Monday, 26 December 2016

VIONGOZI IGUNGA WACHANGANYANA KWA KUMDANGANYA RAIS MAGUFULI

 MKUTANO Maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, umeshindwa kutoa maamuzi kuhusu watendaji waliohusika kutoa taarifa za uongo kwa Rais Dk. John Magufuli kwamba haina upungufu wa madawati bali ina ziada ya 200.

Hali hiyo ilijitokeza mwishoni mwa wiki, baada ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Gordon Dinda, kutoa taarifa kwamba watendaji waliohusika na utoaji wa taarifa hizo kwa kiongozi mkuu wa nchi wameshaanza kuchukuliwa hatua.

Kufuatia taarifa hiyo, wajumbe wa mkutano huo maalumu uliolenga kujadili na kutolea maamuzi mazito taarifa hiyo ya uongo, walimjia juu kaimu mkurugenzi huyo kwa kumtaka awataje kwa majina walioanza kuchukuliwa hatua na kutaja hatua zilizoanza kuchukuliwa.

Madiwani hao walisisitiza kuwa, hawatakuwa tayari kuikubali taarifa hiyo iliyokuwa imetolewa nusu nusu bila kuwafahamu walengwa wa tatizo hilo na endapo ofisi ya mkurugenzi haitawataja.

Watendaji hao wanadaiwa walijihusisha kudanganya kuwa wilaya hiyo ina ziada ya madawati 200, badala ya kusema ukweli kwamba kulikuwa na upungufu wa madawati 1,507.

Pia, wajumbe hao hawakuridhishwa na namna watendaji walivyobadili vituo vilivyopangwa na ofisi za Bunge kwa ajili ya kuchukua madawati yaliyotolewa na serikali, badala yake kufikia uamuzi wa kutumia sh. milioni 23, kwa ajili ya kwenda kuyafuata madawati hayo bila  ridhaa ya kikao cha halmashauri.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Manonga, Hamisi Gullamali aliweka wazi kwamba, jukumu la halmashauri lilikuwa kutoa mafuta kwa ajili ya magari ya jeshi yaliyopangiwa kusafirisha madawati hayo na hapakuwa na barua yeyote ile iliyobadili vituo.

Diwani wa kata ya Mwamala, Athumani Henry, alionyesha kutoridhishwa na majibu yaliyokuwa yakitolewa na kaimu mkurugenzi mtendaji, hivyo kuwatahadharisha wajumbe wa mkutano huo kwamba, taarifa inayotolewa na watendaji ni ile waliyoiagiza wao.

Kwa msingi huo, alisema mpaka sasa uongozi huo hauna taarifa waliyoandaa kutetea upungufu wa madawati hayo.

Diwani wa Kata ya Igunga Mjini, Charles Kishepo, alibainisha kuwa maswali mengi yanayoulizwa na madiwani hao yanatokana na taarifa iliyowasilishwa kwenye mkutano huo kutokuwa na mchanganuo unaoeleweka.

Aliweka bayana kuwa makubaliano ya awali yalikuwa kutengeneza madawati kwa mkopo na malipo ya kila dawati moja walikubaliana iwe sh. 70,000, badala ya sh. 65,000, lengo likiwa ni kumshawishi mzabuni kukubali kutengeneza madawati hayo kwa mkopo.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Peter Onesmo alitumia fursa hiyo kuusisitiza uongozi wa halmashauri kutoa taarifa iliyochanganuliwa kikamilifu, badala ya hiyo waliyoitoa na kuzua maswali mengi miongoni mwa wajumbe.

Akitoa utetezi wa hoja hizo za wajumbe, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dinda, alikiri kwamba taarifa iliyowasilishwa katika kikao hicho ni maagizo waliyopewa kwenye mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani wa halmashauri na hakuna taarifa nyingine zaidi ya hiyo kutoka ofisini kwake.

Hata hivyo, baada ya mjadala mrefu kati ya wajumbe na mkurugenzi huku kila mmoja akitetea hoja yake, ndipo mkurugenzi huyo alipojikuta akiomba radhi kwa taarifa iliyowasilishwa kwenye mkutano huo.

Aliagizwa kuandaa taarifa nyingine na kuiwasilisha kikao kijacho itakayotaja majina kamili na hatua zilizoanza kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

No comments:

Post a Comment