Wednesday 29 June 2016

WABUNGE WATAKA CUF IFUTIWE USAJILI

MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM), Munira Mustafa Khatib ameiomba serikali kukifutia usajili Chama cha CUF kutokana na wafuasi wake kufanya vurugu mara kwa mara visiwani Zanzibar.

Munira, alitoa ombi hilo kwa serikali jana, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza bungeni, akihoji kwa nini chama hicho kisifutiwe usajili kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo.

Alisema mara nyingi katika uchaguzi au matukio mengine ya kisiasa visiwani humo, CUF kimekuwa chanzo cha vitendo vya vurugu na kuwakosesha amani Wazanzibar.

Mbunge huyo alisema mara nyingi vurugu hizo zimekuwa zikiwaathiri wanachama na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni pamoja na kujeruhiwa, nyumba zao kuchomwa moto na mali zao kuharibiwa.

"Kila zinapotokea vurugu Zanzibar, waathirika wakubwa wanakuwa wanachama wa CCM. Hivi serikali kwa nini isikifutie usajili chama hiki ili amani iwepo?’’ Alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni alisema, suala la kufutiwa usajili kwa chama cha siasa lipo chini ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa hivyo hawezi kulitolea majibu.

Baada ya Masauni kujibu swali hilo, mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora, aliomba mwongozo wa Naibu Spika kutaka kujua kwa nini CUF isifutiwe usajili kutokana na kujihusisha na vitendo vya uvunjaji amani visiwani Zanzibar.

Lugora alisema kwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa yupo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ni vyema Naibu Waziri Masauni ajibu swali la Munira kwa nini chama hicho kisifutwe.

Alisema wafuasi wa CUF wamekuwa wakifanya vitendo vingi vinavyowaathiri wenzao wa CCM kisiwani Pemba, ikiwemo mauaji na uharibifu wa mali, hivyo anaomba muongozo wa bunge kuhusu jambo hilo.

Akijibu muongozo huo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson aliwaomba wabunge wampe muda aweze kupitia sheria za vyama vya siasa kabla ya kutoa majibu.

Alisema kwa mujibu wa kanuni ya 68(7), muongozo unaweza kutolewa papo hapo au baadaye, hivyo majibu ya muongozo huo atayatoa baadaye.

No comments:

Post a Comment