Thursday 25 May 2017

NANI KUMRITHI PROFESA MUHONGO? NI BAADA YA RAIS MAGUFULI KUTENGUA UTEUZI WAKE


KITENDAWILI cha nani kumrithi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kimetanda kila kona baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wake.

Ilikuwa takribani muda wa saa tano kupita baada ya awali, Rais Dk. Magufuli kumtaka waziri huyo kujitathmini na kuchukua hatua, baada ya kugundulika madudu na upotevu wa mabilioni ya fedha katika ripoti ya kamati maalumu ya uchunguzi iliyoundwa kuchunguza mchanga wa madini (Makinikia).

Vilevile, ameivunja Bodi ya Wakala wa Madini Tanzania (TMAA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala huo, Dominick Rukaza huku akiviagiza vyombo vya dola kumchunguza Kamishna Mkuu wa Madini aliyepita na wafanyakazi wa TMAA, ambao waliohusika kwenye sakata hilo.

Sakata hilo lilitokea jana, Ikulu, mjini Dar es Salaam, baada ya Rais Dk. Magufuli, kupokea ripoti ya kamati maalumu aliyoiunda kwa ajili ya kuchunguza makontena 277, yaliyokuwa yakisafirisha mchanga kwenda nje ya nchi kwa ajili ya  kuyeyushwa, ili kupata kiwango cha madini aina ya dhahabu au shaba.

“Ninampenda sana Profesa Muhongo, pia ni rafiki yangu, lakini kwenye hili, ajifikirie, ajitathimini na bila kuchelewa ninataka aachie madaraka,” alisema.

Kuhusu wizara, alisema imeshindwa kuisimamia TMAA na ujenzi wa smelters, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuweka utaratibu wa kusimamia makinikia.

“Wameshindwa kitu gani? Mbona wanasafiri hata kwenda laya. Wameshindwa kitu gani kuyasimamia haya makinikia yanapopakiwa hapa. Wanawauliza wale wahusika yanakwenda wapi?

“Kamishna wa madini anafanya nini? Waziri anafanya nini? Na kwa sababu hiyo basi, vyombo vya dola naomba viwachunguze baadhi ya watendaji wa wizara waliokuwa wanahusika na sekta ya madini.

“Ni kwa bahati mbaya nimeteua kamisha wa madini mpya wiki iliyopita, siwezi kumhukumu kwa hili, lakini yule ambaye amekaa kwa muda wa miaka minne, achunguzwe,” aliagiza.

Alisema ripoti hiyo imeonyesha kupotea kwa kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kusafirisha mchanga wenye madini, hivyo lazima hatua ziweze kuchukuliwa kwa wale wote waliohusika.

“Niliondoka na wenzangu kuteta kidogo kwamba, ripoti hii haiwezi kupita hivi hivi. Ripoti hii ikipita hivi hivi, tutakuwa watu wa ajabu, lazima nifanye kitu na mapendekezo yote ya kamati tumeyapokea na yamepita,” alisema.

Aliongeza: “Bodi ya TMAA nimeivunja kuanzia sasa na pili, Mkurugenzi wa TMAA namsimamisha kazi.”

Pia, alivitaka vyombo vya usalama kuwachunguza na kuwafuatilia wafanyakazi wa TMAA waliohusika ili wachukuliwe hatua za kisheria.

"Lazima hatua za kisheria zianze kuchukuliwa na zianze kuchukuliwa kuanzia leo. Hatuwezi tukawa na watu, ambao tumewasomesha, halafu wanafanya mambo ya kipumbavu kwa manufaa yao madogo, wakasahau manufaa mapana ya nchi yetu,” alisema.

Hivyo, aliviagiza vyombo vya dola na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kufanyakazi yao kwa wahusika wote wa TMAA kuanzia mkurugenzi.

Pia, aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kuanza kusimamia shughuli zote za madini kwa sababu vimekuwa vikijisahau.

