MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,
imesema kinachoendelea katika kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na mwenzake ni maajabu
matupu kutokana na upelelezi kuchukua miaka mitatu bila kukamilika.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alisema
hayo jana, mahakamani hapo, baada ya Mwendesha Mashitaka, Inspekta Hamis Said,
kudai upelelezi haujakamilika.
Baada ya Mwendesha Mashitaka huyo
kudai hayo, Hakimu Simba alitaka kujua maendeleo ya kesi hiyo, ambapo mwendesha
mashitaka alidai wapelelezi wanakamilisha mambo madogo madogo.
“Kinachoendelea ni maajabu matupu.
Kesi ililetwa kwa mara ya kwanza Mei 20, 2013, mpaka leo imekuwa ikiahirishwa
mara ngapi?
“Kama kuachiwa, waachiwe na kama
wanafungwa wafungwe, haipendezi miaka mitatu. Ikija mara nyingine, nakuja kuwaachia
washitakiwa wenu, hii sio haki,” alisema.
Awali, mdhamini wa Lwakatare, ambaye
hakuwepo mahakamani hapo, aliieleza mahakama kwamba, amelazwa katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili.
Kutokana na hilo, Hakimu Simba
alimueleza mdhamini huyo kumpelekea tarehe ya kufika mahakamani, ambayo ni
Aprili 12, mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Lwakatare
na Ludovick Joseph wanadaiwa Desemba 28, mwaka 2013, katika eneo la King’ong’o,
Kinondoni, Dar es Salaam, walikula njama za kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru
aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
No comments:
Post a Comment