Wednesday 23 November 2016

WAZAZI WA PANYA ROAD KUKAMATWA, MGAMBO WAPIGWA MARUFUKU KWENYE VITUO VYA POLISI


SERIKALI ya mkoa wa Dar es Salaam, imesema itawakamata wazazi wa watoto watakaokamatwa katika matukio ya uhalifu, hususan yanayovihusisha vikundi vya panya road.

Aidha, imewataka wazazi wa kata ya Chamazi, wilayani Temeke, kufuatilia kwa karibu mienendo na tabia za watoto wao, kutokana na eneo hilo kuripotiwa kukithiri kwa matukio ya watoto kufundishwa vitendo vya ugaidi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitoa maagizo hayo jana, wakati akizindua vyumba vinane vya madarasa katika shule ya msingi Mbande, wilayani humo.

Alisema eneo la Mbande ni miongoni mwa maeneo yaliyotajwa kuwepo kwa baadhi ya watoto, ambao wanafundishwa vitendo vya ugaidi huku kukiwa na matukio mengi ya uhalifu.

"Hivi sasa mtoto yeyote  atakayekamatwa katika tukio la uhalifu,  likiwemo kundi linalojiita panya road  au mbwa mwitu, tutamkamata  sambamba  na mzazi wake, kwa sababu ameshindwa kumlea na kumfundisha maadili mema,"alisema Makonda.

Aliongeza: “Haiwezekani mzazi usijue mwenendo wa mwanao. Kama tutambaini mtoto wako amehusika katika matukio ya uhalifu, tutakukamata.”

Makonda alionya kuwa, haiwezekani vijana wadogo wageuke kuwa tishio katika jamii kwa kuwachoma watu visu na kuwapora.

“Wananchi wanashindwa  kufanya shughuli zao kwa hofu ya  panya road. Watu wanachomwa visu na kuibiwa pochi zao na vijana hao wadogo. Hatuwezi kuvumilia katika hili. Nimetoa maelekezo kwa jeshi la polisi kuwakamata wazazi  wote, ambao watoto wao wanajihusisha katika vitendo vya uhalifu,”alisema Makonda.

Alibainisha kwamba,  kila mzazi ana jukumu la kuangalia mwenendo wa tabia ya mtoto wake ili awe na maisha bora ya baadaye.

Makonda aliwausia wanafunzi wa shule hiyo, kuwa wasikivu na kufuata  maelekezo mema ya  wazazi wao, walimu na viongozi wa dini  ili waweze kufaulu.

Katika hatua nyingine, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es  Salaam, imepiga marufuku mgambo kukaa na kufanya kazi kwenye vituo vya polisi na kuwataka kufanya kazi zao ngazi ya serikali za mitaa na kata.

Pia, limewaonya baadhi ya mgambo wasio waaminifu na wanaokwenda kinyume cha sheria na utaratibu, kwa kunyanyasa wananchi kwa kuomba rushwa kwa kuvitumia vituo hivyo.

Mkuu wa Operesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Lucas Mkondya, aliyasema hayo jana, wakati wananchi wa kata ya Yombo, mtaa wa Machimbo, wilayani Temeke, kutoa changamoto, ikiwemo ya kunyanyaswa na polisi.

Wananchi hao walilalamikia kushamiri kwa vitendo vya uhalifu kiasi cha kuwafanya waishi kwa hofu, ikiwa ni pamoja na kufunga biashara zao mapema.

Walisema katika eneo hilo, kumekuwa na milio ya bunduki, ambapo wamekuwa wakiona ni kitu cha kawaida, huku vitendo vya ujambazi, uvamizi wa vikundi vinavyojiita panya road na mbwa mwitu vikiwakosesha usingizi.

Walisema wamekuwa wakikosa huduma stahiki katika Kituo cha Polisi cha Sigala, kilichoko katika eneo hilo huku wakiwatuhumu baadhi ya polisi kuomba rushwa.

“Tunanyanyasika na watu wasio na silaha kwa nini? Mbona tunanyanyasika hivi?” Alihoji Josephat  Charles, mkazi wa eneo hilo huku akilalamikia kamata kamata ya polisi katika eneo la TANESCO lililoko katika kata yao.

Akijibu changamoto hizo, Mkondya aliwataka wananchi kuwataja bila woga polisi wanaojihusisha na vitendo viovu.

Hata hivyo, Mkondya alisema hali hiyo pia inachangiwa na muingiliano wa mgambo na  askari jamii, ambao hutumia vituo vya polisi.

Alisema baadhi ya  mgambo na askari jamii, siyo waaminifu na hujifanya polisi kwa kuwa hutumia vituo vya polisi kufanya shughuli zao.

“Ndiyo maana raia wakifika katika vituo vyetu vya polisi na kuhudumiwa na mgambo au askari jamii kisha kuombwa rushwa au kunyanyaswa, shutuma zote zinakwenda kwa jeshi la polisi

“Hivyo kuanzia sasa ni marufuku kwa mgambo wala ulinzi shirikishi kufanya kazi zao katika vituo vya polisi. Wafanye kazi zao katika ofisi zao za serikali za mitaa au kata,”alisema.

Alisema mgambo wanatakiwa kukamata watuhumiwa kisha kuwafikisha na kuwakabidhi katika vituo vya polisi, kisha wao kurejea ofisi za serikali za mitaa au kata.

“Hawa ndiyo wanalipaka matope jeshi la polisi, lakini nilishatoa maelekezo mgambo watumike serikali za mitaa, hatutaki kuwatumia katika vituo vya polisi, nimekuwa nikizunguka usiku nawakuta askari mgambo wananipokea kituoni,”alisema.

Aidha, Mkondya alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto, kuendesha gwaride kwa askari wa kituo cha polisi Urafiki, kutokana na madai ya kuomba rushwa ya sh. 50,000 kwa mkazi wa eneo hilo, Yusta Makini, ambaye alidaiwa mtoto wake kukamatwa katika eneo la TANESCO, alipokuwa akienda dukani kununua vocha na kutakiwa kutoa kiasi hicho ili aweze kuachiwa huru.

“Nakuagiza RPC, ufanye gwaride la askari wote wa kituo cha Sigala ili kumtambua askari aliyechukua fedha hizo, achukuliwe hatua,”alisema.

Awali, Kamanda Muroto, aliwaomba radhi wananchi hao kutokana na changamoto zinazojitokeza za ulinzi katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Simon Ngonyani, juzi, aliingia matatani baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kumkabidhi kwa Polisi Temeke ili aeleze jinsi mwananchi alivyouawa katika eneo lake.

Kizaazaa hicho kilimkumba mwenyekiti huyo wa mtaa, baada ya kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha mbele ya Makonda, aliyemtaka kujibu malalamiko ya wananchi, waliyoyaeleza katika mkutano wa hadhara kwamba, katika siku za hivi karibuni, aliuawa kijana katika mtaa huo na hakuna hatua zilizochukuliwa.

"Mkuu wa mkoa wakati napigiwa simu kujulishwa hiyo taarifa, simu yangu ilikuwa imezimwa na ipo kwenye chaji,"alisema, lakini kabla ya kuendelea, Makonda alimkatiza.

"Hatutaki kusikia hadithi za simu, tunataka utueleze unafahamu nini kuhusu kuuawa kwa mwananchi huyo katika eneo lako au hufahamu,"alisema na kuongeza:

"Sijaridhika na maelezo ya huyu mtu, kamanda mchukue ukamhoji ili ufahamike undani wa kifo cha mwanachi, hatutaki watumishi ambao hawana ushirikiano." 

No comments:

Post a Comment