Sunday, 1 January 2017

LEMA AZIDI KUNASA MAHAKAMANI


JINAMIZI la Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema la kukosa dhamana, limeendelea kumkalia vibaya baada ya kukwama kuanza kusikilizwa kwa rufani aliyoikata katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha.

Kukwama kuanza kusikilizwa kwa rufani hiyo jana, mbele ya Jaji Fatuma Masengi, kunatokana na upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Innocent Njau, kuieleza mahakama kuwa haupo tayari kwa usikilizwaji huo kwa kuwa  Novemba 11, mwaka huu, walitiia nia ya mdomo ya kukata rufani kupinga dhamana  ya mbunge huyo.

"Ni kweli mheshimiwa Jaji leo (jana), tumekuja mahakamani kusikiliza rufani iliyokatwa na upande wa utetezi, lakini kwa upande wetu hatupo tayari kusikiliza kwa kuwa tulishawasilisha nia ya kukata rufani Novemba 11 na Desemba 21, mwaka huu.Tuliwasilisha maombi ya rufani hiyo mahakamani na kupokewa na mahakama yako tukufu,” alidai Njau.

Rufani hiyo namba 126 dhidi ya dhamana ya Lema, ilikuwa imekwenda mahakamani hapo  kwa ajili ya kusikilizwa, baada ya Jaji Dk. Modesta Opiyo kutupa mapingamizi mawili  ya upande wa Jamhuri, Desemba 20, mwaka huu, kwa madai kuwa hayakuwa na mashiko kisheria.

Jaji Dk. Modesta baada ya kutupa pingamizi hayo, aliupa upande wa utetezi siku 10, kuwasilisha maombi ya rufani yao mahakamani hapo, ambapo walifanikiwa kuwasilisha maombi ya rufani siku hiyo.

Baada ya maelezo hayo, Jaji Fatma aliunga mkono hoja za upande wa Jamhuri, hivyo kuamuru rufani iliyokatwa na upande wa Jamhuri namba 135 kuendelea.

Hata hivyo, Njau aliiomba mahakama kuwapatia siku tatu ili waweze kuwasilisha hoja zao.

Maelezo hayo ya Wakili wa Serikali, kuomba kupatiwa siku tatu,  yalidhoofisha nguvu ya jopo la mawakili watano wa upande wa utetezi, likiongozwa na Peter Kibatala huku wakionyesha kusikitishwa na hatua hiyo.

Wakili Kibatala alidai upande wa Jamhuri kama umeweza kuwasilisha maombi ya rufani, ni dhahiri kuwa wapo tayari kuwasilisha hoja hizo.

“Mheshimiwa Jaji nadhani upande wa Jamhuri umewasilisha rufani yao mahakamani hapa, naomba tuendelee, ni dhahiri wapo tayari siku tatu ni nyingi sana,”alidai Kibatala.

Baada ya kuwasilikiza mawakili wa pande zote husika, Jaji Fatma aliutaka upande wa Jamhuri kuwasilisha hoja zao mahakamani hapo leo, na upande wa utetezi kujibu hoja hizo Desemba 30, mwaka huu na Januari 2, mwakani, pande zote zitakutana kwa ajili ya hoja za nyongeza.

“Mwanasheria wa serikali kesho (leo), naomba uwasilishe hoja zako mahakamani hapa na upande wa utetezi uwasilishe majibu  Desemba 30, mwaka huu na  Januari 2, mwakani, tutakutana kwa ajili ya hoja za nyongeza," alisema Jaji huyo na kuongeza kuwa, uamuzi wa shauri hilo atautoa Januari 4, mwakani.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri umetia nia ya kukata rufani katika Mahakama ya Rufani Tanzania, kupinga uamuzi wa Jaji Dk. Modesta  wa kuwapa siku 10, mawakili wa Lema kuwasilisha rufani yao katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Hoja za rufani zinazotolewa uamuzi ni kufuatia uamuzi uliotolewa Novemba 11, mwaka huu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa madai sheria haizuii kumpa dhamana mtuhumiwa wa kesi ya uchochezi, lakini kabla ya kutoa masharti ya dhamana, mawakili wa serikali waandamizi, Paul Kadushi na Wakili Mfawidhi wa Serikali mkoani Arusha, Maternus Marandu, walipinga kumpatia dhamana Lema kwa madai wameonyesha nia ya mdomo ya kukata rufani dhidi ya dhamana hiyo.

Baada ya hoja hizo, Hakimu Kamugisha aliahirisha kesi hiyo kwa dakika 10, kwa ajili ya kupata ushauri wa kisheria na baada ya kurejea, alisema kutokana na upande wa Jamhuri kutia nia ya kukata rufani, Lema hawezi kupata dhamana na kuamuru arudishwe Gereza la Kisongo.

Baada ya kesi hiyo kumalizika, mawakili wa Lema waliandika kuiomba mahakama kufanya marejeo ya kesi hizo mbili  440 na 441, ambapo maombi hayo yalipokelewa na kusikilizwa mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi Sekela Moshi, Novemba 14, mwaka huu, ambaye alitupa maombi yao na kuwaeleza kuwa walitakiwa kuta rufani na siyo kuiomba mahakama kufanya marejeo kwa kuwa walikuwa ndani ya muda.

Hata hivyo, mawakili hao bada ya maombi yao kutupwa, waliendelea kukaza buti na kukata rufani siku hiyo hiyo na Desemba 2, mwaka huu, ilitupwa na Jaji Mfawidhi  Fatuma Masengi kwa madai ilikuwa nje ya muda.

Pamoja na kutupwa tena, mawakili hao walipeleka ombi Mahakama Kuu, kuomba kuongezewa muda wa kupeleka notisi ya kukata rufani yao juu ya dhamana ya mteja wao  na hatimaye Desemba 20, Jaji Dk. Modesta alikubali na kuwaongezea muda wa siku 10 na siku hiyo walifanikiwa kukata rufani yao.

No comments:

Post a Comment