Wednesday, 29 June 2016
MATANGAZO YA BUNGE SASA KURUSHWA 'LIVE' REDIONI
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema serikali kupitia mhimili wake wa bunge, ambao ndio ulipitisha kusitishwa utaratibu wa kurusha moja kwa moja matangazo yake kwenye televisheni, itaanza kurusha matangazo hayo kwa njia ya redio kuanzia kikao kijacho cha bunge.
Amesema matangazo hayo yataandaliwa na kurushwa na studio ya bunge, ambayo itayarusha kwa redio zote zilizosajiliwa na serikali, zikiwemo zile za kijamii, ambazo kitakwimu zinahudumia watanzania takriban milioni 17.
Waziri Nnauye alitoa kauli hiyo jana, jijini Dar es Salaam, alipohudhuria tafrija ya kuzindua studio maalumu ya kuandalia vipindi vya redio ya jamii ya COMNETA, iliyoko kwenye makao makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Alisema serikali ilitambua kuwa uamuzi wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya televisheni utaleta malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali kwa sababu ni mpya, lakini ilitoa uhuru kwa wadau kutoa mawazo juu ya maboresho yake.
“Hili suala ni jipya, ni uamuzi uliofikiwa na bunge la serikali ya awamu ya nne na serikali ilijua kuwa kutakuwa na malalamiko mengi, hivyo ikafungua milango kwa wadau kushauri bunge kuendelea na kazi ya maboresho ili kutokuminya uhuru wa habari,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa serikali iliangalia masuala mengi kabla ya kuamua kupitisha uamuzi huo, kubwa likiwa ni kupunguza matumizi ya rasilimali fedha na watu, ambapo baada ya bunge kuanzisha studio binafsi, vyombo vya habari havitatakiwa kupeleka waandishi Dodoma kwa ajili ya bunge kama inavyofanyika sasa.
Aidha, alisema baada ya maamuzi hayo, wawakilishi kadhaa wa vyombo vya habari walikutana na serikali na kutoa maoni kuwa, kama matangazo ya televisheni yana gharama kubwa, ni vyema serikali ikatoa nafasi kwa wananchi kupata moja kwa moja matangazo ya bunge lao kupitia radio, jambo ambalo serikali imeliridhia.
“Wadau mbalimbali walilalamika sana kuwa serikali inaharibu demokrasia. Serikali inajali sana uhuru wa kupata habari kama moja ya njia za kukuza demokrasia, hivyo kulikuwa na kutaendelea kuwepo marekebisho juu ya uamuzi huo ili vyombo vya habari vinufaike pamoja na wananchi na serikali,” alisema.
Pamoja na hilo, Nape alizungumza kuhusu umuhimu wa uzalendo na umakini kwa waandishi wa habari wa Tanzania kuwa, ni mambo makubwa ambayo kila mwanataaluma wa sekta ya habari anatakiwa kuyazingatia ili kutopotosha jamii kwa namna yoyote.
Alisema siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi la wanahabari kutoa taarifa tofauti na chanzo cha habari husika, jambo linalosababisha mkanganyiko kwa wananchi juu ya habari ipi ya chombo kipi waiamini kwa wakati husika.
“Kukosekana kwa uzalendo na umakini kunaweza kuleta madhara makubwa kwa taifa, hivyo waandishi hebu tuwe makini kwa sababu taaluma ya habari inaaminiwa na jamii kwa kiasi kikubwa na ni msaada mkubwa kwa serikali.
“Mfano mzuri magazeti manne (sio Uhuru) ya leo (jana), yalitoa takwimu tofauti kuhusu hatua ya Rais Magufuli kuteua Ma-DC, lakini chanzo kilikuwa kimoja yaani Katibu Mkuu Kiongozi, sasa sijui nini tatizo wakati kulitolewa taarifa ya maandishi,” alisema.
Alisema kukosekana kwa uzalendo kwenye sekta ya habari nchini kulijionesha kulipotokea uhalifu kwenye mapango ya Amboni mkoani Tanga, ambapo gazeti moja la hapa nchini liliandika kuwepo kwa magaidi wa Al-Shaabab, jambo ambalo halikuwa na kweli.
“Sasa gazeti la nyumbani linaandika magaidi wa Al-Shaabab yavamia Tanga, hata kama ni kweli, haifai kuandika hivyo, halafu kesho linaandika tena Al-Shabaab watulizwa na JWTZ, huu ni uchochezi kwa taifa dhidi ya hilo kundi, kwa hiyo tunatakiwa kutanguliza uzalendo,” alisisitiza.
Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda, alisema kuwepo kwa studio hiyo katika majengo ya chuo chake ni fursa kwa wanafunzi, hasa wa taaluma ya habari, kufanya mazoezi ya vitendo ili waje kuwa hodari na ushindani kwenye soko la ajira mara wanapohitimu.
Katika tafrija hiyo, Nape alikuwa mgeni rasmi, ambapo alizindua studio hiyo iliyoanzishwa kwa msaada wa UNESCO, ambao mwakilishi wake hapa nchini, Zulmira Rodrigues, alipata fursa ya kuhutubia na kuishukuru serikali kwa kutambua michango ya redio za jamii kwenye kusambaza habari na kukuza demokrasia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment