Wednesday, 28 December 2016
MAJALIWA KUMWEKA KITIMOTO KIGOGO
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema atamuita Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Hassan Jarufo, amueleze ni kwa nini wakulima wa zao hilo wanacheleweshewa malipo yao kinyume na maagizo ya serikali.
Alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lindi, baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo, wilayani Nachingwea.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwasili wilayani Nachingwea, akiwa njiani kwenda Ruangwa, kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Niliagiza wanunuzi waje na dhamana za mauzo, waziweke benki, ndipo waingizwe kwenye mnada. Kwa maana hiyo mnada ukimalizika, benki inakata fedha husika na kuingiza kwenye chama cha wakulima,”alisema Majaliwa.
Aliongeza: “Hapa tatizo ni kwamba, hatukusimamia vizuri suala hili. Tulipaswa tujiridhishe kwanza kama mnunuzi amelipa fedha benki."
Waziri Mkuu aliongeza: "Tatizo la biashara hii watu wengi ni madalali, wanaangalia hali ikoje na wakibaini kuna cha juu, ndiyo anaagiza na kuamua kuja kulipa. Kama angekuwa amelipa benki, ile hela ya awali ingekatwa katika fedha ya dhamana aliyokwishaitoa.”
Oktoba 16, mwaka huu, wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye uwanja cha Sokoine, wilayani Nachingwea, Majaliwa alisema alishatoa maelekezo tangu Aprili, mwaka huu, kwamba, wanunuzi wa korosho ni lazima watoe asilimia 25 ya malipo wanayotaka ili kuepuka tatizo la madalali kuingilia kati biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na wakuu wote wa wilaya za mkoa huo, wawahimize wakulima wapande miche mipya ya korosho kwa sababu mikorosho iliyopo imezeeka na haitoi mazao ya kutosha.
“Mnatakiwa muwahimize wananchi wapande miche mipya mara tu mvua zitakapoanza ili ianze kukua wakati wakusubiria kung’oa ile ya zamani. Nimeambiwa korosho bora hazipaswi kuzidi punje 190, ili zijae kwenye kilo moja. Ubora wa miti ya korosho ukishuka na idadi ya punje pia inapungua,”alisema.
Aliongeza kuwa kigezo kikuu cha ununuzi wa korosho hivi sasa ni idadi ya punje na kwa Ruangwa na Nachingwea, idadi inakuwa kubwa kwa sababu punje zake ni ndogo.
“Wenzetu wa Tandahimba walipanda miche mipya tangu miaka minne iliyopita, kwa hiyo sasa hivi wanavuna korosho zenye ubora,” alisema Majaliwa.
Alimpongeza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, kwa uamuzi wake wa kuvunja Mfuko wa Wakfu wa Korosho (CIDTF) na akamtaka afute mifuko kama hiyo kwenye mazao mengine, yakiwemo
katani, chai na kahawa, kwani inafanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na bodi za mazao hayo.
“Waziri Tizeba alishaanza na zao la pamba, sasa aende kwenye mazao mengine ili fedha, ambazo watu wa mfuko huu walikuwa wakizitumia kulipana posho, sasa ziende kwenye bodi kuhamasisha wakulima walime zaidi na ikibidi wapewe hata mashine za kupulizia dawa,” aliagiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment