Sunday, 1 January 2017
TAKUKURU YAWASAKA WALIOFICHA MKATABA WA ZANTEL
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na polisi, wanawasaka vigogo walioficha mkataba wa Kampuni ya Zantel na Manispaa ya Kinondoni.
Kampuni hiyo tayari imeilipa manispaa hiyo kiasi cha sh. milioni 627.
Tamko hilo lilitolewa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Happi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na taarifa ya ufisadi uliokuwa unaikabili Zantel, tangu mwaka 2009.
Happi alisema serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha wale wote waliohusika kuuficha mkataba huo katika Manispaa ya Kinondoni, wanapatikana.
“Tutahakikisha tunawabaini waliohusika kuuficha mkataba wa Kampuni ya Zantel kwa muda wa miaka saba katika Manispaa ya Kinondoni na kusababisha kushindwa kuipa manispaa hiyo mapato kwa kipindi chote hicho,” alisema.
Pia, aliipongeza kampuni hiyo kwa kutii agizo lililotolewa na kulipa fedha hizo.
Happi alisema kutokana na ulipaji huo, Manispaa ya Kinondoni kwa sasa tayari imewapa risiti ya malipo ya fedha hizo, ambapo zililipwa Desemba 23, mwaka huu.
Happi alisema baada ya kuwabaini watu hao, watajibu tuhuma za kuisababishia serikali upotevu wa mapato kwa miaka hiyo saba na sababu za kutoonekana kwa kumbukumbu ya mkataba katika manispaa hiyo.
Alizitaka kampuni zilizoingia mkataba na manispaa yoyote Dar es Salaaam, kuhakikisha zinalipa madeni yao mapema katika manispaa husika.
“Mwenye mkataba na serikali tambueni ya kuwa tumeanza msako na endapo tukiwabaini, tambueni mtatakiwa kulipa fedha zote bila kujali nani kasababisha,” alisema.
Pia, alisema fedha zilizolipwa zitatumika kujenga vyumba vya madarasa 40, katika Manispaa ya Kinondoni, ambapo kila darasa litagharimu sh. milioni 17.
“Manispaa ya Kinondoni tuna upungufu mkubwa wa vyuma 79, vya madarasa, hivyo kupitia fedha iliyolipwa na Zantel, tutahakikisha tunajenga vyumba 40, vya madarasa, ambapo kila kimoja kitagharimu shilingi milioni 17,”alisema.
Alisema ujenzi huo wa madarasa ni moja ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuwataka wakurugenzi kuhakikisha kila mwanafunzi aliyefaulu anapata shule.
Dhamira nyingine, Happi alisema ni kuhakikisha wanatekeleza nia ya Rais Dk. John Magufuli ya kutaka kila mwanafunzi apate haki yake ya elimu bure.
Kutokana na hilo, Happi aliwataka wakurugenzi wote wa Dar es Salaam kujipanga kutekeleza maagizo hayo na ikifika Januari, mwakani, tayari kwa kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Hata hivyo, aliwataka maofisa elimu na wakurugenzi kuhakikisha wanatazama maeneo yaliyowazi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa madarasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment