RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, jana aliandika historia mpya ndani ya ukumbi wa bunge, baada ya kushangiliwa kwa nguvu na wabunge, alipotambulishwa kwao na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kikwete alitambulishwa kwa wabunge kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali na majibu, ambapo kwa utaratibu wa kawaida, wageni wanaofika bungeni hutambulishwa baada ya kipindi hicho kumalizika.
Rais huyo mstaafu alifika bungeni kwa ajili ya kumsindikiza mkewe, Mama Salma Kikwete, ambaye jana aliapishwa kuwa mbunge wa kuteuliwa, kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni.
"Kabla ya kuendelea, naomba nimtambulishe mgeni aliyeko ambaye ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete,” alisema Spika Ndugai na kusababisha wabunge kulipuka kwa mayowe mengi ya kumshangilia.
Wabunge hao walimshangilia JK kwa kugonga meza kabla ya Spika Ndugai kuwataka wasimame ili kumpa Rais huyo mstaafu heshima anayostahili, ambapo walifanya hivyo.
Rais mstaafu Kikwete alitambulishwa baada ya mkewe Salma Kikwete kuapishwa kuwa Mbunge wa Kuteuliwa.
Wakati wa shamrashamra za kumshangilia JK, baadhi ya wabunge walisikika wakisema 'tumekumiss, tumekumiss' huku wengine wakisema apewe awamu nyingine ya kuongoza.
Wabunge wengine walitoa kali zaidi baada ya kutaka Kikwete aruhusiwe kuwahutubia, jambo ambalo lilishindikana kwa sababu za kikanuni.
Spika Ndugai alichagiza kwa kusema, katika historia ya Bunge, haijawahi kutokea mgeni kushangiliwa kama ilivyotokea kwa Rais mstaafu Kikwete na kuongeza kuwa, tukio hilo limevunja rekodi.
Baada ya muda, Spika Ndugai aliwasihi wabunge kunyamaza ili shughuli za bunge ziendelee.
Kikwete akiwa na wasaidizi wake pamoja na mwanawe Ali, waliondoka kupisha shughuli za bunge ziendelee.
Baadaye mchana, Rais mstaafu Kikwete aliandika kupitia mtandao wake wa twitter akisema: "Leo asubuhi nimeshuhudia kiapo cha mke wangu, Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete kuwa Mbunge wa Kuteuliwa Bungeni Dodoma.Ni zamu yangu kumuunga mkono."
Awali, Mama Salma Kikwete aliingia ndani ya ukumbi wa bunge baada ya kumalizika kwa wimbo wa taifa na dua, akiwa amesindikizwa na jopo la wabunge huku akishangiliwa na kupigiwa makofi.
Baada ya Mama Salma kumaliza kula kiapo na kuonyeshwa sehemu atakayokuwa akikaa huku akishangiliwa na wabunge, Spika Ndugai alisimama na kusema: “Nilitaka kuona mama anakaa wapi ili akisimama katika maswali nimwone kwani nataka leo nimpe nafasi aulize swali la kwanza."
No comments:
Post a Comment