Wednesday 26 April 2017

NDIKILO: OPERESHENI SAKA MAJAMBAZI PWANI HAILENGI KUMNYANYASA MTU



Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

    MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, ameweka wazi kuwa, oparesheni inayoendelea kufanyika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga hazipo kwa ajili ya kumnyanyasa mtu.

    Amesema wananchi waache polisi na serikali ifanye kazi na doria ili waweze kuwapata wahalifu waliohusika katika matukio ya mauaji yaliyowahi kutokea.

    Mhandisi Ndikilo alieleza, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kuwa wananyanyaswa na polisi hao.

    Alibainisha kwamba, jamii ijenge ushirikiano na jeshi la polisi pamoja na serikali kwa kuendelea kuwataja wanaowadhania ni wahalifu au wauaji badala ya kuwanyooshea kidole askari polisi.

    Mhandisi Ndikilo, alisema matukio hayo ni ya kipindi kirefu yanayohusisha kuuwawa wenyeviti wa vijiji, vitongoji na askari polisi hivyo ni wakati wa kuachia vyombo vya dola vifanye kazi yake.

    “Kuna malalamiko nimefikishiwa kutoka kwa baadhi ya watu wakidai wananyanyaswa na polisi, hapana, niwaombe wananchi waliopo Kibiti na Rufiji ukiambiwa na polisi simama basi usimame, ukihojiwa basi jibu kuliko kukimbia “

    “Ukikimbia nyumba yako ,mji wako, unaweka alama ya kuuliza kuwa taarifa inazozipata polisi kupitia jamii yenyewe basi ni kweli, kama wewe sio mhalifu kwa nini ukimbie “alisisitiza .

    Mkuu huyo wa mkoa ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa, alielezea kwamba, oparesheni inayoendelea haitamwonea mtu yoyote kwani inafanywa kwa kuzingatia sheria.

    Mhandisi Ndikilo alisema ulinzi umeimarishwa zaidi na aliomba kama kunatokea tetesi ama malalalamiko yoyote lijulishwe jeshi la polisi na serikali ya mkoa ili itoe ufafanuzi wa kina.

    Nae kamanda wa polisi mkoani Pwani, kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga, alisema polisi linafanya kazi yake kwa kulinda amani,wananchi na mali zao.

    Alisema watapambana usiku na mchana hadi watakapohakikisha mtandao wa wahalifu unakamatwa .

    Lyanga alisema kuwa wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili viweze kufanya kazi zake vizuri.

No comments:

Post a Comment