Thursday 6 April 2017

WATUHUMIWA MAUAJI YA DK. MVUNGI WAKIRI KUSHIRIKI TUKIO HILO

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa kuwa washitakiwa saba wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, walikiri kushiriki tukio la uvamizi nyumbani kwake, ambapo alijeruhiwa kwa kukatwa mapanga, likiwemo la kichwani sehemu ya utosini.

Aidha, imeelezwa kuwa mshitakiwa Paulo Mdonondo, aliyekuwa miongoni mwa watuhumiwa wa ujambazi waliovamia nyumbani kwa Dk. Mvungi, ambaye alikuwa na kazi ya kulinda majirani wasisogee eneo hilo akiwa amebeba jiwe, alipewa mgawo wa sh. 30,000, ikiwa sehemu ya fedha zilizokuwa zimeibwa kwenye tukio hilo.

Pia, imeelezwa kuwa mapanga matano yaliyotumika katika tukio hilo yaliwekwa katika kiroba na kufichwa na mshitakiwa Msingwa Matonya, kwenye kichaka kilichoko Kibaha Maili Moja, mkoani Pwani, karibu karibu na Hoteli ya Njuweni.

Hayo yalidaiwa jana, mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, alipokuwa akisoma maelezo ya mashahidi 30 na vielelezo 13, vinavyotarajiwa kutolewa kama ushahidi katika kesi hiyo, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Mdonondo, Matonya,  Chibago Magosi, Mianda Mlewa au White, Longisho Losingo, Juma Mangungu na John Mayunda, ambao wanadaiwa kumuua Dk. Mvungi,  Novemba 3, 2013, eneo la Msakuzi, Mbezi.

Inadaiwa washitakiwa hao walikiri kutenda kosa hilo katika maelezo yao ya onyo.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, watu tisa wanaosadikiwa kuwa majambazi, wakiwa vifua wazi huku wamejifunika nyuso zao kwa vitambaa, walivamia nyumbani kwa Dk. Mvungi wakiwa na mapanga.

Katika ushahidi uliosomwa mahakamani hapo, inadaiwa watuhumiwa hao walipiga baruti kwa lengo la kuwatisha wenye nyumba, ambapo Dk. Mvungi na mkewe waliamka na kila mmoja kupita upande wake kwenda kuangalia kilichotokea.

Inadaiwa kuwa Dk. Mvungi alikutana na watuhumiwa akiwa maeneo ya jikoni, ambapo walimjeruhi kwa kumkata na mapanga, likiwemo la kichwani sehemu ya utosini na baada ya hapo, walimfuata mkewe wakimlazimisha awape fedha.

Akisoma ushahidi wa mke wa marehemu Dk. Mvungi, Anna  Mvungi, alidai kuwa siku hiyo, saa saba usiku, wakiwa wamelala, walisikia vishindo kama mabomu, hivyo alimwamsha mumewe, ambaye alienda upande wa kushoto na yeye alienda wa kulia.

Katika ushahidi wake, alidai kuwa watuhumiwa hao wa ujambazi walikuwa vifua wazi na kichwani walijifunika na vitambaa huku wakiwa wamebeba mapanga na kigoda walichokuwa wamechukua jikoni.

Inadaiwa walimwamuru awape fedha, hivyo aliwapa sh. milioni mbili, kompyuta mpakato, bastola na funguo za milango. Pia, inadaiwa walikwenda chumbani kwao, ambako walichukua bastola. Aidha, aliitambua simu aliyokutwa nayo Chibago kuwa ni ya mumewe.

Ushahidi mwingine ni wa Elia Alex, ambaye anadai aliwaona watuhumiwa hao wanne na Dk. Mvungi, alijeruhiwa kwa kukatwa maeneo ya kichwani.

Katika ushahidi mwingine, unadai kuwa mke wa Dk. Mvungi aliweza kuwapatia sh. milioni mbili, ambapo pia waliweza kuchukua simu mbili , kompyuta mpakato, bastola, funguo za milango na simu ya msichana wa ndani.

Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao walifanikiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo baada ya kuvunja milango kwa kutumia mawe na mmoja wa washitakiwa Mdonondo, alikaa mlangoni akiwa na mawe kwa lengo la kukabiliana na majirani watakaojitokeza kutoa msaada.

Ushahidi huo unadai kuwa, baada ya hapo, watuhumiwa hao waliondoka na kwenda kugawana vitu walivyochukua, ambapo Mdonondo alipata mgawo wa sh. 30,000 kwa kuwa alikaa nje.

Inadaiwa baada ya kufanya uhalifu huo, polisi walipata taarifa za kiinterejensia juu ya uwepo wa mshitakiwa Mayuga, aliyekutwa maeneo ya klabu ya Yanga, ambapo walifanikiwa kumkamata.

Inadaiwa mshitakiwa huyo alikiri kushiriki katika tukio hilo la ujambazi na kueleza bastola na risasi zilizochukuliwa nyumbani kwa Dk. Mvungi ziko maeneo ya Kiwalani, anapoishi, hivyo walikwenda huko na kufanikiwa kukuta bastola hiyo ikiwa juu ya ukuta wa tofali linalogusa bati na risasi 21.

Pia, inadaiwa ulikutwa mfuko wa plastiki ukiwa na unga wa baruti, waya mbili na utambi  na alipohojiwa mshitakiwa huyo alidai alipewa vitu hivyo aweke na mwenzake aitwaye Ahmed .

Inadaiwa baada ya hapo, polisi walifanya mitego na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote, ambapo Chibago alikutwa na simu iliyotambuliwa kuibwa nyumbani kwa Dk. Mvungi.

Pia, inadaiwa watuhumiwa hao walifanya uvamizi huo baada ya kupata taarifa kutoka kwa mlinzi wa Dk. Mvungi kwamba, kuna fedha.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Wakili Mwita alidai wanatarajia kuita vielelezo 13, vikiwemo ramani ya eneo ya tukio, ripoti ya daktari kuhusu chanzo cha kifo cha Dk. Mvungi, bastola, mapanga matano , hati za utambuzi na ukamataji  na maelezo ya onyo ya washitakiwa hao.

Hakimu Simba aliwaeleza washitakiwa hao kwamba, wataendelea kukaa rumande kusubiri kesi kusikilizwa Mahakama Kuu.

Washitakiwa waliposomewa shitaka hilo kwa mara ya kwanza, hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza na jana, walisomewa maelezo hayo baada ya shauri hilo kusajiliwa Mahakama Kuu.

No comments:

Post a Comment