Monday, 26 December 2016
RAIS MAGUFULI AFICHUA SIRI YA USHINDI WAKE
RAIS Dk. John Magufuli, amesema ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na zawadi ya rozali, aliyopewa na mtawa (jina halikumbuki) wa Kanisa la Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu la mjini hapa.
Amesema zawadi hiyo, ambayo imempa kibali cha kuiongoza Tanzania katika awamu ya tano ya serikali, ndiyo imesababisha aamue kusali misa ya Krismasi kwenye kanisa hilo kwa mwaka huu.
Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana, alipopewa nafasi ya kuzungumza na mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki, waliohudhuria misa maalumu ya krismasi kwenye hilo, lililoko katikati ya mji wa Singida.
“Katika kampeni zangu za mwaka jana, nilipita hapa mjini Singida na nilibahatika kuhudhuria misa ya kwanza Jumapili moja.
"Wakati natoka nje, nilikutana na huyo mtawa, ambaye aliniomba nikubali kuchua zawadi ya rozali na niitumie wakati wote wa kampeni ili inisaidie kushinda,” alisema na kushangiliwa na waumini hao.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli amewataka wakulima kuzitumia vizuri mvua chache za msimu huu kwa kulima mazao yanayostahilimi ukame ili kuepuka baa la njaa.
Aliwataka wazingatie ushauri wa wataalamu katika kilimo chao ili waweze kulima kisasa na kujipatia mazao ya kutosha kwa ajili ya familia zao.
Kwa upande wa wakulima mkoani Singida, aliwahimiza kulima alizeti kwa nguvu zote kwa kuwa zao hilo lina soko la uhakika ndani na nje ya nchi, kikiwemo kiwanda cha kukamua mafuta cha Mount Meru.
Awali, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Mhashamu Edward Mapunda, aliwataka wakazi wa mkoa huo kutambua kuwa kuharibu mazingira ni dhambi kubwa.
Askofu Mapunda alisema hali iliyopo sasa ni mbaya mno kwa sababu shughuli za kibinadamu zimeleta madhara makubwa kwenye mazingira kiasi cha kutishia nchi kugeuka kuwa jangwa.
Kiongozi huyo wa kiroho alisema ni vyema Watanzania waanze kujenga utamaduni wa kupanda miti ya kutosha katika matukio mbalimbali na maadhimisho yakiwemo ya kijamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment