Tuesday, 27 December 2016

CCM YAIBOMOA CHADEMA

KASI ya viongozi na wanachama wa CHADEMA kukihama chama hicho na kujiunga na CCM katika maeneo mengi nchini, inazidi kuongezeka huku wengi wakitoa sababu ya kubakwa kwa demokrasia ndani ya chama hicho na kuchoshwa na sera zisizo na mashiko.

Hivi karibuni, viongozi watatu na wafuasi wawili waliokuwa tegemeo ndani ya CHADEMA katika Jimbo la Segerea, Ilala, Dar es Salaam, walikihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Viongozi hao walisema wamefikia uamuzi huo kutokana na ubabe, ufinyu wa demokrasia na kuukubali utendaji wa Rais Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Waliohama ni aliyekuwa mjumbe wa Kamati Tendaji (CHADEMA) Jimbo la Segerea, Daniel Ndegetu, Katibu wa Baraza la Wazee la CHADEMA jimboni humo, Joel Sasabo na Katibu kata wa CHADEMA kata ya Kimanga, Mwalimu Antony Gella.

Wengine ni  Samweli Lyimo na Joseph Shausi, ambao kwa pamoja  walikiri kwamba, hali siyo shwari ndani ya chama hicho, hususan jimbo la Segerea.

Akihutubia viongozi na wanachama wa CCM wa Jimbo la Segerea, wakati wa hafla ya kuwapokea, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, aliwapongeza kwa uamuzi huo  na kuongeza kuwa, hayo ni matunda ya  utendaji bora wa Rais Dk. Magufuli.

“Nimeambiwa kuwa nyie ndiyo mlikuwa mkiiletea matatizo makubwa CCM mlipo kuwa CHADEMA, hivyo tunaamini ni wawajibikaji wazuri,  tunaomba muendelee kufanya hivyo mkiwa CCM,”alisema Madabida.

Alisema CCM ni Chama kinachoongozwa kwa misingi ya demokrasia, katiba na sera na kwamba, mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanyika ndani ya Chama yanalenga kukirudisha katika reli ili kiweze kuwatumikia Watanzania wote.

“Ni wakati wa  siasa za kuwatumikia wananchi. Mabadiliko yanayofanyika yanahitaji tubadilike kifikra,” alisema Madabida.

Pia, aliwataka watendaji wa CCM na wanaohitaji kuwania nafasi za uongozi ndani ya Chama, kujitathmini na kuacha tabia ya kung’ang’ania madaraka.

“Kama ni kiongozi na umeongoza na kujiona huwezi, basi waachie wengine. Ukiendelea kung’ang’ania utaua Chama. Mabadiliko ndani ya CCM ni makubwa, hivyo ni lazima tuyatumie kujipima,”alisema Madabida.

Akizungumza  kwa  niaba ya wenzake, baada ya kuapishwa na kukabidhiwa kadi za CCM, Mwalimu Gella alisema utendaji bora wa Rais Dk. Magufuli na Katibu Mkuu Kinana, umewavuta.

“CHADEMA wameishiwa sera, anayoyafanya Rais Dk. Magufuli ndiyo tulikuwa tukiyapigia kelele, ikiwemo watumiashi hewa, ufisadi na maisha bora kwa Watanzania wote, lakini sasa  CHADEMA wanaupa mgongo ukweli,”alisema Gella.

Alimshutumu aliyekuwa Mbunge wa Segerea, Dk. Makongoro Mahanga, kuivuruga CHADEMA na kwamba, hali ndani ya chama hicho mkoa wa Dar es Salaam sio shwari kwani viongozi wamekuwa wakiikanyaga katiba yao.

“Viongozi wa CHADEMA mkoa na wilaya wakiongozwa na Dk. Mahanga wamekuwa wakipanga safu ya watu wanaowataka wao huku wakiendekeza ubabe ndani ya chama,” alisema.

No comments:

Post a Comment