Tuesday 22 November 2016

LEMA AKWAA KISIKI MAHAKAMA KUU


JINAMIZI la  kukosa dhamana limeendelea kumkalia kooni mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha,  kutupilia mbali maombi yake.

Dhamana ya Lema ilizuiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Novemba 11, mwaka huu, mbele ya Hakimu Desdery Kamugisha, hali iliyofanya  jopo la mawakili wake, wakiongozwa na Peter Kibatala kuandika barua kuiomba mahakama  kuu kufanya marejeo ya wa uamuzi wa mahakama hiyo.

Akisoma uamuzi jana,  Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Sekela Moshi,  alisema mahakama hiyo imepitia hoja zilizowasilishwa na mawakili wa upande wa jamhuri na utetezi.

Alisema baada ya kupitia hoja hizo, mahakama hiyo imeyakataa maombi ya kufanya marejeo ya uamuzi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi juu ya dhamana ya Lema.

“Nimekataa ombi la upande wa utetezi la kufanya  marejeo ya uamuzi ya mahakama ya hakimu mkazi kwa kuwa hayana  mashiko kisheria kwa kukosa hoja za kisheria,"  alisema.

Jaji Sekela alisema hoja za mapingamizi ya awali zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali,  Paul  Kadushi,  kabla ya kusikiliza maombi ya utetezi zilikuwa na mashiko kwa kuwa zinalenga katika vifungu vya mwenendo mzima wa dhamana.

“Ni kweli kama alivyosema awali Kadushi,  sheria namba tano (e) ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) kifungu cha 148-160 vinaeleza utaratibu mzima wa kukata rufani na vipengele hivi havikuzingatiwa na upande wa utetezi katika maombi yao, hivyo hakimu mkazi alikuwa sahihi.”

“Nimetilia maanani hoja mbili za kisheria zilizowasilishwa na jamhuri kuwa maombi ya utetezi yalikiuka matakwa ya kisheria kwa kuwa katika barua ya maombi hakuna sehemu yoyote inayoonyesha kuwa upande wa utetezi unataka kukata rufani,”alisema.

Alisema sheria  hiyo iko wazi na inautaka upande wa utetezi kama haujaridhika na uamuzi wa hakimu, basi ukate rufani, lakini siyo kupeleka maombi ya barua mahakama kuu kama walivyofanya.

“Sheria inataka upande usioridhika ukate rufaa au kutoa sababu za kuishawishi mahakamakuu kufanya marejeo ya majalada namba 440 na 441 lakini katika maombi yao hakukuwa na sababu yoyote ile,” alisema.

Kuhusu kifungu cha (43)(2) cha sheria ya mahakimu sura ya 11, kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba 25 ya  mwaka 2002 ambayo ilitolewa na Kadushi, pia haikubishaniwa na upande wa utetezi na hakuna mahali popote sheria hiyo imetajwa na upande wa utetezi, hivyo ni kweli hoja hii  ya maombi haina mashiko.

Jaji alisema  mahakama imemaliza kazi yake na kuutaka upande wa utetezi kufuata utaribu wa kisheria kama haujaridhika na uamuzi huo.

Awali, Lema alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha Novemba 8, mwaka huu, mbele ya  hakimu mkazi Kamugisha akituhumiwa kwa  kesi mbili za uchochezi namba 440 na 441.


Wakati huo huo baada ya mahakama kumaliza shughuli zake, mwandishi wa habari hii alishuhudia jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Wakili Peter Kibatala, likihaha  kukata rufani chini ya hati ya dharura.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kibatala alisema wana nyaraka zote, hivyo wanakata rufaa chini ya hati ya dharura juu ya pingamizi la dhamana ya Lema liliotolewa na upande wa jamhuri.

Mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni jopo hilo la mawakili wa utetezi lilikuwa linahangaika mahakamani hapo kushughulikia rufani  hiyo ambayo bado ilikuwa haijafanikiwa.

Katika hatua nyingine, Uhuru ilishuhudia kuimarishwa kwa ulinzi katika mahakama hiyo kuanzia mapema asubuhi kabla ya mbunge huyo kupelekwa mahakamani.

Aidha askari wa Kikosi Cha Kutuliza Ghasia (FFU) na askari magreza walikuwa wamejaa mahakamani hapo wakiwa na silaha za moto, wakifanya doria katika eneo lote la mahakama hiyo.

Pia magari yote yaliyokuwa yakiingia katika viunga vya mahakama hiyo yalikuwa yakikaguliwa na wananchi nao walikuwa wakikaguliwa.

Baada  kesi kumalizika saa 5.03 asubuhi, wafuasi wa CHADEMA waliokuwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza hatima ya dhamana ya mbunge huyo, akiwepo mbunge wa Monduli Julius Kalanga, Dk. Dodwin Mollel (Siha) na wabunge wa viti maalumu mkoa wa Arusha, Cecilia Pareso na Joyce Mukya, walipigwa na butwaa bila ya kujua cha kufanya baada ya Lema kukosa dhamana.

Ilipotimu saa 5.48 asubuhi, Lema aliondolewa mahakamani hapo  na kurudishwa rumande  katika gereza la Kisongo kwa kutumia gari aina ya Land Rover, lenye namba za usajili Mt 0071 ambalo lilisindikizwa na chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kikosi Cha Kutuliza Ghasia.

No comments:

Post a Comment