Wednesday, 5 April 2017

TRA YAKUSANYA TRILIONI 10.87/-


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema katika malengo ya mwaka wa fedha 2016/2017 ya kukusanya sh. trilioni 15.1, kufikia Machi, mwaka huu, imeshakusanya sh. trilioni 10.87.

Imesema katika muda uliobaki, ambao ni miezi mitatu (Mei-Julai), ina uhakika wa kufikia lengo la makusanyo kutokana na mipango iliyojiwekea, hasa kwenye ukusanyaji wa kodi ya majengo.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa makusanyo hayo, kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.99, ikilinganishwa na makusanyo ya miezi tisa ya mwaka wa fedha uliopita wa 2015/2016, ambapo zilikusanywa sh. trilioni 9.88.

Kayombo alisema kwa takwimu za makusanyo ya Machi, mwaka huu, jumla ya sh. trilioni 1.34, zilipatikana, ambalo ni ongezeko la asilimia 2.23, kwenye makusanyo ya Machi, 2016.

Alisema kutokana na mafanikio hayo, TRA inaendelea kuwashukuru wananchi kwa kuelewa umuhimu wa kulipa kodi kwenye maendeleo ya taifa, huku pia akikiri kuutambua mchango wa vyombo vya habari.

Kuhusu hatua zinazofuata ili kukusanya kodi katika muda uliobaki, alisema tayari wametoa viwango vya kodi za majengo kwenye maeneo, ambayo hayakufanyiwa tathimini katika kipindi kilichopita.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wamiliki wa majengo katika maeneo mbalimbali nchini, kufika ofisi za TRA kwenye maeneo yao au kwa kutembelea tovuti ya mamlaka hiyo ili kuangalia viwango stahiki.

"Vilevile tunasisitiza matumizi ya EFD kwenye biashara na uhakiki wa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), kwenye mikoa ya Arusha, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Morogoro, " alisema.

Aliongeza kusisitiza kuwa, wakazi wa Dar es Salaam, ambako tayari uhakiki huo umepita, bado wanayo fursa ya kufanya hivyo kwenye ofisi zote za TRA, hivyo wajitokeze ili kuepuka usumbufu.

"Tuseme tu kwamba bila uhakiki wa TIN, hutaweza kulipia kodi yoyote, ikiwemo kufufua leseni yako ya udereva, hivyo hili zoezi ni muhimu, " alisema.

Alisema ofisi zote za TRA ziko wazi kwa mwananchi mwenye maulizo, hivyo wasisite kuzitembelea wakati wowote, siku na saa za kazi.

Ni takriban miezi tisa sasa, TRA hawajatoa taarifa za makusanyo ya kila mwezi, utaratibu waliokuwa wakiutumia awali, jambo lililotolewa ufafanuzi jana, kuwa wameamua kubadili kutoka kila mwezi na kufanya kila baada ya robo ya mwaka wa fedha.

No comments:

Post a Comment