Aliongeza: "Nimesikitishwa na  fedha nyingi zinazopotea, nimejiuliza maswali mengi, Kwa nini watendaji waliochaguliwa kusimamia na kusomeshwa na fedha za Watanzania wanafanya hivyo. Wanashindwa kudhibiti na kusimamia kazi waliyopewa ya kuhakikisha wanapima na kujua kiwango cha dhahabu kilichopo kabla ya kuruhusu kusafirishwa kwenda nje?"

Alisema Watanzania wanapoteza kiasi kikubwa cha fedha zinazotokana na  madini, ambacho kingeweza kuwasaidia kununua dawa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya hapa nchini.

“Bora wangekuwa wamesahau dhahabu tu kwenye mchanga, lakini cha ajabu wamesahau shaba, fedha, chuma, salpha. Haya yote watu wala hawajali,” alisema.

Rais Dk. Magufuli alisema kitendo hicho kinaumiza na kusikitisha, hivyo aliwaomba Watanzania wote kwa pamoja, kushikamana kukomesha hali hiyo.

Akizungumzia baadhi ya watu waliojitokeza kwa ajili ya kuvuruga jitihada za kamati hiyo, alisema kuna baadhi ya watu walihongwa fedha ili waweze kukwamisha uchunguzi huo.

“Kuna watu ambao walijitokeza kutaka kuingilia uchunguzi huu. Kwa bahati nzuri majina yao tunayo. Wapo wengine ambao mmewaona wenyewe walijitokeza hadharani baada ya kupewa fedha.

“Kuna mmoja anajiita profesa wakati ni daktari. Yeye alihongwa fedha na kuanza kuzungumza ambayo hayajui,” alisema.

Rais Magufuli alisema amesikia wengi wakibwatuka kwenye mitandao ya jamii kutokana na jeuri ya fedha walizopewa na waliowatuma.

“Ukishamuona mtu anabwatuka kwa suala, ambalo ni la kitaifa, ujue kabisa hawezi kuwa anazungumza bure, lazima atakuwa amepewa kitu,” alisema Rais Dk. Magufuli.


Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dotto Biteko, amepongeza uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli, katika sakata la mchanga wa dhahabu.

Rais Magufuli, jana, alitengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kutokana na sakata la mchanga wa dhahabu.

Akizungumza mjini hapa jana, Biteko, alisema kuwa Rais Magufuli, amechukua uamuzi sahihi baada ya tume aliyounda kubaini madudu.

Biteko, alimpongeza Rais Magufuli kwa kuchukua uamuzi huo kuwa, sekta ya madini iligubikwa na ukakasi kabla ya tume kutoa taarifa ya ufisadi kwa baadhi vigogo wa Wizara ya Nishati na Madini.

Mwenyekiti huyo alisema Rais Magufuli hakumuonea mtu katika uamuzi wake kwa kuwa amepata muongozo kutoka tume iliyoundwa kuchunguza sakata hilo.

“Nampongeza Rais kuchukua hatua haraka kwa viongozi na wahusika wote wa madini, hakumuonea mtu kwa wote waliochukuliwa hatua kwa sababu walishindwa kusimamia kikamilifu wizara,"alisema Biteko.

Biteko, ambaye ni Mbunge wa Bukombe-CCM, alisema nchi ilikuwa ikiibiwa madini mengi ambayo hayakuwa yakilipiwa mrabaha, hatua iliyosababisha taifa kupoteza mabilioni ya fedha.

Alisema fedha 'zilizotafunwa' kupitia mchanga wa dhahabu, zilikuwa na uwezo wa kupeleka maendeleo katika sekta mbalimbali kwa wananchi.

"Fedha iliyokuwa inapotea ingepatikana, ingeweza kuwasaidia Watanzania. Rais amethibitisha ni kiongozi asiyetaka mchezo,"alisema Biteko.

Alipoulizwa endapo kamati yake haikuwahi kubaini kuwepo kwa wizi huo, alisema: “Kilichokuwa kinatokea kwa kamati yetu ni kuletewa taarifa za uongo."

No comments:

Post a Comment