Thursday 6 April 2017

MCHUMI BOT ASEMA DENI LA TAIFA LINAVUMILIKA





TANZANIA bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje kwa wakati.

Hiyo ni kutokana na tathmini iliyofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ilionyesha thamani ya sasa ya jumla ya deni la Taifa kwa Pato la Taifa, ni asilimia 34.2, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56.

Tathmini hiyo iliyofanywa Novemba, 2016, inaonyesha kuwa,  kwa upande wa thamani ya sasa ya deni la nje pekee kwa Pato la Taifa, ni asilimia 19.9, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40.

Kwa upande wa thamani ya sasa ya  deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150 na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani, ambayo ni asilimia 145.3, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250.

Kutokana na tathmini hiyo, imeelezwa kuwa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani, umefikia asilimia 11.5, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 7.8, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Mchumi kutoka BoT, Lusajo Mwankemwa, alipozungumza na Uhuru, kuhusu mwenendo wa deni la taifa, baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu ukubwa wa deni hilo.

Alisema ulipaji wa deni la Taifa hauangalii ukubwa wa deni lililopo bali kadri deni linavyoiva, tofauti na inavyoaminiwa na wananchi wengi kutokana na yanayosemwa na baadhi ya wanasiasa bila kuwa na utafiti.

Mchumi huyo alisema hali ilivyo sasa, sehemu kubwa ya deni la Taifa linaiva kwa kipindi cha muda mrefu, hivyo kwa wastani wa deni lililopo sasa, litaiva katika kipindi cha miaka isiyopungua 11.9.

"Hali hii inaashiria kwamba, athari zake kwenye bajeti ziko chini sana," alisisitiza.

Aidha, alisema serikali imekuwa ikilipa madeni ya nje na ndani kwa mujibu wa mikataba, ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Desemba 2016, serikali ilitumia jumla ya sh. bilioni 2,570.1, kulipia madeni ya ndani na nje yaliyoiva.

"Kati ya kiasi hicho, malipo ya deni la ndani ni shilingi bilioni 1,822.3 na deni la nje ni shilingi bilioni 747.8 na malipo ya deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji ya shilingi bilioni 1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi bilioni 455.2," alifafanua Lusajo.

Pia, alisema kutokana na muundo wa deni la Tanzania, ambao sehemu kubwa ya madeni yake yanaiva kwa muda mrefu, kuanzia miaka mitano hadi 50, upimaji wa deni la Taifa huangaliwa kwa kutumia thamani ya sasa ya deni.

"Badala ya kutumia thamani halisi ya deni, wachumi tunatumia thamani ya sasa ya deni, hali inayowezesha tathmini iweze kufanyika kwa madeni yanayoiva kwa muda mrefu, kinyume na thamani halisi ya deni kwa pato la Taifa, ambayo inaangalia hali ya deni kwa muda mfupi.

"Kwa kuzingatia hali hiyo, vipo viashiria mbalimbali, ambavyo vimetumika na vilikubalika kimataifa katika upimaji wa uhimilivu wa deni la Taifa kuanzia mwaka 2015 hadi 2036," alisema mchumi huyo.

Aliongeza: "Kwa kuzingatia vigezo hivyo, uwiano wa deni lote la ndani na nje kwa thamani ya sasa kwa pato la Taifa kwa mwaka 2015/2016, Kenya ilikuwa asilimia 45.6, Tanzania asilimia 34.2, Uganda asilimia 24.1 na Rwanda asilimia 22.7. 

"Vile vile, uwiano wa deni la nje kwa thamani ya sasa kwa Pato la Taifa, Kenya ilikuwa asilimia 19.4, Tanzania asilimia 19.9, Uganda asilimia 10.7 na Rwanda asilimia 17.3, ambavyo vyote bado viko chini ya ukomo," alisema.

Lusajo alisema masuala yanayohusu uchumi ni ya kitaalamu zaidi na kwamba, yanahitaji ufuatiliaji wa mambo, kama yanavyotolewa na BoT kwa njia mbalimbali, hivyo ili mwananchi aepuke kudanganywa, ni vema akafuatilia na kujiridhisha badala ya kuzungumza jambo bila kuwa na ufahamu nalo.

No comments:

Post a Comment