Sunday, 1 January 2017
SERIKALI YATOA ONYO KALI
SERIKALI imetoa onyo kali kwa watu wanaotumia kisingizio cha migogoro ya ardhi, kusababisha uvunjifu wa amani katika jamii.
Aidha, imesema tayari imewatia mbaroni watu 13, waliohusika na tukio la vurugu zilizosababisha kuchomwa mkuki kinywani na kutokea shingoni, mkulima Agustino Mtitu, akiwemo aliyetenda tukio hilo.
Onyo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipokuwa akifungua semina kwa waandishi wa habari, iliyoandaliwa na wizara yake mjini Morogoro.
Lukuvi alisema wapo watu wanaojificha kwenye kivuli cha migogoro ya ardhi, kutenda uhalifu, hususan kwa kufanya vurugu na kudhuru watu, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Alisema serikali haitamvumilia wala kumfumbia macho yeyote atakayebainika kuhusika na uvunjifu wa amani kwa kisingizio hicho na kwamba, wanaohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Kilichotokea hivi karibuni huko Mikumi siyo suala la mgogoro wa ardhi, ule ni uhalifu, ambao hauwezi kufumbiwa macho. Tutachukua hatua kali kila tunapobaini kuwepo kwa watu wanaotaka kuchochea vurugu kwa kisingizio hicho.
“Tunatambua kwamba wapo wafugaji wanawatumia watu kusababisha hali ya kutoweka kwa utulivu, hususan kwa kuwatuma walishe mifugo bila ya kuzingatia haki za wengine, hilo halikubaliki,”alisisitiza.
Waziri Lukuvi alisema serikali itaendelea kupambana na wanaotekeleza matukio ya fujo kupitia mgongo wa ardhi, kwa kuwa ni ukiukaji wa sheria na kusababisha wengine washindwe kuishi kwa amani na utulivu huku wakiendeleza shughuli zao za maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Steven, alisema tayari watu 13, wametiwa mbaroni kutokana na tuhuma za kuhusika na vurugu hizo za Mikumi, zilizosababisha mtu mmoja kuchomwa mkuki kinywani na wengine kujeruhiwa.
Dk. Kebwe alisema watu hao wanaendelea kuhojiwa na kwamba, mamlaka zinazohusika zitakapokamilisha kazi yao, watafikishwa mahakamani.
“Serikali mkoani Morogoro ipo macho na ipo imara. Yeyote atakayetenda jambo kinyume na sheria, tutamchukulia hatua stahili. Waliohusika na vurugu zile tunaendelea kuwasaka,lakini mhusika mkuu tayari tumeshamtia mikononi na wenzake tukiendelea kuwahoji,”alisema.
Kukamatwa kwa watu hao kunatokana na tukio hilo lililodaiwa kusababishwa na wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment