Friday 25 November 2016

MWINYI: MAGUFULI NI KIBOKO


RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika jana, Rais mstaafu Mwinyi alisema lengo la kukutana na Rais Dk. Magufuli na kufanya naye mazungumzo kwa mara ya kwanza, ni kumpongeza kwa kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani na pia kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake.

Mzee Mwinyi aliyataja maeneo, ambayo Rais Dk. Magufuli ameyafanya kwa mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa, ambapo amebainisha kuwa, hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha mwaka mmoja, zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo ikilinganishwa na wakati uliopita.

"Rushwa ilikuwepo tangu enzi ya hayati Mwalimu Nyerere, aliipondaponda kabisa, lakini hakuimaliza na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta sunami, nafurahi sana,"alisema Mwinyi.

Alilitaja eneo lingine kuwa ni kuimarisha utendaji kazi serikalini, ambapo alisema hatua zilizochukuliwa na serikali ya Rais Dk. Magufuli zimeongeza kasi na ametoa wito kwa viongozi na wananchi kuunga mkono juhudi hizo.

"Tuliobaki tumsaidie kwa kumuombea dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale watu wanapopotosha, tuseme sio hivyo, ilivyo ni kadhaa kadhaa, tusiwaache watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyoifanya mwenzetu ni nzuri, nzuri, nzuri ya ajabu," alisisitiza Rais mstaafu Mwinyi.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment