RAIS Dk. John Magufuli amewaapisha viongozi aliowateua
kushika nyadhifa mbalimbali, wakiwemo makatibu wakuu, naibu katibu mkuu, mabalozi
na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao, ilifanyika jana,
Ikulu, Dar es Salaam, ambapo ilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan.
Walioapishwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo na Profesa Kitila Mkumbo, ambaye ameteuliwa
kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Viongozi wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ave Maria Semakafu; Baraka Luvanda aliyeapishwa
kuwa Balozi wa Tanzania nchini India na Sylvester Ambokile, aliyeapishwa kuwa
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Aidha, Dk. Magufuli amemwapisha Charles Kichere kuwa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo baada ya kuapishwa,
viongozi hao walikula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, kilichoongozwa
na Katibu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha.
Akizungumza baada ya kuapishwa kwa viongozi hao, Makamu
wa Rais Samia, aliwapongeza kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo na kuwataka
kufanyakazi kwa kutanguliza maslahi ya Taifa na kwa kuzingatia sheria na
taratibu zilizowekwa.
“Tutawapa ushirikiano wote mtakaouhitaji ili kufanikisha
kazi zenu, lakini na nyinyi msituangushe. Kichere tunakutegemea ukaimarishe
ukusanyaji wa mapato pale TRA na pia ukawaambie maofisa wako na mameneja wa
mikoa, waache kutoa kauli za kuigombanisha serikali na wafanyabiashara,
wakusanye kodi kwa kufuata sheria na taratibu na pia wawe na lugha nzuri.
“Profesa Kitila Mkumbo, tunategemea utaongeza msukumo
kutatua matatizo ya maji, utasaidia kufanikisha kampeni ya kumtua mama ndoo ya
maji kichwani, Watanzania wapate maji safi na salama, ”alisema Makamu wa Rais.
No comments:
Post a Comment