Thursday, 16 March 2017

RAIS SABA WA PAKISTAN, SRILANKA KIZIMBANI DAR





RAIA saba kutoka Pakistan na Sri-Lanka, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma uhujumu uchumi kwa kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya sh. milioni 459.

Washitakiwa hao, ambao walifikishwa mahakamani hapo jana na TCRA, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ni raia wanne wa Pakistan, Dilshad Ahmed (36), Rohail Yaqoob (47), Khalid Mahmood (59), Ashfaq Ahmad (38), Muhamad Aneess (48), Imtiaz Ammar na raia mmoja wa Sri-Lanka, Ramesh Kandasamy.

Ahmed na wenzake walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri, ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Johannes Karungula kutoka TCRA, waliwasomea mashitaka saba.

Mashitaka waliyosomewa ni kula njama, kujipatia kwa udanganyifu huduma za mawasiliano, kuendesha huduma za mawasiliano bila kuwa na leseni kutoka TCRA, kuingiza na kusimika vifaa vya mawasiliano bila ya leseni, kutumia vifaa ambavyo havijadhibitishwa na mamlaka hiyo na kuisababishia TCRA hasara ya sh. milioni 459.

Katuga alidai kabla ya Novemba, 2016, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao  walikula njama ya kutenda kosa la matumizi ya huduma za mtandao kinyume cha sheria.

Pia, alidai tarehe tofauti kati ya Novemba, 2016 na Februari, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walijipatia huduma za mtandao kwa nia ya kukwepa gharama za malipo halali kwa kujipatia huduma hiyo kwa kutumia njia ya mawasiliano ambayo haijasajiliwa.

Aidha, wanadaiwa katika kipindi hicho, mkoani humo, waliendesha huduma za simu za kimataifa bila ya kuwa na leseni inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Shitaka la nne, washitakiwa hao wanadaiwa  Novemba 20, 2016, jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria, waliingiza nchini vifaa vya mawasiliano, ambavyo ni Sim Box, bila ya kuwa na leseni inayotolewa na mamlaka hiyo.

Washitakiwa hao wanadaiwa  tarehe isiyofahamika Novemba, 2016, Dar es Salaam, walisimika na kutumia vifaa vya mawasiliano, ambavyo ni Sim Box yenye namba 115200.8.n.t.n na kompyuta mpakato mbili aina ya Dell, bila ya kuwa na leseni kutoka TCRA.

Shitaka lingine washitakiwa hao wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Novemba 2016 na Februari, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu, walitumia vifaa hivyo vya mawasiliano kwa kuunganisha katika huduma ya mawasiliano kwa lengo la kupata  mawimbi  ya mtandao bila ya kuthibitishwa na TCRA.

Washitakiwa hao wanadaiwa  katika kipindi hicho, Dar es Salaam, kwa kutumia vifaa vya mawasiliano visivyosajiliwa, waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya sh. milioni 459.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa husikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa.

Hakimu Mashauri aliwataarifu washitakiwa hao kwamba, mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana, hivyo watatakiwa kuomba katika mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo iliahirishwa Machi 29, mwaka huu, ambapo washitakiwa hao walirudishwa rumande hadi tarehe hiyo, shauri hilo litakapopelekwa kwa kutajwa kutokana na upelelezi kutokamilika.

No comments:

Post a Comment