Thursday 24 November 2016

CCM YAKUNJUA MAKUCHA, WANACHAMA 380 WAVULIWA UANACHAMA, YAWAONYA WATAKAOANZA KAMPENI MAPEMA UCHAGUZI WA 2017


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekunjua makucha kwa kuwachukulia hatua kali za kinidhamu kwa viongozi na wanachama wake 600, waliobainika kukiuka maadili ya uongozi, ikiwemo kukisaliti Chama katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita.

Wanachama hao ni kutoka katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, ambayo imeshawasilisha ripoti zake makao makuu ya CCM, kuhusu hatua iliyochukua dhidi ya wanachama waliokisaliti wakati wa uchaguzi huo.

Katika orodha hiyo, wapo wanachama waliopewa onyo kali, waliosimamishwa uongozi na wengine kuvuliwa uanachama. Pia wapo wanaosubiri maamuzi ya vikao vya juu kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Mikoa, ambayo imeshachukua hatua hizo dhidi ya wanachama hao, idadi ikiwa kwenye mabano ni Kigoma (54), Lindi (152), Mwanza (120), Shinyanga (40), Singida (7), Manyara (41), Iringa (1), Morogoro (1), Mara (109) na Ruvuma (75).

Waliovuliwa uanachama katika mkoa wa Kigoma ni 34, Lindi 44, Mwanza 93, Shinyanga 32, Manyara watano, Mara 109, Ruvuma 61 na Singida wawili.

Hayo yalielezwa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, alipozungumza na waandishi wa habari, nyumbani kwake, Oysterbay, Dar es Salaam.

Mangula alisema kuchukuliwa hatua kwa wanachama hao ni utekelezaji wa agizo la mkutano mkuu wa CCM wa mwaka 2012, ambao uliagiza wanachama wanaokiuka maadili ya uongozi wachukuliwe hatua.

"Tayari vikao husika katika baadhi ya mikoa vimeshaanza kuchukua hatua, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mkutano mkuu wa CCM," alisema.

Hata hivyo, Mangula alisema hajaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na mikoa ya Morogoro na Iringa, ambayo kila mmoja umemvua uongozi mwanachama mmoja kwa kosa hilo.

"Haiwezekani mahali tulikopoteza majimbo na kuwepo mgawanyiko mkubwa ndani ya Chama, apatikane mtu mmoja, lazima tufuatilie ili kujua kuna nini?" alihoji Mangula.

Alisema wanatarajia kutuma ujumbe maalumu katika mikoa hiyo miwili ili kufuatia suala hilo kwa lengo la kubaini nini kimetokea na kupata ukweli kabla ya kuchukua hatua.

Hata hivyo, alisema kazi ya kupokea taarifa za hatua mbalimbali katika mikoa mingine, ikiwemo visiwani Zanzibar, inaendelea na pindi zitakapowasilishwa atatoa taarifa.

Mangula pia aliwaonya wana-CCM wanaotarajia kuomba kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Chama wa mwakani, kufanya vitendo kinyume na taratibu, kwani nyendo za kila mmoja zitafuatiliwa na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao.

"Wapo ambao wameanza mikakati ya kujipanga na kuwapitisha watu ili kutengeneza mtandao kwa ajili ya uchaguzi wa 2020," alisema Mangula na kuonya kwamba, Chama hakitafanya makosa na wataondolewa kwa kuzingatia kanuni zinazosimamia masuala hayo.

Makamu Mwenyekiti alisema kila mwanachama anayo haki ya kutangaza nia ya kugombea uongozi, lakini haruhusiwi kuanza kampeni kabla ya uteuzi wa wagombea katika ngazi husika.

Aidha, Mangula alisema mwanachama atakayethibitika ametoa rushwa, jina lake litaachwa na yule atakayeshinda, lakini ikathibitika ametoa rushwa, atanyang'anywa nafasi yake na hatua kali zaidi dhidi yake zitachukuliwa.

"Wanaoanza kampeni mapema kwa maslahi binafsi, wanahangaika bure. Wapo waliopanga kuweka wenyeviti wa wilaya, mikoa hao wote tunao, tukipata taarifa tutawashughulikia,"alisema.

Makamu Mwenyekiti pia alionya kuwa ni mwiko kwa mwanachana yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya Chama na kwamba, atakayebainika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.

Pia, aliwaonya wapiga kura kuepuka kupokea posho au msaada wa usafiri kutoka kwa wagombea na kuongeza kuwa, watakaopatikana na hatia hiyo nao watashughulikiwa.

"Ni marufuku kwa mgombea kutumia ukabila, dini au ubaguzi wa aina yoyote, kuvuruga umoja na mshikamano kama njia ya kutafuta ushindi,"alionya Mangula.

"Ni kosa kubwa kukisaliti chama au kukikosesha ushindi. Atakayekivuruga na kushirikiana na upinzani kukihujumu, adhabu yake ni kufukuzwa. Kanuni ndizo zitakazotumika kuwachukulia hatua,"alisisitiza.

Kuhusu tathmini ya utekelezaji ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kipindi cha mwaka mmoja, Mangula alisema anaamini kwa kasi ya Rais Dk. John Magufuli katika usimamizi wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ndani ya miaka minne ijayo inawezekana.

"Kumekuwa na mafanikio makubwa na wananchi wanaona matunda ya kazi iliyofanywa na Dk.Magufuli na usimamizi wa Chama ni muhimu na ni wa lazima, hivyo uhakika wa 'perfomance' hii ya ahadi tulizozitoa itakapokamilika, hakutakuwa na sababu ya watu kuhoji kwa nini muendelee nyinyi,"alisema.

Kuhusu wimbi la viongozi na wanachama kutoka kambi ya upinzani wanaohamia CCM, alisema kwa maelezo wanayotoa, wanaona Rais Magufuli anatenda yale waliyokuwa wanayapigia kelele kwa hiyo haoni sababu ya wao kuendelea kupinga.

Hata hivyo, alisema ni lazima kuwa waangalifu na CCM haipokei kila anayekuja kwani kuna wengine wanakuja kuangalia ili watuchunguze na ikifika wakati wa uchaguzi wanaondoka au wameingizwa ili wachunguze, hivyo si kila anayekuja ana nia nzuri licha ya kujitangaza kwamba wana nia nzuri.

LOWASSA NA WENZAKE SI TISHIO

Akifafanua iwapo makada walioihama CCM na kuingia upinzani wakati wa uchaguzi ni tishio katika uchaguzi mkuu ujao, alisema: "Wala si tishio, sisi Chama ni wingi wetu, umoja wetu na kinachotuunganisha ni haya, utaratibu tuliojiwekea na 'perfomance' yetu. Kama kuyumba ilikuwa mwaka jana, maana 'walituambush', baada ya hapo hawana nafasi tena...ilikuwa ni kama vita, sasa hivi tumejiandaa."

Katika uchaguzi mkuu uliopita, waziri mkuu aliyejizulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, ajiondoa CCM, baada ya kuenguliwa kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha urais na kuhamia CHADEMA kugombea kiti hicho bila mafanikio.

TATHMINI YA MALI ZA CHAMA

Akizungumzia tathmini ya mali za Chama, Mangula alisema ripoti yake imeshakamilika na kwamba, imeshajadiliwa kwenye sekretarieti na sasa inatarajiwa kupelekwa kwenye vikao vya Kamati Kuu ya CCM.

Hata hivyo, Mangula alikiri kwamba baada ya kuipitia taarifa hiyo, kuna kikosi kitatumwa ili kuthibitisha kile kilichoandikwa na uhalisia katika maeneo husika.

Alisema kwa muda mrefu Chama hakikufanya vizuri kwenye usimamizi na hivyo kusababisha uharibifu na ubadhilifu, ambapo kuna baadhi ya viongozi walifikia hatua ya kuzifanya mali zao.

“Tuna viwanja vingi kwenye maeneo muhimu, ambavyo vikisimamiwa, tunaweza kufanya uwekezaji mkubwa utakaokiingizia Chama mapato.
Tuna viwanja vya michezo kama CCM Kirumba, Mwanza,”alisema.

AMPONGEZA MAKONDA NA MTOPA

Mangula pia alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi, Ali Mtopa kwa ziara anazofanya kwa lengo la kukiimarisha Chama na kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Mbali na Mtopa, alimtaja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwa ni mfano mzuri wa viongozi, kutokana na ziara anazofanya mkoani mwake kwa lengo la kubaini kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Alisema katika ziara hizo, Makonda amekuwa akiongozana na viongozi na wataalamu, ambao huwatumia kujibu kero zinazotolewa na wananchi katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment