Saturday, 11 June 2016

NIDA KUTOA NAMBA YA UTAMBULISHO KWA KILA MTANZANIA


MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeanza mpango wa kutoa namba ya utambulisho kwa kila mtanzania, ili kujua idadi ya Watanzania wanaoishi nchini.

Mpango huo utakwenda sambasamba na utoaji wa vitambulisho vipya, ambavyo vitakuwa na saini ya mtoaji na mpokeaji .

Akizungumza Dar es Salaam, jana, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi wa NIDA, Rose Mdami, alisema vitambulisho hivyo vitasaidia kuleta usalama katika nchi.

Alisema ifikapo Desemba 31, mwaka huu, kila mtanzania anatakiwa awe amepata namba ya utambulisho huku mchakato wa kuandaa vitambulisho vipya ukiendelea.

Rose alisema wapo baadhi ya Watanzania, ambao walipata vitambulisho hapo awali, lakini vitaendelea kutumika kama kawaida kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

Alisema  tayari wameazima mashine 5,000 kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambazo zitawapa taarifa mbalimbali kwa ajili ya utoaji wa vitambulisho vipya.

Rose alisema kwa siku wana mpango wa kuandikisha wananchi 20,000, ambapo lengo ni kuwapatia vitambulisho Watanzania milioni 22.

Hata hivyo, alisema mpango huo wa utoaji wa namba ya utambulisho kwa kila Mtanzania, utasaidia kugundua wafanyakazi hewa waliopo sehemu mbalimbali.

Alisema mpango huo unatarajiwa kuanza Agosti, mwaka huu, sehemu za kazi, hivyo kila mfanyakazi anatakiwa apate namba hiyo ya kumjulisha kuwa yeye ni mfanyakazi wa sehemu alipo.

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vyao kwa ajili ya kuchukua namba za utambulisho, kwa ajili ya faida yao na nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment