lake likiendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wa tukio hilo na pindi upelelezi utakapokamilika, wanatarajia kuwafikisha mahakamani.
Hata hivyo, wakati uharibifu huo unafanyika, imeelezwa kuwa, yapo makubaliano kati ya serikali na wataalamu kutoka Bonde la Kati Singida, waliofika wilayani humo kushughulikia kusogezwa mbele kidogo kwa utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu la kuondolewa kwa mashine hizo na kuwekwa umbali wa mita 100, kutoka chanzo cha maji ili kunusuru mazao hayo kukauka.
No comments:
Post a Comment