Thursday 25 May 2017

SMZ YAINGIA MKATABA NA BAKHRESA KUJENGA MJI WA KISASA FUMBA


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetiliana saini mkataba na Kampuni za Bakhresa, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mji wa kisasa, maarufu kama 'Sertilite City', utakaojengwa Fumba, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Chini ya mkataba huo, kampuni za Bakhresa, zitajenga mji wa kisasa, utakaobadili haiba ya nchi, ambapo kukamilika kwake kutaiwezesha Zanzibar kuwa na majengo makubwa yenye ghorofa zaidi ya 30 na hoteli zenye hadhi zaidi ya nyota tano.

Waliotia saini mkataba wa ujenzi wa mji huo ni  Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa kampuni hizo, Said Salim Bakhresa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa ZIPA, Nassor alisema jumla ya hekta 3,000, zimetolewa na serikali ili kufanikisha mradi huo, ambao tayari majengo kadhaa yameanza kujengwa.

Aliongeza kuwa, katika mji huo, kutakuwa na nyumba za kibiashara za kuishi watu, zenye ukubwa tofauti, kulingana na mitaa, ambapo mitaa mingine zitafikia ukubwa wa zaidi ya ghorofa 30.

"Kutakuwa na majengo tofauti kulingana na maeneo, kutakuwa na 'Private Villa' na katika mitaa mikubwa, kutakuwa na ghorofa zaidi ya 30," alifafanua Salum.

Aliongeza kuwa, pia kutakuwa na kiwanja cha kimatifa cha mpira wa miguu na viwanja vidogo, kituo cha kibiashara, ukumbi wa kimataifa wa mikutano na bandari ndogo, itakayounganisha Dar es Salaam na Pemba.

"Kwa kweli utakuwa ni mji wa kivutio wa aina yake kwa wenyeji na wageni mbalimbali, ambao bila shaka watakuwa na shauku ya kutembelea na kupata huduma mbalimbali," alisema Mkurugenzi huyo wa ZIPA.

Kwa upande wake, Bakhresa alisema tayari wametenga Dola milioni 500, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mji huo katika hatua za awali, huku gharama ikitarajiwa kuongezeka kulingana na mahitaji ya baadae.

Aidha, alieleza kuwa, manufaa yatakayopatikana ni pamoja na nafasi za ajira 3,000 za moja kwa moja kwa wananchi, jambo ambalo pia litabadili hali zao za kimaisha.

Awali, Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohammed, aliwahakikishia ushirikiano wa kila aina wawekezaji hao wazalendo na kuwaomba waendelee kuiunga mkono serikali katika azma yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema Sheria Namba 11 ya Mwaka 2004, inatoa nafasi kwa serikali kuwalinda wawekezaji, hasa wazawa, hivyo kuwaomba wawekezaji wengine kuitumia fursa hiyo ili kuendelea kuwekeza zaidi Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), imeweka mazingira salama ya kiuwekezaji, hasa katika maeneo huru yaliyotengwa, ili wawekezaji wazawa na wageni, waendelee kuwekeza katika maeneo hayo kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Mradi huo wa ujenzi wa mji wa kisasa, utakuwa miongoni mwa miradi mikubwa iliyowekezwa Zanzibar na Bakhresa, ambayo itaendelea kuisaidia Serikali ya Zanzibar kukuza kipato cha wananchi wake na pato la taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment