Tuesday, 27 December 2016
MAPIGANO WAKULIMA NA WAFUGAJI YAZUSHA BALAA, MKULIMA ACHOMWA MKUKI MDOMONI NA KUTOKEZEA SHINGONI
MKULIMA Agustino Mtitu, amenusurika kifo baada ya kuchomwa mkuki mdomoni na kutokezea shingoni.
Aidha, watu wengine wanane wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, kufuatia kuzuka kwa mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Dodoma Isanga, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi, lilitokea juzi, saa tano asubuhi, katika kijiji cha Dodoma Isanga, kilichoko kata ya Masanze.
Akizungumiza tukio hilo, mmoja wa wakulima, mkazi wa kijiji hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Stanley George, alisema akiwa katika shughuli zake za uchomaji mkaa, alisikia kelele zikipigwa na baadhi ya wananchi wakilalamikia wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya mahindi.
Alisema baada ya hali hiyo, Mtitu alifika katika eneo hilo kuwahoji wafugaji hao sababu za kuingiza ng'ombe kwenye mashamba ya wakulima.
George alisema baada ya kuwahoji wafugaji, mmoja wao alitokea kwa mbele na kumchoma mkuki mdomoni na kutokea upande wa pili wa shingo ya Mtitu.
Alidai kuwa baada ya wafugaji hao kufanya tukio hilo na kubaini kuwa wanakijiji wamegundua, walikimbia na kuacha mifugo yao shambani ikiwa imedhibitiwa.
Alisema dakika chache baadaye, wafugaji hao wanaochunga ng'ombe wa mfugaji mmoja wa jamii ya kimasai, waliyemtaja kwa jina la Sele, walirudi kwa lengo la kutaka kuteka ng'ombe zao, ndipo walipoanza kujeruhi wakulima wengine, akiwemo mwenyekiti wa kijiji.
Diwani wa kata ya Masanze, Bakari Pilo, akizungumzia tukio ilo kwa njia ya simu, alisema wafugaji hao walirudi kwa mara ya pili na kufanya shambulio kwa lengo la kuteka ng’ombe zao, ndipo walipowakata mapanga, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Stephano Daud, George Andrea na Mwenyekiti wa Kitongoji, Saimon Luhoga.
Pilo alisema baada ya kuona hali imekuwa mbaya, walifanya jitihada za kuwafikisha wananchi waliojeruhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, ambapo kati ya hao tisa, wakulima wanane walilazwa na mmoja aliyechomwa mkuki mdomoni alitakiwa kuwahishwa katika Hospitali ya Rufani Morogoro.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jacob, alikiri kupokewa kwa majeruhi huyo juzi na kusema kuwa, alipelekwa kwenye
chumba cha upasuaji na kufanikiwa kutolewa mkuki huo, ambao ulikuwa umekaa sehemu mbaya.
“Kutokana na jitihada za madaktari kufanya kazi nzuri, hali yake kwa sasa inaendelea vizuri na amelazwa wodi namba moja kwa ajili ya matibabu zaidi,”alisema Dk. Jacob.
Tukio la wafugaji kushambulia wakulima, limekuwa likitokea mara kwa mara kijijini hapo, ambapo Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule, aliiomba serikali kufanyia kazi suala hilo ili kupunguza mapigano ya wakulima na wafugaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulurich Matei, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, ofisi yake inaendelea kukusanya takwimu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment