Tuesday, 27 December 2016

NAPE AWAONGOZA WANAHABARI KUMUAGA BUKUKU








WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye , jana aliwaongoza mamia ya wananchi kuuaga mwili wa mpigapicha wa magazeti ya Guardian na Nipashe, Mpoki Bukuku.

Shughuli za kuuaga mwili wa Mpoki, zilifanyika jana jioni, kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Wazazi, Tabata Kimanga, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Mpoki, alifariki dunia Ijumaa iliyopita, alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, baada ya kugongwa na gari katika maeneo ya Mwenge.

Hadi mauti yalipomkuta, akiwa na umri wa miaka 44, Mpoki alikuwa mpigapicha wa magazeti ya The Guardian. Awali, aliwahi kufanyakazi katika  kampuni za Business Times na Mwananchi.

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili wa marehemu, Nape alisema kifo cha Mpoki kimeacha pigo kubwa katika familia yake na tasnia ya habari.

Alisema amemfahamu Mpoki siku nyingi na mchango wake ni mkubwa katika tasnia ya habari.

Alisema tasnia ya habari itaenzi mchango wa Bukuku kupitia kazi zake kwa kuwa mbali na misukosuko ya kikazi, alikuwa ni mwalimu kwa wapigapicha mwenye kuzingatia maadili.

"Bukuku ameacha pengo kubwa hivyo hatosahaulika. Wanahabari hatuna cha kufanya ila tunamshukuru Mungu na kupitia kazi zake tujifunze yale yote aliyoyafanya," alisema.

Nape alisema wanahabari wengi wamepita katika mikono yake na alikuwa akifanya kazi kwa lengo la kukuza na kusimamia fani hiyo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya The Guardian, Richard Mwigamba, alisema kifo cha Bukuku ni pigo kwa kampuni kutokana na utendaji wake uliokuwa mfano kwa wengine.

Alisema The Guardian hawana la kusema zaidi ya kumuombea na kuitaka familia kuishi kwa kumtumainia Mungu.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la  Wahariri (TEF), Deodatus Balile aliitaka serikali kutumia kifo cha Bukuku kujitathmini upya katika kuwathamini waandishi na kazi zao.

Alisema kitendo cha kuendelea kuwatesa waandishi wa habari hadi kufikia kuwekwa ndani na wakuu wa wilaya, kinawadhalilisha na kusahahu mchango wao kwa jamii katika haki ya kutoa habari.

"Bukuku ni mfano wa walioteswa katika fani hii wakati akitekeleza majukumu yake. Serikali kupitia sheria mpya ya habari, itunge kanuni za kulinda haki za wanahabari na iwe kiama kwa wakuu wa wilaya wawekwe wao ndani,’’alisema Balile.

Mwakilishi wa wapigapicha nchini, Suleiman Mpochi, alisema Bukuku ni alama isiyofutika duniani.

Alisema Bukuku hakuwa mchoyo wa taaluma, amefundisha wengi na kusaidia katika kupata ajira, hivyo kifo chake ni pigo katika tasnia na jamii kwa ujumla .

Viongozi wengine walioshiriki kumuaga marehemu Mpoki ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saeed Kubenea.

Marehemu Mpoki anatarajiwa kuzikwa leo, katika makaburi ya familia yaliyoko eneo la Msalato, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment