Thursday 25 May 2017

UCHUNGUZI WA KAMATI WABAINI DHAHABU YA MATRILIONI IMEIBWA NCHINI






KAMATI Maalumu ya Uchunguzi wa Mchanga wa Madini (makinikia), imebaini udanganyifu mkubwa kwenye mchanga huo, ambao umeligharimu taifa mabilioni ya fedha.

Machi 29, mwaka huu, Rais, Dk. John Magufuli, aliteua kamati maalumu yenye wajumbe wanane, kwa ajili ya kuchunguza aina na viwango vya madini vilivyomo kwenye mchanga wa madini, uliomo ndani ya makontena yaliyozuiliwa na serikali.

Akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa kamati hiyo Ikulu, mjini Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Mruma, alisema chimbuko la kufanyika kwa uchunguzi huo, linatokana na ukweli kuwa, viwango vya madini yaliyomo kwenye makinikia, havijulikani na mikataba yake haipo wazi.

“Hali hii inaleta hisia kuwa, nchi inaibiwa na hainufaiki vya kutosha na uchimbaji wa madini hapa nchini, hususani kwenye biashara ya makinikia,” alisema.

Profesa Mruma alisema katika uchunguzi huo, kamati ilibaini kuwepo kwa viwango vingi vya juu vya dhahabu ndani ya makinikia, uliofanyiwa uchunguzi.

Alisema viwango hivyo ni kati ya gramu 671 hadi 2,375, kwa tani, sawa na gramu 1,400 kwa tani.

“Wastani huu ni sawa na kilo 28, kwenye kontena moja lenye wastani wa tani 20 za makinikia,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwenye makontena 277, yaliyozuiwa bandarini, yatakuwa na wastani wa tani 7.8 za dhahabu, zenye thamani ya sh. bilioni 676.

“Aidha, kwa kutumia viwango vya juu, ambavyo ilikuwa gramu 2,375 kwa tani, kontena moja lenye tani 20 za makinikia, ni sawa na kilo 47.5 za dhahabu,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema katika makontena 277, yaliyozuiwa, kutakuwa na kilo 13,157.5, ambazo thamani yake ni sh. trilioni 1.4.

“Hivyo, thamani ya dhahabu katika makontena hayo 277, ni kati shilingi bilioni 676 na shilingi trilioni 1.439,” alisema.

Aidha, alisema taarifa walizozipata kutoka kwa wakala na wazalishaji, zinaonyesha kuwa, makinikia yana wastani wa gramu 200, kwa tani, kiwango ambacho ni sawa na kilo nne za dhahabu katika kila kontena.

“Hivyo, makontena 277 ya makinikia yatakuwa na tani 1.2 za dhahabu.
Kiasi hiki kina thamani ya sh. bilioni 97.5. Thamani hii ni ndogo, ikilinganishwa na thamani halisi iliyopatikana katika uchunguzi. Kati ya shilingi bilioni 676 na shilingi trilioni 1.439, kwa tofauti hii inaonyesha kuwa kuna upotevu mkubwa wa mapato ya serikali,” alisema.

Pamoja na viwango vikubwa vya dhahabu kwenye makinikia, alisema kamati ilipima na kupata viwango vikubwa katika madini ya shaba, ambapo kiwango cha chini kilikuwa gramu 15.09 kwa tani hadi gramu 33.78 kwa tani, sawa na wastani wa asilimia 26.

Kwa upande wa shaba, alisema kiwango kilichopatika ni tani 5.2 na kiwango cha juu kilichopimwa ni tani 6.75 kwenye kila kontena lenye tani 20 za makinikia.

“Hivyo, kiasi cha wastani wa shaba kwenye makontena 277, ni tani 1,440.4, ambazo thamani yake ni shilingi bilioni 17.9  na kiasi cha juu ni tani 1,871.4, ambazo zina thamani ya shilingi bilioni 23.3. Hivyo, thamani ya shaba katika makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini ni kati ya shilingi bilioni 17.9 na bilioni 23.3,” alisema.

Alisema nyaraka za usafirishaji, ambazo kamati ilizipata kutoka bandarini, zinaonyesha kuwa makinikia yana wastani wa kiwango cha shaba cha asilimia 20.

“Kiwango hiki ni sawa na tani nne za shaba kwenye kila kontena, hivyo makontena 277, yaliyozuiwa bandarini yatakuwa na tani 1,108 za shaba. Kiasi hiki cha shaba kina thamani ya sh. bilioni 13.6,” alisema Profesa Mruma.

Vilevile, alisema wastani wa kiwango cha madini ya fedha kilichopimwa ni kilo 6.1 na kiwango cha juu ni kilo saba kwa kontena lenye tani 20 za makinikia.

