Tuesday, 27 December 2016

UVCCM YAWATUNUKU VYETI RAIS MAGUFULI NA KINANA


UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umewatunuku vyeti vya heshima vya kutambua utumishi bora, ujasiri na uzalendo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu wake, Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana.

Pia, umewahimiza viongozi wengine wa Chama na jumuia zake, kufuata nyayo za utendaji, utumishi na umakini walionao viongozi hao kwa kuthubutu kukipigania na kukitetea Chama  mahali popote.

Vyeti hivyo vilitolewa juzi na UVCCM wilaya ya Bukoba Vijijini na kumkabidhi Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka, alipoitembelea wilaya hiyo kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kata ya Kimondo mjini hapa.

Aidha, vyeti hivyo vilivyotiwa saini kwa pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Bukoba Vijijini, Evith Barongo na Katibu wa UVCCM wilayani humo, Emmanuel Shitobelo, pia vilitolewa kwa viongozi wengine wa juu wa CCM ngazi ya taifa.

Viongozi wengine waliopewa vyeti hivyo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula, aliyekuwa Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadifa Juma Khamis.

Akisoma maelezo kabla ya kukabidhi vyeti hivyo, Shitobelo, alisema wamemtunuku Mwenyekiti wa CCM Dk. Magufuli kutokana na ujasiri wake katika kukomesha ufisadi, uvivu na uzembe maeneo ya kazi, kurudisha nidhamu, uwajibikaji, uwazi na jinsi anavyowatetea wananchi masikini.

"Amepatikana kiongozi mwenye dhamira na uthubutu, mzalendo, anayependa watu wafanye kazi, wajitume na kutumia vyema rasilimali za taifa. Hatutaacha kumuenzi na kusifu juhudi zake,"alisema.

Shitobole alimtaja Mangula kwamba, ni kiongozi aliyeonyesha umakini katika kusimamia maadili, miiko, kanuni, katiba na kwamba, amekuwa hayumbi katika kuelezea dhamira na malengo ya CCM kisera na kiutaratibu.

Alisema UVCCM wilayani humo wanayo kila sababu ya kuwaenzi na kutambua mchango waliotoa viongozi hao na kutaka wengine waige na kupita juu ya nyayo zao.

Shitobole alimweleza Shaka kwamba, Katibu Mkuu Kinana baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alifanya kazi kubwa ya kukirudisha Chama kwenye misingi yake na kukubalika na wananchi.

"Pengine bila ya juhudi za Kinana, hapa tulipo sasa kisiasa tusingekuwepo. Amefanya kazi kubwa ya kurudisha  matumaini yaliyofifia, ametembea karibu nchi nzima, kijiji kwa kijiji, huyu ni jasiri na hodari,"alieleza Shitobole

Pia, cheti kingine amepewa Nape,  aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, ambaye alitajwa kama kijana akiyeshiba na kuhifadhi sera za Chama, kuijua itikadi na kukitetea na pia ni mahiri wa kujenga nguvu ya hoja.

"Tumemtunuku cheti Nape kwani aliposhika wadhifa huo, amekuwa mahiri wa kujibu na kuchambua hoja, kujibu mapigo  ya upotoshaji toka upinzani kwa wakati, ni kiongozi aliyeshiba dhana na itikadi ya siasa ya ujamaa na kujitegemea,"alisema.

UVCCM  pia imempongeza kwa dhati Mwenyekiti wa UVCCM Taifa na Mbunge wa Donge, Sadifa kwa kuituliza jumuia na sasa inapata heshima ya pekee mbele ya Chama na serikali.

Sadifa ametajwa kuwa, chini ya uongozi wake, jumuia imejipambanua, imerudisha heshima, imesimama kama jeshi kamili la Chama huku vijana wakiwa na umoja kuliko wakati mwingine wowote.

"Tumemtunuku cheti pia mwenyekiti wetu wa Taifa kwa sababu bila yeye jumuia ingeyumba, isingepata heshima kama iliyonayo sasa, chini ya uongozi wake yapo mambo ya kujivunia na kukumbukwa,"alisema katibu huyo.

Shaka alimaliza ziara ya siku nane mkoani Kagera, mwishoni mwa wiki, ya kukagua uhai wa jumuia, Chama na kuzindua miradi ya maendeleo katika wilaya zote mkoani humu.

No comments:

Post a Comment