Wednesday 5 April 2017

UVCCM YAMSHUKIA SUMAYE


UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, atazeeka na kuwa kikongwe, iwapo ataendelea kusubiri na kuota iko siku upinzani utaiondoa CCM madarakani.

Pia, umoja huo umesisitiza kuwa, Sumaye na wenzake walioko upinzani hawana uaminifu wa kutosha katika jamii, misuli na ubavu wa kumng'oa Rais Dk. John Magufuli katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Msimamo huo ulitolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipotakiwa kutoa maoni yake, kufuatia kauli ya Sumaye, aliyoyatoa mkoani Geita, akidai kuwa serikali ya Rais Dk. Magufuli imeshindwa mapema kazi ya kuongoza na upinzani utamuondoa madarakani ifikapo mwaka 2020.

Shaka alisema Sumaye na viongozi wa upinzani wamebaini kuwa, Rais Dk. Magufuli ndani ya mwaka mmoja na nusu wa serikali yake, ameonyesha umakini na kuinyoosha nchi, amerudisha heshima, anasimamia misingi ya nidhamu kazini, utawala bora, uwajibikaji, ukusanyaji kodi na pia anapambana vikali na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Alisema kundi la mafisadi, wabadhirifu wa mali za umma, wakwepa kodi na ushuru, wapiga dili na baadhi ya watu waliozoea kuiba mali za umma, wanailalamikia kasi hiyo na kuiona ni kizingiti katika kufanikisha malengo yao.

"Sumaye anaota akikumbuka zama za uuzaji holela wa viwanda na mashirika ya umma kwa bei ya kutupa irejee. Amezoea kuona ardhi yenye rutuba akwapue. Zama hiyo imepita na haitarudi, mafisadi na jamii yao wanamuona Dk. Magufuli amekwamisha ulaji wao na sasa wanapayuka hovyo mitaani,"alisema.

Aidha, Shaka alisema nchi yoyote duniani unapomalizika uchaguzi mkuu mmoja, wananchi na vyama vya siasa hufanya kazi, huzalisha mali na sio kuendelea kupiga porojo za kisiasa kwenye majukwaa kama anavyofanya
Sumaye na wenzake.

"Huu sio wakati wa kampeni, Sumaye na kundi lake ikiwa wana maneno ya kupayuka, wayahifadhi vifuani ili kampeni zitakapofika waseme, wananchi watapembue mchele na pumba. Asijifanye mbashiri na kupiga ramli kwani ni sawa na kuandikia mate wakati wino upo,"alisema.

No comments:

Post a Comment