Hivyo, alisema kiasi cha wastani wa fedha kwenye makontena 277 ni kilo 1,689, sawa na tani  1.7, ambazo thamani yake ni sh. bilioni  2.1.

Alisema kiasi cha juu ni kilo 1,939, sawa na tani 1.9, ambazo thamani yake ni sh. bilioni 2.4.

“Hivyo, thamani ya fedha katika makontena 277 yaliyozuiwa bandarini ni kati ya sh. bilioni 2.1 na bilioni 2.4,” alisema.

Profesa Mruma aliongeza: “Nyaraka za usafirishaji, ambazo kamati ilizipata kutoka bandarini, zinaonyesha kuwa makinikia yana madini ya fedha kwa takriban kilo 150. Kiwango hiki kinamaanisha kuwa, kuna kilo tatu za fedha kwenye kila kontena la tani 20 za makinikia."

"Kwenye makontena 277, yaliyozuiwa bandarini, kiasi cha madini ya fedha kilichopo kwenye nyaraka za usafirishaji ni kilo 831. Kiasi hiki cha fedha kina thamani ya sh. bilioni 1.0. Kwa takwimu hizi, kwa upande wa fedha nako kuna upotevu mkubwa wa mapato ya taifa,” alifafanua.

Kuhusu salpha, alisema wastani uliopimwa ni tani 7.8, wakati kiwango cha juu kilikuwa tani 10.2 kwa kontena lenye tani 20 za makinikia.

“Hivyo, makontena 277 yaliyozuiwa bandarini, yatakuwa na wastani wa tani 2,161 za salpha, ambazo thamani yake ni shilingi bilioni 1.4  na kiasi cha juu ni tani 2,825.4, ambazo zina thamani ya shilingi bilioni 1.9,” alisema.

Alisema thamani ya salpha katika makontena 277, yaliyozuiwa bandarini ni kati ya sh. bilioni 1.4 na bilioni 4.9.

Kuhusu madini ya chuma, Profesa Mruma alisema wastani uliopimwa ni tani 5.4, wakati kiwango cha juu kilikuwa tani 6.1, kwa kontena lenye tani 20 za makinikia.

Hivyo, alisema makontena 277 yaliyozuiwa bandarini yatakuwa na wastani wa tani 1,496 za chuma, ambazo thamani yake ni sh. bilioni 2.3 na kiasi cha juu ni tani 1,695, ambazo zina thamani ya sh. bilioni 2.6.

“Hivyo, thamani ya chuma katika makontena 277, yaliyozuiwa bandarini ni kati ya sh. bilioni 2.3 na bilioni 2.6. Kama ilivyo kwa salpha, thamani hii ya chuma ni kubwa ukizingatia kuwa, haijawahi kutumika kukokotoa mrabaha katika mauzo ya makinikia,” alisema.

Pia, alisema uchunguzi ulionyesha kuwepo kwa madini mkakati, ambayo kwa sasa yanahitajika sana duniani na yana thamani kubwa, sambamba na thamani ya dhahabu. Aliyataja madini hayo kuwa ni iridium, rhodium, ytterbium, beryllium, tantalum na lithium.

Profesa Mruma alisema wastani wa iridium uliopimwa ni kilo 6.4, wakati kiwango cha juu ni kilo 13.75, kwa kontena lenye tani 20 za makinikia.

“Hivyo, makontena 277 yaliyozuiwa bandarini yatakuwa na wastani wa kilo 1,773  za iridium, ambazo thamani yake ni sh. bilioni 108, wakati kiasi cha juu ni kilo 3,808.8, ambazo thamani yake ni sh. bilioni 231,”alisema.

Kwa upande wa rhodium, alisema wastani uliopimwa ni kilo 0.034, wakati kiwango cha juu ni kilo 0.078, kwa kontena lenye tani 20 za makinikia.

Hivyo, alisema makontena 277 yaliyozuiwa bandarini yatakuwa na wastani wa kilo 9.4 za rhodium, ambazo thamani yake ni sh. bilioni 0.7, wakati kiasi cha juu ni kilo 21.6 ambazo ni sh. bilioni 1.5.

Vilevile, alisema ytterbium ilipatikana kwa wastani wa kilo 3.7 na kiwango cha juu kilikuwa kilo 4.9, kwa kila kontena lenye tani 20 za makinikia.

Alisema makontena 277 yaliyozuiwa bandarini yatakuwa na wastani wa kilo 1024.9 za ytterbium, ambayo thamani yake ni sh. bilioni 12.4, wakati kiasi cha juu ni kilo 1,357.3,  ambazo sh. bilioni 16.4.

Kuhusu beryllium, Profesa Mruma alisema wastani wa kiasi kilichopimwa ni kilo 19.4 na kiasi cha juu kilikuwa kilo 26.9, kwa kila kontena lenye tani 20 za makinikia.

“Hivyo, wastani wa beryllium kwenye makontena 277 ni tani 5.4 zenye thamani ya sh. bilioni 6.0 na kiwango cha juu kilichopimwa katika makontena 277 ni tani 7.5, ambazo thamani yake ni sh. bilioni 8.3,” alisema.

Akifafanua kuhusu madini ya tangalum, Profesa Mruma, alisema ilipatikana ikiwa na wastani wa kilo 11.7 na kiwango cha juu kilikuwa kilo 17.3, kwa kila kontena lenye tani 20 za makinikia.

“Hivyo, makontena 277 yaliyozuiwa bandarini yatakuwa na wastani wa kilo 3240.9 za tantalum, ambazo thamani yake ni sh. bilioni 1.9, wakati kiasi cha juu ni kilo 4,792, ambazo thamani yake ni shilingi bilioni 2.8,” alisema Profesa Mruma.

Alisema wastani wa kiasi cha madini ya lithium kilichopimwa ni kilo 21.5 na kiasi cha juu kilikuwa kilo 29.8, kwa kila kontena lenye tani 20 za makinikia.

Hivyo, alisema wastani wa lithium kwenye makontena 277 ni  kilo 5,955.5 zenye thamani ya sh. bilioni 1 na kiwango cha juu kilichopimwa katika makontena 277 ni kilo 8,254.6, ambazo ni sh. bilioni 1.4.

Alisema kiwango cha fedha kilichopatikana katika makinikia hayo kilikuwa kati ya gramu 202.7 hadi 351 kwa tani, wastani ukiwa ni gramu 305.

MAPENDEKEZO YA KAMATI

Kutokana na hali hiyo, Profesa Mruma alisema kamati iliishauri serikali kuendelea kusitisha usafirishaji mchanga wa madini ‘makinikia’ nje ya nchi mpaka mrabaha stahiki utakapolipwa serikalini kwa kuzingatia thamani halisi ya makinikia kama ilivyoainishwa kwenye uchunguzi huu.

Pia, kamati iliishauri serikali ihakikishe kuwa ujenzi wa smelters nchini unafanyika haraka ili makinikia yote yachenjuliwe hapa hapa nchini. Hii itawezesha madini yote yaliyomo kwenye makinikia kufahamika na kutozwa mrabaha halisi.

Vilevile, alisema TMAA inatakiwa kufunga tepe za udhibiti kwenye makontena mara tu baada ya kuchukua sampuli ili kudhibiti udanganyifu unaoweza kutokea baada ya uchukuzi wa sampuli.

Alisema kutokana na uwepo wa madini mbalimbali yenye viwango tofauti kwenye mbale, TMAA ipime viwango vya dhahabu na metali nyingine muhimu katika mbale zote zinazosafirishwa nje ya nchi, bila kujali kilichoonyeshwa kwenye andiko la msafirishaji wa mbale husika.

Aidha, alishauri kuwa Wizara ya Nishati na Madini, ibainishe tabia za mbale (aina za madini na viwango vyake), zilizomo kwenye vyanzo mbalimbali nchini.

Profesa Mruma alisema kamati imependekeza serikali ijumuishe metali zote zenye thamani katika kukokotoa mrabaha wa makinikia na mbale za madini mbalimbali.

Vilevile, serikali iwachukulie hatua watendaji wa TMAA na wizara, kutokana na kutosimamia vyema tathmini ya viwango halisi vya madini/metali mbalimbali, vilivyopo katika makinikia na mbale za madini mengine, viwango ambavyo hutumika katika kukokotoa mrabaha.

Pia, alisema serikali ifanye uchunguzi wa kushtukiza kwa kadri itakavyowezekana katika udhibiti wa uzalishaji na usafirishaji wa madini nje ya nchi ili kujiridhisha kuwa, taratibu zilizowekwa kisheria zinatumika ipasavyo.

Aidha, ilishauri uchunguzi zaidi ufanywe na wataalamu wa mionzi kwenye scanner zinazotumika bandarini ili kubaini aina au mfumo sahihi wa scanner, unaofaa katika kuchunguza mizigo yenye tabia (properties) kama za makinikia na mbale za madini

Profesa Mruma alisema katika kutekeleza uchunguzi huo, kamati iliongozwa na hadidu za rejea, ambazo ziliwekwa na serikali.

“Tulitembelea maeneo yote yenye makontena yenye shehena ili kuyachunguza pamoja na kuchukua sampuli. Maeneo hayo yalibainika katika bandari ya Dar es Salaam na bandari kavu. Kulikuwa na makontena 277, lakini makontena mengine yalikuwa katika migodi ya Bulyankulu na Buzwagi,” alisema.

Profesa Mruma alisema walifanya uchunguzi wa kimaabara na kubaini aina, viwango, kiasi na madini yaliomo kwenye makinikia.

No comments:

Post a Comment