Wednesday, 28 December 2016

AMUUA MWENZAKE WAKIGOMBEA SODA

MTUMISHI wa Kampuni ya Upishi na Ulishaji katika sherehe ya ZZ Cartering ya Jijini Arusha,  Novatus Thadei (26), amefariki dunia kwa kuchomwa kisu kifuani na mtumishi mwenzake, Hamis Msoffe (16).

Tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, katika ugomvi wa kugombea soda walizopewa na tajiri yao kwa ajili ya sikukuu ya Krismas.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, ikiwa ni muda mfupi baada ya wafanyakazi hao kumaliza kuhudumia chakula cha sikukuu.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, tajiri wa wafanyakazi hao aliamua
kuwapongeza kwa kazi nzuri kwa kuwagawia soda.

Akizungumzia tukio hilo, lililotokea eneo la Kwamromboo, Kamanda Mkumbo alisema tajiri yao huyo alipohakikisha kazi hiyo imemalizika, aliamua kuwagawia soda moja moja kila mmoja, lakini Hamis alichukua soda ya mtumishi mwenzake na kuificha ndani ya begi, ambapo marehemu alianza kuitafuta bila mafanikio.

"Unajua wakati Hamis anaficha hiyo soda kwenye begi, kumbe marehemu alikuwa akimuona,  lakini akaanza kuuliza nani kanywa soda yake, lakini hakuna aliyemjibu, ndipo alipomtaja Hamisi kuwa ndiye aliyeichukua na ndipo walipokamatana kwa ugomvi,”alisema Mkumbo.

Alisema baada ya Hamis kunyooshewa kidole kwa yeye ndiye aliyeiba soda hiyo, walishikana mashati huku wakipigana, lakini baada ya Hamis, ambaye ni mdogo kwa umri, kuzidiwa nguvu na marehemu, alikimbilia eneo lililokuwa na visu vya upishi na kisha kumchoma nacho marehemu kifuani.

Kamanda Mkumbo alisema Hamis anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili, likiwemo la mauaji.

Wakati huo huo, mtoto Cliford Alex (12), mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Sekei, jijini Arusha, amefariki dunia wakati akiogelea kwenye bwawa la kuogelea la Hoteli ya Kitalii ya Mount Meru.

Kamanda Mkumbo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi, ambapo alisema mtoto huyo alifariki dunia kutokana na kujirusha katika bwawa hilo eneo la kina kifupi na kujigonga kichwani katika sakafu.

Alisema marehemu alikuaw akiogelea na watoto wenzake, lakini walipoona mwenzao kajirusha kama samaki katika bwawa hilo, walishangaa kuona amekaa ndani ya maji kwa muda mrefu bila kuibuka na ndipo walipopiga kelele.

Alisema baada ya wazazi na wafanyakazi wa hoteli hiyo kufika katika bwawa hilo, waliona maji yakiwa na rangi nyekundu, ikiashiria kuchanganyika na damu, ndipo walipoingia na kukuta mtoto huyo akivuja damu nyingi huku akiwa amepasuka kichwani.

No comments:

Post a Comment