Thursday, 16 March 2017

VITA DAWA ZA KULEVYA KUONGEZEWA KASI-MAKONDA

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametangaza kuongeza kasi katika vita dhidi ya dawa za kulevya na kwamba katika hilo hataangali sura ya mtu.

Mbali na hilo amesema wamegundua mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watumiaji wa dawa hizo ya kumeza dawa ya meno na kutumia chumvi lengo likiwa kuficha kugundulika na vipimo husika.

Amesema katika vita dhidi ya  dawa za kulevya hakutakuwa na kificho na operesheni hiyo  haifanyiki kwa sababu ya kisasi au kumkomoa mtu.

Makonda alionya kwamba ataendelea kumshughulikia mtu yoyote anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali nafasi yake na uwezo wake.

Aliyasema hayo jana katika hotuba yake ya kutimiza mwaka mmoja tangu kushika wadhifa wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Nimemaliza mwaka mmoja leo (jana) tokea Rais Dk. John Magufuli aniteue kuwa mkuu wa mkoa. Sasa nimekomaa kesho (leo) naanza mwaka wa pili ambapo nitaongeza kasi kubwa ya utendaji wangu. Naongeza spidi mara mbili nikiwa ninazo mbinu za kutosha za kivita,”alisema Makonda.

Akizungumzia vita hivyo, Makonda alisema imekuwa na mafanikio makubwa ambapo kitendo cha kuwatangaza kwa kuwataja moja kwa moja watuhumiwa wanaojihusisha na biashara hiyo kimechangia kwa kiasi kubwa kukamatwa kwa wahusika na watumiaji wengi kujisalimisha.

“Katika vita hii hakuna kificho. Unaitwa unahojiwa na tunakushughulikia. Tuliamua kuwataja hadharani ili hata wale wanaotoa taarifa waamini kwamba taarifa zao tumezifanyia kazi,” alisema Makonda.

Aliongeza kuwa: “Kama tungekuwa tunawaita kimyakimya na kuwahoji kisha wakatoa rushwa tukachukua mimi na Kamishna Sirro (Simon Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam) nani ambaye angeona?” alihoji Makonda.

Makonda alisema katika utendaji wake hakuna wa kumnyamazisha na kwamba kelele zinazoendelea kusikika dhidi yake zinamuongezea ari ya kufanya kazi huku akiamini kwamba kazi anayoifanya inakubalika.

“Unataka Makonda akae kimya? Wewe ni nani wa kuninyamazisha? Umetokea wapi? Kama huwezi kukaa upande wa Mungu tutakupiga tu,” alisema Makonda huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliofurika katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay.

Aliongeza: “Katika vita hii hatuna kisasi na mtu. Tunapamba na watu wanaharibu ndoto na matumaini ya wazazi kwa watoto wao.”

Makonda alisema mpaka sasa wapo vijana  takribani 11,854  wanaohaha kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

“Natoa onyo, kama unajusisha, kuuza, kutumia, kutakatisha fedha zinazotokana na biashara ya  dawaza kulevya au kuficha siri nitakushughulikia na hivi sasa nimekomaa na ninakuja na mbinu mpya,” alisema.

Alisema katika vita hiyo amebaini kwamba baadhi ya watumiaji walikuwa wakitumia mbinu za hali ya juu ili kufanya vipimo visibaini kama wanatumia.

“Baadhi walikuwa wakila dawa ya kusafisha meno Colget na chumvi  ambapo akipimwa mtumiaji vipimo haviwezi kubaini kama anatumia. Kuna mbinu nyingine ya kutumia chimvi ili kuficha vipomo kubaini nayo tumeibaini...sasa nasi tunatumia mbinu nyingine ambayo siisemi,”alifafanua Makonda.

Alisema wale waliokuwa wakikataa kuwa wanatumia dawa hizo walikuwa wakiwaacha rumande hadi wanapata arosto.

“Waliokuwa wanakataa kuwa hawatumii tulikuwa tunawaacha sero baada ya siku tatu tu unamsikia naumwa.. nataka kwenda hospitali, hali inaanza kujitokeza na kumwathiri,”alisema.

Makonda aliongeza kuwa baadhi yao walipokuwa wanaitwa polisi walikuwa hawatokei kutokana na kuogopa kubainika kuwa wanatumia na kabla ya kufika kituoni walikuwa wanakula dawa ya kusafisha meno au chumvi nyingi.

Alisema msako huo ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na wasanii na wamiliki wa maeneo ya starehe na biashara  yaliyokuwa yamekithiri kwa biashara hiyo kuchukua hatua.

AFICHUA SIRI NZITO 

Katika kuonyesha kwamba bado anaendelea kupambana katika vita hiyo, Makonda alisema ana taarifa nzito kuhusu mtanzania ambaye amewekwa bondi Brazil baada ya ndugu zake kudhulumiana  zaidi ya sh. milioni 200.

“Huyu mfanyabiashara yuko Kigamboni na katika kutakatisha fedha hizo alichukua mkopo Benki ya Posta kisha kufungua duka, wakati ndugu yake akiendelea kuteseka Brazil. Tutamshughulikia,”alionya.

Alisema ana taarifa nyingi kuhusu kusambaratika kwa mtandao wa biashara hiyo ambapo baadhi ya wahusika wamekimbia nchi na wanaendelea kuulizana kuhusu hali inavyoendelea.

Makonda alisema  katika kuunga mkono vita hiyo, mfanyabiashara maarufu nchini Azim Dewji ametoa eka tatu kwa ajili ya kujenga kituo kikubwa cha kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya

KAMISHNA SIRRO ALONGA

Kwa upande wake, Kamishna Sirro alisema taarifa za kupanda maradufu kwa bei ya dawa za kulevya  jijini Dar es Salaam kunaashiria kwamba usambazaji wa dawa hizo umepungua baada ya kubanwa.

“Hata hivyo, natoa angalizo kwa viongozi wa dini zote na wazazi. Mmesikia Mkoa wa Pwani viongozi wanauawa, Tanga na Mwanza pia. Tusipo kuwa makini hii hali itatugharimu sana,”alisema Sirro.

Alisema kumekuwa na mazoezi ya judo na karate pamoja na vijana wadogo kupewa mafunzo ya matumizi ya silaha katika nyumba za  ibada.

“Naomba waumini mtunze sana waumini wenu,”alionya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim, alisema kamati inaunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika  mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Alisema msingi wa mapambano hayo ni kukataa maovu ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza, hivyo kuitaka jamii kuunga mkono kwa kukemea na hata kuchukia tu.

Aidha, Alhad Salum alisema kitendo cha Makonda kukaa kimya na kutojibu kelele zinazopigwa kutokana na utendaji wake kunaashiria kukomaa kwake.

“Tungeshangaa sana kama angejibu. Hii inaonyesha jinsi sasa alivyokomaa,”alisema.  

No comments:

Post a Comment