Wednesday 29 June 2016

KIKOSI CHAUNDWA KUWASAKA WAUAJI MWANZA NA TANGA


POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imeunda kikosi maalumu kitakachofanya uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika na mauaji ya Mwanza na Tanga.

Akizungumza na Uhuru  jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema kikosi hicho tayari kimeshaanza kufanyakazi ya kuwatafuta wale wote waliohusika na matukio hayo ya mauaji.

Alisema operesheni hiyo inaendelea vizuri na jitihada za kuwatafuta watu hao zinaendelea. Aliwahakikishia wananchi kwamba lazima watu hao watakamatwa.

“Wananchi kuweni na subira, tunawahakikishia kwamba watu wote waliohusika na mauaji hayo na kukimbilia Dar es Salaam, kwa ajili ya kujificha, tutawakamata na tutawashughulikia kweli kweli.

"Tunachowaomba ni kutoa ushirikiano kwa polisi pale mnapoona mtu au kikundi cha watu, ambao mnawatilia mashaka katika mitaa yenu.
Toeni taarifa ili watu hao wachukuliwe hatua mapema kabla hawajafanya uhalifu,” alisema Kamanda Sirro.

Huo ni mwendelezo wa kuwatafuta watu hao baada ya jeshi hilo kuwaua vinara  wawili  wa matukio ya mauaji katika mikoa ya Mwanza na Tanga.

Watuhumiwa waliohusika na mauaji hayo ni  Salumu Saidi (30) na  Mohamed Abdala, maarufu kama Abuu Seif, ambao walifariki dunia baada ya kufanya mashambulizi ya kurushiana risasi na polisi, kufuatia
kuzingirwa kwenye nyumba zao.

Mauaji yaliyotokea msikitini  Mwanza, yalifanyika Mei 18, mwaka huu, ambapo watu watatu waliuawa, ambao ni Imamu wa msikiti huo, Ferouz Elius, Mbwana Rajabu na Khamis Mponda, ambaye alikuwa dereva bodaboda.

Katika mauaji ya Tanga, yalitokea Mei 30, mwaka huu, watu wanane  waliuawa, wakiwemo Issa Hussein (50), Mkola Hussein (40), Hamis Issa (20), mtu mmoja aliyejulikana kwa  jina moja la Mikidadi(70), Mahamudi, ambaye ni mkwe wa Mikidadi(35), Issa Ramadhani(25), Kadiri(25) na Salumu, ambao walikuwa wachunga ng’ombe.

No comments:

Post a Comment