Wednesday, 5 April 2017

MAKONDA AFICHUA UFISADI WA KUTISHA MRADI WA DMDP


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameibuka na kufichua ubadhirifu wa mabilioni ya fedha katika Mradi wa Maendeleo na Uboreshaji jijiji la Dar es Salaam (DMDP), ambapo zaidi ya sh. bilioni 7.5, ilikuwa zitafunwe na wajanja wachache.

Fedha hizo ni kati ya sh. bilioni 10, ambazo ilikuwa zitolewe kama fidia kwa wananchi waliopitiwa na miradi ya DMDP, hususan miundombinu na  uboreshaji wa huduma za kijamii katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke.

Kufuatia ufisadi huo, Makonda aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), kufanya uchunguzi mzito kuanzia kwa watendaji wa ofisi za serikali za mitaa, mpaka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali ndani ya wiki mbili.

Makonda alisema kati ya sh. bilioni 10, ambazo ziliingizwa kwenye miradi ya DMDP katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke, fedha ambazo zilipangwa kuporwa na mafisadi ni nyingi kuliko, ambazo zingeelekezwa katika miradi.

Hii ina maana kwamba, kati ya sh. bilioni 10, sh. bilioni 7.5 zingeliwa na watu, ambapo sh.bilioni 2.5 pekee ndizo zingeelekezwa katika ulipaji fidia.

Makonda alisema vitabu 10, vya uthamini wa miradi ya DMDP, viliwasilishwa kwake ili aweze kuvipitisha, ambapo kati ya vitabu hivyo, vitabu vinane alibaini vimekiuka utaratibu.

“Wilaya za Ilala na Temeke  ndiyo zimebainika kuwa na ukiukwaji mkubwa  katika uthamini, ambapo shilingi bilioni 6.6, ilikuwa zilipwe kwa uthamini hewa au watu wasio stahili,”alisema Makonda.

Alisema Kinondoni ilibainika na kiasi cha fedha hewa sh. bilioni 1.8, ambazo zilitakiwa kulipwa kinyume cha sheria.

Akizungumzia njia, ambazo watendaji hao walikuwa wakitumia kuiba fedha za umma, Makonda alisema wakati anapitia vitabu hivyo vya uthamani, alibaini kasoro nyingi, ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya uthamini kutokuwa na majina ya watu waliotakiwa kulipwa fidia au kuandikwa jina moja.

“Pia, kuna mihuri tofauti na kuna watendaji wengine wametia saini hati za wilaya nyingine. Mfano mtendaji wa Temeke, anasaini hati ya Kinondoni wakati hakuna utaratibu huo,”alisema Makonda.

Alisema katika hali ya kushangaza, kuna kampuni za usafirishaji mafuta kwa njia ya mabomba (hakuzitaja), ziliingizwa kama kampuni za uthamini.

“Yaani kampuni ambayo ina ujuzi wa kusafirisha mafuta inapewa kazi ya kuthamini ardhi na mali? Ukiangalia katika orodha ya kampuni katika orodha ya uthamini hiyo, kampuni haipo,” alibainisha.

Alisema kuna baadhi ya watu kutoka kampuni za uthamini, waliingia makubaliano na wananchi katika suala la malipo kwa kuongeza thamani ya uthamini wa mali zao.

“Walikuwa na makubaliano kwamba, mwananchi anaongezewa thamani ya kiwanja au nyumba yake ili watendaji hao wapate cha juu. Hili haliwezekani,”alibainisha Makonda.

Katika hali ya kusikitisha, Makonda alisema kuna taarifa inaonyesha shimo la kutupia taka limethaminiwa na kutakiwa kulipwa fidia ya sh. milioni nne.

“Nawaagiza TAKUKURU ndani ya wiki mbili wafanye uchunguzi kutoka ngazi ya chini hadi Ofisi ya Mthamini Mkuu na hao watakaobainika  wachukuliwe hatua haraka,”aliagiza.

Makonda alisema zaidi ya dola milioni 300,  zilitolewa kwa ajili ya mradi wa DMDP  na kwamba, zingetumika kwa vipindi vitano, ambapo Rais Dk. John Magufuli aliagiza zitumike kwa umakini  mkubwa.

“Fedha hizi zaidi ya shilingi bilioni saba, ilikuwa ziishie katika mikono ya watu wachache, wakati ilitakiwa zitumike kwa ajili ya kuboreshea miundombinu yetu, kununua dawa  kwa ajili ya wananchi,”alionya mkuu huyo wa mkoa.

Alisema tayari ametoa maelekezo kwa watendaji wakuu wa halmshauri katika kulifuatilia suala hilo na kwamba, ubadhirifu huo aliushtukia baada ya kufanya uchunguzi na timu yake kisha kuagiza uhakiki ufanyike ndipo yalipobainika madudu hayo.   

No comments:

Post a Comment